Home Latest News SERIKALI NA MIKAKATI YA KUIMARISHA SEKTA YA MIFUGO

SERIKALI NA MIKAKATI YA KUIMARISHA SEKTA YA MIFUGO

229
0
SHARE
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akizungumza wa wafugaji wa Kijiji cha Mperani kilichopo wilayani Mkinga mkoani Tanga.

NA AMINA OMARI, TANGA

SERIKALI imekuwa ikiendesha zoezi la upigaji chata (alama) mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambapo lengo kuu ikiwa ni kutambua idadi kamili ya mifugo yake.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwapo takwimu zinazoonyesha kuwa nchi ya Tanzania ina idadi kubwa ya mifugo huku sekta hiyo ikiwa bado haijatoa mchango mkubwa wa kiuchumi kwa kuwa asilimia kubwa ya wafugaji wanafanya ufugaji wa kiholela huku baadhi ya mazao yatokanayo na mifugo hiyo yakishindwa kuingia kwenye soko kutokana na kutokuwa na ubora.

Hivi karibuni Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amefanya ziara mkoani Tanga kujionea namna ambavyo zoezi la uwekaji alama linavyoendelea kuzungumza na wafugaji pamoja na wadau wa sekta hiyo.

Anasema Tanzania ina utajiri mkubwa wa mifugo barani Afrika kwani ni nchi ya tatu kwa utajiri wa mifugo ikizifuatia nchi za Sudan na Ethiopia, lakini bado sekta hiyo imekuwa haijaweza kuchangia ipasavyo katika pato la Taifa.

“Kwani takwimu za kisayansi zinaonyesha kuwa, Tanzania ina mifugo takribani milioni 28 ambapo asilimia 97 ya mifugo yote hiyo ni mifugo ya asili huku idadi ndogo ikiwa ni mifugo ya kisasa,” anasema Naibu Waziri Ulega.

Anasema hivyo kukamilika kwa zoezi hilo kutaweza kutoa taswira halisi wakati huu ambapo nchi inatekeleza sera ya viwanda kwani itasaidia kutoa mwanga wa uwekezaji mkubwa katika sekta ya mifugo.

“Tunahitaji uwekezaji wa viwanda kwa ajili ya kuchakata nyama pamoja na bidhaa zitokanazo na mifugo hivyo ni lazima kuhakikisha tunakuwa na mifugo yenye ubora,” alisema Naibu Waziri.

Hivyo anasema iwapo hakuna hatua za haraka zitakazoweza kuchukuliwa ikiwamo kufanya udhibiti wa mifugo yetu kwa sasa tunaweza kuimarisha mifugo ya wenzetu.

Waziri Ulega anasema zoezi hilo litasaidia  kutambua uingiaji wamifugo kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa wakiingia kwa wingi katika ardhi ya nchi yetu kwa ajili ya kutafuta malisho.

Anasema kwani mara nyingi ifikapo wakati wa kiangazi malisho yanapokuwa haba ndipo wafugaji huanza kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho.

“Changamoto kubwa ipo katika maeneo ya mipakani ambapo ndipo wafugaji hutumia fursa hiyo kuingiza mifugo nchini na wafugaji wa nchi kuipeleka nje ya nchi kwa kisingizio cha kutafuta malisho,” anasema Ulega.

Licha ya mkakati huo bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maeneo ya malisho pamoja na mitamba bora kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.

Hivyo Waziri Ulega anasema ili kumaliza tatizo la malisho Serikali inatarajia kuzirejesha ranchi zote zilizo binafsi kwa watu binafsi na kushindwa kuziendeleza na kuzigawa kwa wafugaji.

Anasema lengo la kuchukuwa ranchi hizo ni kusaidia kumaliza changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji kugombania maeneo ya ardhi kwa ajili ya malisho na kilimo.

Hivyo anasema Serikali imeamua kuja na mpango huo ili kuepusha wafugaji wetu hususani wale waishio mipakani kwenda kwenye malisho ya mifugo yao katika nchi jirani.

“Tutachukuwa mapori yote ambayo wamiliki wake wameshindwa kuyaendeleza na kuyagawa kwa wafugaji ili waachane na ufugaji wa kuhamahama ambao umekuwa hauna tija kwao,” anasema Naibu Waziri.

Anaongeza kuwa utaratibu huo utakapokamilika utasaidia wafugaji hapa nchini kufuga kwa kisasa na kuachana na kufuga kiholea ikiwamo kumaliza migogoro baina yao na wakulima.

Katika hatua nyingine Waziri Ulega anawataka watendaji kuimarisha mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yote ili kuepuka migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

“Iwapo mtatenga maeneo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi basi migogoro baina ya wakulima na wafugaji itaweza kuwa historia ndani ya nchi hii, kwani kila mtu ataweza kufanya shughuli zake bila usumbufu,” anasema Waziri huyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, akizungumzia changamoto za ufugaji mkoani humo, alisema ni pamoja na baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kupakana na hifadhi ya Mkomazi.

“Hifadhi ile imepakana na mto Mkomazi ambao ndio unategemewa na wanyama walioko hifadhini pamoja na mifugo hivyo hapo ndipo penyechangamoto ya mifugo kuchanganyika na wanyama wa hifadhi,” anasema RC Shigela.

Anasema changamoto hiyo ya ukosefu wa malisho, inachangia wafugaji wengi kukimbilia nchi jirani ya Kenya kutafuta maeneo ya malisho.

Akizungumzia changamoto ya mitamba bora, Naibu Waziri huyo anasema Serikali imejipanga kuagiza mitamba 600 kutoka nje ya nchi na kuisambaza nchini kote.

Anasema lengo la Serikali ni kuhakikisha kupitia mitamba bora itakayozalishwa na vituo vyetu vya nchini na itakayoagizwa kutoka nje kusaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa kutoka lita mil mbili kwa mwaka hadi kufikia lita mil 3.8.

“Tutahakikisha wafugaji wetu wa ngombe wa maziwa wanafaidika na ufugaji huo kwa kuwasaidia kuongeza uzalishaji lakini pamoja na kuimarisha masoko ya ndani na nje,” amebainisha.

Anasema kupitia mpango wa Tanzania Livestock Master Planning (TLMP), tunatarajia kufanya maboresho makubwa katika sekta ya mifugo na kuifanya yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa malisho katika kipindi cha kiangazi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Mkoa wa Tanga, John Bwire, ameiomba Serikali kuzijengea uwezo taasisi zake za utafiti ili waweze kuja na suluhisho la changamoto hiyo.

Anasema taasisi hiyo ina uwezo wa kutafiti mbegu bora ya nyasi atakayoweza kutoa malisho mengi na mfugaji kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi ya malisho kwa kipindi cha kiangazi.

Anasema mbegu hiyo ambayo wameshaifanyia utafiti wa awali, ina uwezo wa kudumu zaidi ya miaka mitano na kusaidia kuzalisha nyasi kwa wingi tofauti na nyasi za kawaida.

Naye Daktari wa Mifugo Mkoa wa Tanga, Zodiac Lyimo, amesema mkoa huo una upungufu mkubwa wa mitamba bora kwani hitaji halisi ni mitamba 1,000 wakati iliyoko kwa sasa ni mitamba 200.

Anasema ili kumaliza changamoto hiyo juhudi za makusudi zinahitajika ili kuweza kumkomboa mfugaji lakini pia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa ya maziwa kutoka lita 50,000 hadi kufikia lita 120,000 kwa siku.