Home Habari UKITAKA KUMDANGANYA MWAFRIKA, MDANGANYE MSOMI – 3

UKITAKA KUMDANGANYA MWAFRIKA, MDANGANYE MSOMI – 3

488
0
SHARE

Na Victor Makinda

Mfululizo wa makala haya umenijengea chuki na uadui, lakini pia umeniletea marafiki na watu wa karibu. Chuki na uadui na marafiki ni kutoka kwa wasomaji wangu.

Wapo wasomaji wanafurahishwa mno na mfuliluzo wa makala hizi, lakini wapo wasomaji wanaoumizwa na kuchukizwa na makala hizi, cha kuwafurahisha na kutia moyo wanaochukizwa na waonafurahishwa wote hawaachi kufuatilia na kusoma makala hizi.

Wanao nichukia wananituhumu kuwa nina chuki na wasomi wa kiafrika na ndiyo sababu nimekuwa ‘nikiwananga’ katika kumbi huu  Ukweli Ulivyo, hawa wanachomwa na ukweli kwani ukweli humchoma mwongo mithili ya msumali wa moto kwenye kidonda.

Mmoja ameniandikia ujumbe na kuniasa kuacha chuki na wasomi, au ninafanya hivyo kwa kuwa sijasoma? Nilimjibu kuwa sina chuki na wasomi na kamwe sitawachukia.

Ninawapenda wasomi lakini ninawachukia kwa matendo yao na kamwe sitoacha kuwaeleza ukweli ili wabadili fikra na mitazamo yao, waache kuwaza kwa kutumia matumbo yao makubwa na waanze kuwaza kwa kutumia vichwa vyao vilivyokaririshwa nadharia nyingi ambazo zikibadilishwa katika matendo na uhalisia zitatutoa hapa tulipo.

Wasomi waache kudanganywa na kutudanganya waafrika tusio wasomi kwa mustakabali wa ustawi wa bara letu. Pia nilimweleza msomaji wangu kuwa ni kweli sijasoma kwa kiwango cha kuitwa msomi.

Lakini nimetoa ujinga katika shule ya sekondari nimepita pita katika vyuo vya kati ndivyo vilivyonipa ujuzi na uwezo wa kufanya ninayoyafanya lakini huenda matokeo haya iwe ni mazuri au mabaya yamesababishwa na wasomi waliotangulia ambao baada ya kupata elimu wao, hawakushughulisha vichwa vyao kubuni namna nzuri na bora ya kuwapa elimu watoto wa kiafrika/kitanzania.

Ninakumbuka wakati ninamaliza shule katika wilaya niliyotoka palikuwa na shule za sekondari mbili tu na magereza mawili. Naam idadi ya shule za sekondari na idadi ya magereza ilikuwa inafanana.

Lakini pia ukweli haumchagui nani wa kuusema.

Yeyote anayebaini mapungufu katika lolote, anayebaini udanganyifu katika lolote popote ana haki ya kuusema ukweli ulivyo. Wanafalsafa wengi waliowahi kuibadili dunia hii kimtazamo na kifikra sidhani kama walikuwa na elimu kubwa/wasomi.

Shaabani Robert mwandishi nguli wa vitabu vya riwaya, lugha na mashairi hakuwa na elimu ya chuo kikuu. Kazi zake za fasihi zinatumika kufundishia wasomi wa ngazi tofauti ikiwemo. Ukweli ni ukweli tu, moja katika sifa za ukweli lazima ukweli huo uwe kweli na usemwe na msemaji mkweli hauchagui ni msomi au lah.

Ninaamini juu ya falsasa ya Ukweli na namna ukweli unavyokutenga na jamii ama kuunganisha na jamii. Ndio, kuna falsafa inasema ukiwa mkweli utachukiwa na wengi, utapendwa na wachache, utaheshimiwa na kuogopwa na wote.

Dhana hii ndiyo dhana ya kweli na ndivyo Ukweli ulivyo juu ya matokeo yatakayokupata pale utakapoichagua njia ya ukweli. Msemakweli yeyote awaye kamwe hawezi kupendwa katika jamiii ya wasema uongo na waliozoea’ blabla’.

Watanzania kwa bahati mbaya sana wamezoea uongo na wanapendwa kudanganya na kudanganywa. Hapo wapo wasomi na hata wasio wasomi, wengi wao wamezoea kusikia uongo na kamwe hawataki kuusikia ukweli. Hii inatokana na mazoea ya muda mrefu juu ya kuambiwa na kuelezwa uongo.

Hali hiyo haikujitokeza tu kwa bahati mbaya bali ni mfumo kongwe ulioasisiwa na wajanja wachache (wasomi), kwa kutumia ujuaji wao na kwa kutumia umbumbu na imani ya wasio wasomi kwa wasomi, wasomi hao wamekuwa wadanganyifu wakubwa na kuiaminisha jamii ndivyo sivyo.

Jamii ya kiTanzania imezoea kudanganywa na kuepewa ahadi hewa. Mifano ipo wazi, ulingo wa siasa ni moja kati ya mifano

dhahiri. Wanasiasa wengi ni waongo. Wachache wanauishi ukweli. Ni waongo sio kwa sababu hawaujui ukweli, lah hasha ni waongo kwa sababu wamedanywa na kudanganya, wanaendelea kuwadanganya wengine kwa lengo la kutimiza matakwa yao na kushibisha matumbo yao.

Mifano katika hili la wanasiasa na uongo ni mingi isiyotosha gazeti hili kuiorodhesha. Maeneo mengi nchini petu na Afrika kwa ujumla maendeleo yamezorota na umaskini umetamalaki kwa sababu ya uongo.

Watu hawasemi ukweli, watu hawaambiwi ukweli. Na uongo una sifa moja kuu. Uongo ukiurudia rudia kuusema mara nyingi hugeuka sura na kufanana na ukweli. Wasomi na wanasiasa wa kiAfrika ni waongo.

Walianza kuusema uongo kitambo kirefu. Wameurudia rudia uongo huo mara nyingi. Mwisho wa yote uongo huo umekuwa kama ukweli na umegeuka kuwa ni utamaduni na kuwa ni kizazi cha kudanganywa, kudanganya na kudanyika.

Tanzania kuna nuru na taa ya ukweli imeanza kuimulika jamii yetu. Nchi yetu imepata kiongozi mkuu wa dola Msema Kweli. Ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ni msema kweli. Yeye mwenyewe mara zisizo hesabika amejinadi kuwa ni Msema Kweli. Na amekuwa akisema kuwa msema kweli ni Mpenzi wa Mungu.

Ndiyo, msema kweli anabaki kuwa mpenzi wa Mungu na mara nyingi kama sio zote anajenga uadui na kuchukiwa na wanadamu ambao wamezoea kusema na kusikia uongo ukisemwa. Rais Magufuli amebadilisha kabisa dhana hiyo kongwe ya viongozi na wanasiasa na wasomi wetu.

Dhana ya kusema uongo kudanganywa na kudanganya. Dhana ya watu kupenda kusikia na kuelezwa uongo. Nchi yetu kwa sasa inaonja radha mpya kabisa. Watanzania sasa wanaanza kuzoea mtindo mpya wa uendeshwaji wa siasa.

Mtindo wa kuelezwa na kusikia ukweli. Hofu yangu ni je, mtindo huu wa siasa za kusema ukweli pasi kuwadanganya waliozoea kudanganywa utaleta matokeo chanya katika sanduku la kura?.

Narudi tena pale pale kuwa matokeo ya kuusema na kuuishi ukweli ni vigumu kuyaepuka. Naam, Ukiwa ukweli utapendwa na wachache, utachukiwa na wengi, utaheshimiwa na kuogopwa na wote.

Watakaokuheshimu ni wale wanaokuchukia na kukupenda. Kwa kuwa ukweli na uongo hauchanganyiki, Ukweli hudhihiri na kuishi ukiwa hai siku zote. Anayekupenda atayashuhudia matokeo ya ukweli na anayekuchukia atayashuhudia matokeo ya ukweli.

Na kwa kuwa ni Ukweli, matokeo ya ukweli yatakuwa na zao chanya kwa walioambiwa ukweli wakakupenda na hata kwa walioambia ukweli na wakakuchukia.

Wote watafaidi matunda ya ukweli. Hili ni somo gumu, utulivu wa akili na uwezo wa kupembua unahitaji. Huko mbeleni nitaandika makala maalumu juu ya Ukweli ulivyo, namna unavyodhihiri na matokeo chanya ya kuusema na kuushi ukweli.

Nimalize mfululizo wa makala haya kwa kutoa wito kwa jamii ya kiafrika kuutafuta, kuujua na kuuishi ukweli. Ukweli ni uhuru, ukweli ni maendelo,.

Ukweli ni amani, utulivu. Ukweli huleta mshikamano na umoja na utulivu. Tuushi ukweli nao ukweli utatuweka huru.