Home Habari NYALANDU ‘KUWAVUA GAMBA’ WENGI CCM

NYALANDU ‘KUWAVUA GAMBA’ WENGI CCM

527
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

UAMUZI wa Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu wa kujiuzulu ubunge na nafasi zote ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umetajwa kukishtua chama hicho na kuchukua hatua za kufukuza makada wengine wenye makandokando au wajivue gamba wenyewe. Dhana ya ‘kujivua gamba’ iliasisiwa na Halmashauri Kuu (NEC) chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete mwanzoni mwa kipindi chake cha utawala wake.

Kujivua gamba kulilenga kukisafisha chama ili kujitenga na kashfa mbalimbali zilizoitikisa nchi kama Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Meremeta, TanGold, Mwananchi Gold, Deep Green Finance na kashfa nyininezo.

Sasa ni dhahiri kwamba kujiuzulu kwa  Nyalandu, ambaye alitangaza dhamira yake ya kujiunga na chama kikuu cha upinzani — Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kutawalazimisha waliogoma kujivua gamba kufukuzwa ndani ya CCM.

Kumekuwa na mgongano wa maelezo kuhusu Nyalandu ambaye alisema kuwa alimwandikia barua ya kujiuzulu ubunge Spika wa Bunge, Job Ndugai, lakini taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Spika, ilibainisha kuwa Nyalandu alikuwa tayari amefukuzwa uanachama na CCM.

Spika Ndugai alisema kwamba alikwisha mtaarifu kwa barua Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), na kumjulisha kwamba Jimbo la Singida Kaskazini liko wazi.

Hili linazua maswali kuwa kuna jambo CCM wanalificha. Nyalandu mwenyewe aliandika kwenye mtandao kwamaba hajawahi kuitwa na kuhojiwa na kamati yoyote ya CCM na au kuandikiwa barua ya kumvua uwanachama.

Lakini alipohojiwa na Rai kuhusu Nyalandu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, hakuweza kutamka bayana kama Nyalandu amewahi kujadiliwa na Kamati ya Maadili na Nidhamu ya Chama, bali alitoa wito kwa makada wa chama hicho ambao wanaojiona wamejichafua, ni vema wajiondoe mapema kama alivyofanya Nyalandu.

“Wale watakaokidhoofisha chama, na wote wenye makandokando ya kukosa uadilifu, wanaokifanya chama kinuke mbele ya wananchi, ama waondoke sasa kama alivyofanya Nyalandu au tutawafagia.

“Tayari serikali inafanya uchunguzi wa ushiriki wa baadhi ya watu ambao wengine ni wanachama wetu, kwenye maskendo makubwa  mbalimbali, uchunguzi huo unaendelea vizuri. Watakaobainika kuwa wameshiriki katika vitendo ambavyo ni kinyume na kanuni ya maadili ya uongozi ya chama, au wamevunja sheria za nchi, wameenenda na kutenda kwa hila, vikao vya chama vitachukua hatua kali na stahiki dhidi yao.

“Nikisema hatua kali inajumuisha kufukuzwa uanachama. Chama kitachukua hatua kali ikijuimuisha kufukuzwa chama.

“Mambo haya wanachama wa CCM wanapenda mno, kwa sababu haya mambo ya haki, uadilifu, unyenyekevu, mambo ya kuchukizwa na rushwa ndio tunayopigania sasa. Kupinga ubadhirifu wa mali za umma ndio mambo ambayo yanatutambulisha sisi kama wanachama wa CCM. Hivyo hatuwezi kukubali kiongozi mmoja achafue taswira ya CCM hilo haliwezekani,” alisema.

Aidha, maamuzi hayo ya CCM yanatajwa kuwaweka rehani baadhi ya makada wake wanaodaiwa kuchunguzwa kwa tuhuma mbalimbali kama vile rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Baadhi ya makada hao ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Profesa Anna Tibaijuka.

Makada hao mapema mwaka huu, walihojiwa na Kamati  Ndogo ya Maadili ya CCM, chini ya Mwenyekiti wake Philip Mangula, kwa tuhuma za kupokea mgawo wa fedha za Escrow kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira, licha ya kutoa maelezo ya kina kuhusu walivyopokea fedha hizo, inaelezwa kuwa kila mmoja alifunguliwa faili kwenye Idara ya Maadili ya CCM.

Profesa Tibaijuka ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne, alipokea Sh bilioni 1.6, Chenge naye akipokea kiasi kama hicho, huku Ngeleja akipokea Sh milioni 40.4.

Chenge na Ngeleja, wote ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC). Chenge alituhumiwa katika kashfa ya ununuzi wa rada na nwaka 2007 alilazimika kujiuzulu uwaziri wa Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu, kama ilivyokiwa ikiitwa wakati ule.

Chenge ni msomi aliyehitimu Shahada ya Umahiri wa Sheria, Chuo Kikuu cha Havard, Marekani, na alikuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali aliyetumikia Serikali kwa muda mrefu zaidi kuliko watangulizi wake.