Home Habari CHADEMA SASA KUJENGA ‘UKUTA’ MPYA

CHADEMA SASA KUJENGA ‘UKUTA’ MPYA

746
0
SHARE
NA MWANDISHI WETU

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema katika mwaka huu wa 2018, kitafanya mageuzi ya kisiasa na kuendelea kuboresha mikakati yake kama chama kikuu cha upinzani nchini, RAI linaripoti.

Hatua hiyo imekuja baada ya chama hicho kupata wakati mgumu kisiasa katika kipindi cha mwaka 2017, na kuacha doa baada ya kushindwa chaguzi mbalimbali—pamoja na uchaguzi wa marudio katika kata 43 ambapo kiliambulia kata moja tu.

Aidha, kuzorota kwa mikakati mingi ya chama hicho, pamoja na Umoja wa Kupinga Udikteta (UKUTA), ulioanzishwa mwaka 2016, pia inadaiwa kumechagiza chama hicho kujipanga upya.

Tangu Rais John Magufuli, aingie madarakani, Chadema na vyama vingine vya upinzani, vimekuwa vikilalamika kukosa fursa ya kufanya siasa, hasa baada ya mikutano ya hadhara na maandamano kupigwa marufuku.

Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alisema mwaka 2018, chama hicho kitajipanga upya kufanya siasa zake nchini.
Pamoja na kukiri kuwa chama kimekutana na wakati mgumu kwenye harakati za kisiasa mwaka 2017, alisema changamoto hizo zimewafunza kisiasa.
Pamoja na mambo mengine, alisema wanatarajia kufanya mageuzi makubwa mwaka huu.
“Mwaka 2017, ulikuwa wa changamoto kubwa kwa wananchi na wanasiasa, lakini tumejifunza na tumejipanga, ili mwaka ujao tuweze kubadilika na kuendana na hali halisi,”alisema Dk. Mashinji.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti, Freeman Mbowe. Katika salamu zake za mwaka mpya 2018, Mbowe ambapo alisema Chadema kitaendelea kupigania haki na demokrasia nchini.

Alisema chama hicho hakitaogopa tena vitisho, kamatakamata ya viongozi kama ilivyokuwa mwaka 2017.

Mbowe alisema kuna umuhimu wa chama hicho kikuu cha upinzani kuendeleza mema yote katika mikakati yake ya kudai haki na demokrasia halisi nchini.

Alisema viongozi wa chama, wana ari ya kufanya kazi kwa bidii, kwa nguvu na kwa akili zao zote, ili kufikia malengo yake.

Alisema: “Katika utawala wa awamu ya tano, imeonekana wazi hauheshimu Katiba na kufuata sheria, hivyo tutaendelea kuwasisitiza viongozi waheshimu Katiba na Sheria. Hatuwezi kuongoza nchi kwa matamko wakati zipo sheria tulizozitunga zituongoze.”

Katika kile kinachoonekana kuibua upya ile kauli mbiu ya UKUTA (Umoja wa Kupinga Udikteta) ilioanzishwa na chama hicho mawaka 2016 baada ya kupigwa marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, Mbowe amesema chama hicho hakitaogopa vitisho, kamatakamata ya viongozi wa Upinzani kama tulivyoshuhudia 2017.
Alisema: “Tutaendelea kupigania utawala unaofuata sheria, Katiba Mpya na uhuru wa watu kutoa maoni na kuendelea kukosoa Serikali kila tunapoona inakosea, kwani ni haki ya kikatiba kufanya hivyo mradi hatuvunji sheria.”
Aidha, aliwataka viongozi wa dini waendelee kumkosoa mtu yoyote—awe kiongozi wa upinzani, au wa Serikali, na kukusitiza kwamba uhuru wa maoni lazima uheshimiwe.
Akitoa mfano, alisema kiongozi wa zamani wa Libya, Muhamar Gaddafi, aliwapa wananchi wake kila kitu walichotaka, lakini aliwanyima uhuru, hawakuruhusiwa kuikosoa serikali yao, walinyimwa uhuru wa kuchagua kiongozi waliyemtaka. Wakati ulipofika, wananchi hao hao ndio waliomtoa madarakani.
Alisema watu hawawezi kupata maendeleo kama hawapo huru, uhuru na maendeleo ni vitu vinavyokwenda pamoja. Huwezi kuleta maendeleo katikati ya watu ambao wamejawa hofu, hawana uhuru wa kusema na kukosoa.