Home Makala NATAMANI NIKUTANE NA RAIS NIMWELEZA UKWELI

NATAMANI NIKUTANE NA RAIS NIMWELEZA UKWELI

214
0
SHARE

NA VICTOR MAKINDA

MARA KWA MARA huwa napita nje ya viunga vya Ikulu ya Dar es Salaam, nikielekea kwenye mizunguko yangu ya kusaka riziki.  Nipitapo hapo huwa naangalia ndani ya jengo hilo kupitia upenyo wa nondo nene. Naambulia kuwaona ndege tausi na madhari tulivu ya jengo hilo la kuvutia.  Huwa  najisemea moyoni, Rais kipenzi cha Watanzania anakaa muleee.  Kwa kweli huwa natamani sana kuingia nionane nae nimweleze ukweli.

Ukweli Ulivyo ninatamani sana kukutana ana kwa ana na Rais Dk. John Magufuli, nimweleze ukweli. Msomaji unaweza kujiuliza kwa nini  natamani kukutana na Rais wetu. Tamanio langu kuu la kutaka kuonana na Rais huyu mzalendo kipenzi cha Watanzania ni moja tu. Ninataka kumweleza ukweli. Ndiyo, hata yeye mwenyewe rais wetu huwa anasema kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu, nami ninataka kumweleza ukweli juu ya hali halisi ilivyo  na namna Watanzania wanavyomzungumza huku mtaani kuhusu utawala wake kwa kipindi cha miaka miwili. Ninataka kumweleza ukweli ili  nami niwe mpenzi wa Mungu kwa kuusema Ukweli.

Ukuta wa Ikulu ni kikwazo kwangu ila ninaamini ipo siku nitaonana nae. Lakini siwezi kusubiri mpaka siku hiyo ifike nipate fursa ya kumuona   ana kwa ana, nitatumia ukurasa wangu huu huu kukutana nae na kumweleza kile ninachokusudia kumweleza. Kufanya hivyo hakufuti kiu yangu ya kukutana nae. Natamani  kukutana na Rais wangu  kipenzi cha watanania,  Rais Magufuli.

Rais wetu ni msomaji, ni mfuatiliaji wa vyombo vya habari. Mara nyingi amekuwa akipiga simu kwenye vituo vya luninga na kusema chochote iwe ni kupongeza ama kutoa ufafanuzi. Tunaye Rais anayefuatilia vyombo vya habari. Tunaye Rais anayethubutu si kufuatilia tu taarifa mbalimbali bali pia kuwasiliana moja kwa  moja na waandishi, watangazaji wa chombo husika. Hilo kwangu kama mwanahabari mchambuzi linanipa moyo mno. Si tu mimi bali wanahabari wengi ninaamini wanafurahishwa na hatua hiyo nzuri. Inatutia moyo kuona kuw kazi za mikono yetu inamfikia.

Nikiamini hilo ninaamini kuwa Rais wetu anasoma pia gazeti hili kongwe pendwa la Rai. Ninaamini pia rais wetu anasoma ukurasa huu wa Ukweli Ulivyo kwani yeye ni Msema Kweli, ninaamini hawezi kuupita ukurasa huu unaojinadi kwa kuusema kweli. Naam, natamani sana kukutana na Dk. Magufuli, ninataka nimwambie Ukweli.

Msomaji unaweza kuwa unajiuliza maswali, ni Ukweli upi ninaotaka kumweleza Rais Magufuli. Yapo mengi ya Ukweli kabisa ambayo bila kupepesa macho, kwa heshima na taadhima kwa kiongozi wangu huyu mzalendo aliye tayari kufa kwa ajili ya maisha ya wanyonge wa nchi hii ambayo ninakusudia kumweleza.

Nikikutana naye nitamsalimia kwa heshima na taadhima kubwa, tena kuizidi ile ya aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Dodoma, rafiki yangu, kaka yangu Jordan Lugimbana. Baada ya kumsalimu nitamweleza lengo langu la kukutana naye. Sina shaka ataniruhusu niseme nini ninataka kumweleza.

Nitamwambia, Mheshimiwa Rais nimekuja kwako nikiwa ni mwananchi wa kawaida kabisa.  Mmoja kati ya wanyonge wa nchi hii ambao umeapa kuwapigania. Kwanza nimekuja kukupongeza kwa miujiza unayoifanya.  Hapa huenda akaniuliza swali, miujiza ipi ninayoifanya?. Nitamweleza, Rais wangu kuwa wewe ni Masiha wetu, wewe ni mtenda miujiza. Unafufua matumaini ya wengi yaliyokufa. Wengi waliokata tamaa unawarejeshea matumaini makuu. Wanaiona nchi ya ahadui kupitia kwako.

Sina shaka hujaja mwenyewe, wewe umeletwa. Aliyekuleta sio mwanadamu bali ni Mungu kwa minajiri ya kuwakomboa waTanzania. Umekuja kutukomboa sisi watanzania wanyonge ambao kwa miaka zaidi ya 50 tangia tumepata uhuru hatukuwahi kuwa na kiongozi wa aina yako. Ndiyo, hatukuwahi kuwa na kiongozi asiyepepesa macho. Viongozi tuliwaowahi kuwa nao walikuwa na sera ya kulindana. Rais Magufuli wewe tangia umeingia madaraka yapata miaka miwili  sasa umeweza kwa kiasi kikubwa kukiruka kiunzi hicho cha sera ya kulindana hasa hasa kwenye maovu.

Kwa viongozi wanaotokana na watu, watu waliounda mitandao ya uongozi  na kuwaandaa watu wao muda mrefu kabla ya kipindi cha uchaguzi ni vigumu mno kutowalinda watu wale ambao wameshiriki kikamilifu kukufanya kuwa kiongozi wao.

Nionavyo Mheshimiwa rais umefanikiwa hilo kwa kuwa wewe hukutokana na mtandao. Wewe sio zao la mtandao. Hukufinyangwa na mtu au kikundi cha watu kuwa kiongozi, hii inakupa wepesi wa kuifanya kazi yako kwa kuzingatia ukweli pasipo kupepesa macho na kumwonea aibu mtu.

Naam, huna wa kumwogopa wala kumuhofu. Bali watu wengi kama sio wote wanakuogopa na kuihofu misimamo yako, watu hawa si wengine bali ni wavivu, wala rushwa, wafanya magendo, wazembe, majambazi, wanyang’anyi na wahujumu uchumi. Mheshimiwa rais nikuonavyo sidhani kama unaye wa kumlipa fadhira, nadhani huna.Nitamwomba mheshimiwa rais azidi kunisikiliza.

Kuhusu mitandao ya kutafuta viongozi

Mhemiwa rais, kwa kuwa wewe sio zao la mtandao kama nilivyotangulia kusema na hautokani na zao la mtandao unaifanya kazi yako ya urais kuwa rahisi japo huwa unanung’unika mara ka mara kuwa kazi ya Urais ni Mateso makubwa, lakininionavyo ni kwa sababu wapo waliozoea uchafu, usafi wako ni kikwazo kwao. Pambana nao wasikukwamishe., Na kwa kuwa wewe ni kiongozi mkuu wa dola na Mwenyekiti wa Chama kinachotawala CCM,  Mheshimiwa rais ninataka kukueleza ukweli kabisa kuwa fanya kila liwezekanalo dhibiti mazingira yoyote ya uundwaji wa mitandao ya kutafuta uongozi ndani ya Chama chako CCM na serikali yako tukufu unayoiongoza.

Kwa nini nasema hivyo, nasema hivyo kwa sababu ninaaamini kuwa na ndivyo ukweli ulivyo, hakuna biniadamu ambaye yupo tayari kutoa pasipo kupata. Wana mtandao ndio ambao huwayumbisha viongozi wetu.Hutikisa nchi, hupanga agenda zao na hufanikiwa hujuma zao kwani wana nguvu na sapoti ya utawala.

Wana mtandao  hushiriki kuasisi mitandao na kumpandikiza mtu wao kwa huchanga mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kugharamia lengo lao. Hawa baadhi fedha zao huwa ni haramu na hutokana na misingi isiyo na uadilifu. Kana kwamba haitoshi hutoa pesa nyingi ili kuwasimika viongozi wawatakao ili kupata upendeleo katika baadhi ya mambo iwe ni  ya kisiasa au kiuchumi.Hasa hasa kufanikisha upigaji.

Mheshimiwa rais wana mtandao wengi ni wakwepa kodi na baadhi ni wauza madawa ya kulevya na hata magendo  mengine. Wana mtandao ni majangiri wakubwa hufanya bishara za kuuza nyara za serikali pamoja na magendo makubwa. Wana mtandao, huwa hawaguswi kwani anayejaribu kuwaguswa, huguswa yeye kabla ya wanamtandao kuguswa. Hawa niwatu wenye kinga kubwa kisiasa na kiuchumi. Wanafahamaika na wanalindwa na viongozi waliowafinyanga.

Mheshimiwa rais, tumia nguvu yako kubwa uliyopewa na katiba yetu kuhakikisha kuwa ndani ya serikali yako, na katika chama chako unachokiongozi ipigwe marufuku ya kisheria kuasisi mitandao ya kuelekea uchaguzi mkuu. Hii inatoka na madhara makubwa ya wana mtandao ambayo huwa wanaisababishia nchi baada ya mtu wao kupita katika nafasi fulani. Mtu huyo hugeuka kutoka kuwa kiongozi wa watu wote na kuwa kiongozi anayelinda maslahi ya wachache walioshiriki kumfinyanga., Matokeo yake nchi baada ya kupiga hatua za kimaendeleo inapiga hatua kiufukara. Kwani wana mtandao huifilisi nchi kwa kukwepa kodi na kuhujumu uchumi huku wakipewa ulinzi na viongozi waliotokana na mitandao yao.

Ninao mfano mmoja Mheshimiwa rais. Kuna bwana mmoja rafiki yangu, alipiga picha na kiongozi mmoja mkuu wa awamu zilizopita, picha ile akaisafisha kwa ukubwa wa ukutani, akaibandika dukani kwake. Ni duka la jumla, Mheshimiwa rais huwezi amini. Maofisa wa mamlaka ya mapato wilayani kule walikuwa wanaliogopa kweli duka hilo. Kisa walipita siku moja kwa lengo la kulifunga duka hilo kwa kuwa lilikuwa linadaiwa kodi nyingi, walipoiona picha ya mmiliki wa duka akiwa katika picha na kiongozi mkuu, Maofisa wa TRA wakahofu ukaribu wa mmliki wa duka na kiongozi mkuu. Yule bwana akawa ni mfanya biashara anayekwepa kodi kwa kutumia picha aliyopiga na kiongozi mkuu tu. Wale maofisa wa TRA, walihofu kuwa huendayule bwana ni mwanamtandao au ana unganika na kuwasiliana na kiongozi huyo.

Wangapi wamefanya hivi, ni kiasi gani cha pesa kimepotea kama kodi ambayo ingewasidia wanyonge wa nchi hii?. Ndiyo maana ninasema Mheshimiwa rais, tafadhar tafadhari, pambana kuhakikisha unaweka misingi imara madhubuti itakayokomesha mitandano ndani ya chama na serikali yako ya kizalendo.

Moja katika vyanzo vingi vya ufukara wa watanzania ni mitandao ya uongozi ambayo imejenga na kuleta sera za kulindana inayotoa fursa kubwa kwa wasio wazalendo kupiga pesa nyingi ambazo zingewasaidia masikini wan chi hii. Mheshimiwa Rais wewe ni shahidi katika hili, hata ulipoingia hapa Ikulu umebaini mengi ambayo pengine hukuwa unayajua. Nimewahi kukusikia mara nyingi ukisema kuwa nchi hii imeliwa sana.  Sasa ninakueleza ukweli rais wangu, walioitafuna nchi hii sio wengine ni wana mtandao na makundi yao.

Narudia kusema kuwa nina kupongeza sana kwa kuonesha nguvu kubwa na dhamira ya dhati ya kupambana na wabadhirifu na kuivunja vunja mitandao fukarishi kwa watanzania.  Lakini Mheshimiwa Rais kuna walio kinyume na wewe ambao hawachezi ngoma unayopiga wewe wanapanga na kujaribu, kuhujumu juhudi zako…..

Itendelea wiki ijayo…