Home Latest News KITAKACHOVIOKOA VYAMA VYA UPINZANI HIKI HAPA

KITAKACHOVIOKOA VYAMA VYA UPINZANI HIKI HAPA

589
0
SHARE
Na Thadei Ole Mushi

Leo naomba niwatoe hofu vyama vya upinzani huku nikiweka tahadhari kwa chama changu cha CCM.

Aidha, ninachokiandika siku zote kinaweza kutumiwa na vyama vyote kwa kuwa lengo letu ni kuijenga Tanzania yenye maendeleo yanayomgusa kila mwananchi.

Kwa haraka haraka ukiangalia hali ya kisiasa nchini, inaonyesha kama vile CCM inaimarika sana huku vyama vya upinzani vikionekana kama vinakufa. Ukimkuta mwana CCM yeyote, anashangilia kwa watu kuhama ukwenda CCM, mpinzani utamkuta anasononeka na kufikiri kuwa upinzani unakufa na CCM inaimarika. Ukweli ni upi?

Kwa kuwa ukweli ukisemwa huonekana kwa urahisi kuliko uongo. Hebu soma halafu pima kama ni ukweli au uongo.

Ni kweli kuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, upinzani ulikuwa unatisha sana. Ulikuwa na nguvu kubwa sana. Upinzani ulikuwa bado kidogo ufanikiwe kufanya mapinduzi ya kidemokrasia.

Si jambo la kubeza kwa chama cha upinzani kufanikiwa kupunguza kura za CCM hadi mgombea wake kupata ushindi chini ya asilimia 60. Tafsiri rahisi ni kwamba walikuwa karibu kabisa kufanikiwa kugawana kura nusu kwa nusu. Haya ni mafanikio makubwa na wala sio ya kubeza.

Wataalamu wengi wanakubaliana kuwa kuna hatua saba za chama au kikundi cha watu kupitia kufikia mapinduzi ya kisiasa. Ukisoma ‘anatomy of revolution’ utagundua kuwa Chadema walikuwa wamefikia ngazi ya pili—ambayo ilikuwa ya muhimu sana, lakini sasa hivi wamerudi mwanzo kabisa na inawabidi waanze upya, au wasubiri CCM wajichanganye.

Hatua hii ya pili inaitwa ‘kujikosoa’. Hii ni hatua ambayo chama au kikundi cha watu wenye nia ya kufanya mapinduzi, huungwa mkono na tabaka la wasomi katika kuikosoa serikali.

Tabaka hili huamsha tabaka la chini yake—wananchi wa kawaida ambao ni wengi—kuungana na wanaotaka kufanya mapinduzi na hatimaye wakishajiunga, huingia katika hatua ya tatu—kuenea kwa kundi kubwa la wananchi wasioridhika.

Mara nyingi mkifikia hatua hii, wanaotaka kufanya mapinduzi au kuondoa utawala uliopo madarakani, iwe kwa kura au njia yoyote ile, siasa zake huwa nyepesi sana. Ni hatua ambayo wasomi hujitokeza hadharani kuunga mkono wale wanaotaka kufanya mapinduzi. Hujitokeza hadharani na kukosoa utawala uliopo. Kwa kufanya hivyo huamsha ari ya waliowengi, ambao ni wananchi walalahoi na kuwaunga mkono wapinzani.

Ukicheza nao hawa walalahoi, hufikia hata uwamuzi wa kuwa tayari kufa, alimradi tu anayehubiriwa kuwa mbaya wake lazima aondoke madarakani.

Pitia mapinduzi yoyote yale, au pitia sababu za vyama vyote duniani vyama tawala, huwa rahisi sana kuondolewa madarakani pindi wanapofikia hatua hii ya kukosolewa na wasomi maana ni ngumu kuwajibu. Usicheze na nguvu ya akili.

Kwa sasa ni kama hatua hii imekufa kwa kuwa inaonekana kama wasomi badala ya kukosoa, wanarudi kuungana na CCM.

Tumeona wasomi wengi ambao walikuwa wamejinasibisha na upinzani wakirudi kuiunga mkono CCM. Hapa nazungumzia wasomi kama kina Kitila, Dk. Slaa na wengineo ambao siku za karibuni wamejiunga na CCM.

Hofu ndani ya CCM kutaifufua Chadema kwa maana rahisi kabisa—kitendo cha wenyeji kuwa na hofu ya kupoteza maslahi yao ndani ya nchi, kutokana na wageni kuhamia kwa wingi.

Kuna hofu na chuki ndani ya CCM inayoendelea ndani kwa ndani. Wenyeji ambao ni wana CCM asilia, wanaanza kuongea lugha moja dhidi wale wanaohamia.

Ni kweli kuwa ‘wakuja’ wanakuwa na hadhi daraja la kwanza ndani ya CCM, jambo ambalo japokuwa halisemwi hadharani, linasemwa chini chini.

Kitendo cha wakuja (wanaohamia), hawa kupewa masilahi ya wana CCM asilia kunatengeneza tabaka ambalo hapo baadaye linaweza kumegukia upinzani na hapa ndipo ule usemi wa upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM utakapotimia.

Kuna watu wako CCM toka enzi na enzi, kazi yao ni kukipigania chama tu, watu hawa liwake jua inyeshe mvua, chama kitukanwe au chama kisifiwe, wao wapo na CCM yao.

Hawa ni wale waliohakikisha Lowassa haingii Ikulu, si kwa kuwa hafai, ila kwa kuwa hayupo CCM. Hawa ni wana CCM kindakidaki—ambao aidha kwa uCCM wao wameitwa tahira, hawana akili, wamepoteza marafiki zao—kisa tu chama chake.

Ni kweli itawahuzunisha sana kama wapinzani ambao wawapunguzia kura 2015 kupewa maslahi ambayo wapo wana CCM ambao wangeweza kuyafanya.

Ukweli ni kwamba hili linazungumzwa kichinichini. Kama hali hii ya chuki na wasiwasi itaendelea,  kuna watu wanaoijua CCM ndani na nje, wanaweza kushawishika kuondoka na hili linatakiwa liwe ni sala kuu ya wapinzani kuendelea kuomba hawa wahamiaji wapewe hadhi kuliko CCM asilia. Hili litatokea muda si mrefu.

Vyama vingi vya siasa duniani vimepasuka kutokana na msuguano wa ndani ya chama—hasa kwenye suala la maslahi. Kunapokuwa na vita ya maslahi kati ya makundi mawili, kundi linaloona kama linaonewa hujitoa ufahamu na kumwaga mboga na ugali wake, ili  wakose wote.

Je, kundi la wachungaji na maaskofu kuanza kuhoji ni tabaka jipya la wasomi linataka kujitokeza?

Kuna haja ya kusoma na kutafsiri tukio hili kwa kina. Sio jambo la kuacha liende kimya kimya.
0712702602