Home Latest News MISRI NA UTAMADUNI WA KUTAWALIWA KIMABAVU

MISRI NA UTAMADUNI WA KUTAWALIWA KIMABAVU

702
0
SHARE
Marais wa zamani wa Misri: Anwar Sadat (1970-81) na Hosni Mubarak (1981-2011).
NA HILAL K SUED

Misri kuwa na milolongo ya tawala za kijeshi ni kitu kisichokaa vyema kwa nchi hiyo. Nchi iliyo kaskazini mwa Bara la Afrika ina historia kubwa na inasadikiwa kuwa ni kitovu cha ustaarabu duniani.

Ni nchi iliyoendelea kielimu, kama siyo kiuchumi na mara nyingi imekuwa mstari wa mbele katika masuala ya Bara la Afrika, kisiasa, kijamii na hata kiuchumi na kuwa kiunganisho muhimu kati ya Afrika na nchi za Kiarabu.

Ni nchi yenye wasomi wengi katika fani mbali mbali, lakini mapungufu yake makubwa yako katika masuala ya demokrasia na utawala bora.

Inawezekana hulka ya Wamisri ni kutawaliwa na milolongo ya madikteta wanajeshi. Hii inazidi kudhihirika baada ya ujio wa kiongozi wao wa sasa Generali Abdel-Fattah Al-Sisi aliyeingia madarakani mwaka 2013 baada ya kumpindua aliyekuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia – Mohamed Morsi.

Hebu tazama: Tangu nchi hiyo ilipoupindua utawala wa kisultani wa Mfalme Farouk mwaka 1952 ni wanajeshi tu ndiyo wametawala, ingawa baadaye hawa waliamua kuvua sare zao na kuvaa nguo za kiraia.

Hawa ni pamoja na Jenerali Mohammed Naguib (1952-54), Luteni Kanali Gamal Abdel-Nasser 1952-70, Kanali Anwar Sadat (1970 hadi kuawa kwake mwaka 198, na Kamanda wa Jeshi la Anga Hosni Mubarak kuanzia 1981 hadi alipopinduliwa kwa nguvu ya umma mwaka 2011.

Kitu kikubwa cha kushangaza ni kwamba baada ya takriban miaka 30 ya utawala wa kikandamizi wa Hosni Mubarak, Wamisri walisema inatosha na wakaja juu kwa wingi katika maandamano ya kumtaka aondoke. Lakini baadaye walirudi kule kule.

Sote tunakumbuka maandamano ya kila siku ya halaiki ya watu katika Medani ya Tahriri (Tahrir Square) jijini Cairo, maandamano ambayo wananchi wengi walipoteza maisha katika mapambano na vikosi vya serikali.

Baada ya Mubarak kusalimu amri na kung’atuka (na baadye kukamatwa) wengi tulitarajia kwamba ndiyo ulikuwa mwisho wa udikteta nchini humo. Lakini wapi.

Baada ya kipindi cha mpito chini ya utawala wa Jeneral Hussein Al-Tantawi, kuliandaliwa uchaguzi katika mazingira ya demokrasia ya vyama vingi na katika uchaguzi huo Mohamed Morsi, wa muungano wa vyama chini ya mwavuli wa Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood) alishinda na kuwa rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia.

Tukumbuke pia kwamba chama cha Udugu wa Kiislamu kilikuwa kimepigwa marufuku tangu enzi za Rais Abdel Nasser katika miaka ya 50 na kilikuwa kinaishi kwa siri. Hivyo baada ya kuondolewa utawala wa Hosni Mubarak kiliruhusiwa kugombea katika uchaguzi.

Vile vile ikumbukwe wafuasi wa Udugu wa Kiislam ndiyo waliotoa mchango mkubwa sana katika harakati zile za maandamano za kumng’oa Hosni Mubarak.

Lakini mwaka 2013, kutokana na kile kinachosadikiwa kuwapo kwa msukumo wa nchi za magharibi, hususan Marekani, Morsi alipinduliwa na Jeneral Abdel Fattah Al-Sisi ambaye alikuwa amemteua katika wadhifa huo miezi mitatu tu nyuma. Hatua ya kwanza Sisi alichukua ni kumuweka Morsi jela.

Kulizuka maandamano makubwa tena nchini humo ya wafuasi wa Morsi wakidai kufunguliwa kwake na kurejeshwa madarakani, lakini waandamanaji walikabiliana na vikosi vya jeshi la Sisi ambao walitumia nguvu kubwa na ukatli kuyazima maandamano na mamia walipoteza maisha.

Na ingawa mwanzo Sisi alisema yeye anashika usukani kwa muda tu hadi uchaguzi mwingine ambao yeye binafsi asingegombea, lakini aligeuza mawazo na kuamua kugombea. Hii pia, inavyoaminika, ni kutokana na msukumo wa kutoka Marekani ambayo haikuwa inajisikia vyema kwa kiongozi wa chama cha Kiislamu kuwa Rais wa Misri, nchi ambayo ni swahiba wake mkubwa katika eneo hilo.
Na kama ilivyotarajiwa na wengi, Sisi alishinda uchaguzi ule kutokana na chama cha Udugu wa Kiislamu kususia kushiriki kwa madai kwanza Morsi aachiwe huru na utawala wake uliochaguliwa kihalali na wananchi urejeshwe.

Hata hivyo tangu achaguliwe, utawala wa Sisi umedumu kwa mtutu wa bunduki katika kukabiliana na wapinzani, hasa wale wa chama cha Udugu wa Kiislam. Maelfu yao walikamatwa na kuwekwa ndani. Baadhi yao walifunguliwa mashitaka na kuhukumiwa vifo.

Mwaka jana katika kesi moja zaidi ya watuhumiwa 300 walihukumiwa adhabu hiyo iliyosababisha shutuma kali kutoka jamii ya kimataifa na makundi mbali mbali ya haki za kibinadamu.

Aidha chama cha Udugu wa Kiislamu kilipigwa marufuku tena na safari hii kuainishwa kuwa chama cha kigaidi. Kiongozi wake, Mohamed Badie na viongozi wengine 13 walihukumiwa kunyongwa kwa makosa ya kuchochea maandamano ya kupinga mapinduzi ya Sisi dhidi ya Morsi.

Morsi mwenyewe alihukumiwa miaka 20 jela kwa makosa kama hayo, ingawa yeye alikuwa na kesi mbili dhidi yake ambazo zilizokuwa zikimkabili.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu wanautuhumu uendeshaji wa kesi hizo chini ya utawala wa Sisi kwa kutozingatia haki, kwani mahakama huendeshwa kwa siri na watuhumiwa kunyimwa uwakilishi wa kisheria.

Wanaomuunga mkono Sisi wanasema kiongozi huyo amesaidia sana kuleta hali ya utulivu na kumsifu kwa kutoipeleka nchi kuwa katika hali kama ilivyo Libya, Iraq na Syria. Yeye mwenyewe Sisi anasema: “Sina muda wa kuendelea kuzozana na magaidi hawa.”

Lakini wachunguzi wa mambo wanadai utulivu huu anaojigamba nao umekuja kwa umwagikaji mkubwa wa damu ya Wamisri. Si hilo tu, bali pia wanadai utawala wa Jenerali Sisi umeirudisha nchi nyuma na kuwa katika hali zaidi ile ilivyokuwa katika miaka ya mwishoni ya utawala wa mwanajeshi Hosni Mubarak.

Utawala kandamizi wa miaka mingi wa Hosni Mubaraka, uminywaji wa demokrasia na haki za binadamu pamoja na uhuru wa vyombo vya habari ndiyo ulisababisha ghasia za maandaano makubwa ya Wamisri mwaka 2011 uliomg’oa.

Historia inajirudia kwani Wamisri, pamoja na mafanikio yao katika nyanja nyingine nyingi, utawala wa kidemokrasia halisi hawauwezi kabisa. Wamezoea kutawaliwa kimabavu.