Home Latest News POLISI USALAMA BARABARANI YAJA NA ‘OPARESHENI KAMATA’

POLISI USALAMA BARABARANI YAJA NA ‘OPARESHENI KAMATA’

740
0
SHARE
NA JOHANES RESPICHIUS

UKITAJA visababishi vikuu vya vifo, huwezi kuacha kutaja ajali za barabarani ambazo kwa mujibu wa Shirika la Afya Dunia (WHO), huchangia vifo vya watu milioni 1.2  kila mwaka.

Ajali nyingi za barabarani zimekuwa zikisababishwa na madereva wasio na weledi wa kazimhiyo, ambao hawazingatii masuala ya kiusalama kwa vyombo vya usafirishaji ikiwa ni pamoja na kutotii sheria zilizowekwa.

Ni dhahiri kwamba kila nchi inazo sheria za usalama barabarani ambazo hapa Tanzania zinasimamiwa na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani ambacho kwa kiasi kikubwa limekuwa likifanya kazi nzuri kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.

Pamoja na kuwapo kwa sheria mbalimbali, lakini kumekuwa na changamoto ya ajali nyingi katika Bara la Afrika ambalo halina hata asilimia 10 ya vyombo vyote vya moto duniani, lakini linaongoza kwa ajali.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2015 ambayo inabainisha ajali nyingi zinasababishwa na  mwendo kasi, ulevi na matumizi mabaya ya vifaa vya usalama kama matumizi ya mikanda, kofia au ‘helmet’ za waendesha pikipiki (bodaboda), na hata viti maalumu kwa katika magari kwa ajili ya watoto.

Ajali hizi husababisha vifo ambapo kwa Tanzania, zaidi ya watu 3,400 hufariki kila mwaka jambo ambalo huifanya kuongoza kwa vifo vingi Afrika ambayo ni sawa na asilimia 32.9 ya ajali zote milioni 125 zinazotokea duniani kila mwaka.

Lakini takwimu za dunia, watu milioni 1.2 hufariki kila mwaka ambapo asilimia kubwa ya ajali hizo zinatokea Afrika licha ya kuwa chini ya asilimia 10 ya vyombo vya moto, hiyo inaonyesha kwa kiasi gani ajali zinavyopoteza nguvu kazi kubwa barani Afrika.

Desemba 28, mwaka jana, Kikosi cha Usalama Barabarani, kilitoa tathimini ya makosa ya usalama barabarani nchini kwa mwaka 2017, ambapo kilibainisha ongezeko la makosa hayo kutoka 137,152 mwaka juzi, hadi 178,285 kuanzia Januari 1, hadi Desemba 25, mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la makosa  41,133 sawa na asilimia 23.

Tathmimi ya hali ya ajali za barabarani kwa mwaka 2017, ilitolewa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Misilmu, ambaye anasema hali hiyo ilitokana na jitihada za kikosi hicho za kukabiliana na vyanzo vya ajali.

Anasema Kikosi cha Usalama Barbarani,  kimekuwa likichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ajali, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani, kufanya doria na oparesheni barabarani, kudhibiti mwendo kasi kwa kutumia tochi.

“Pia tumekuwa tukifanya ukaguzi wa magari kabla ya kuondoka katika stendi za mabasi, kupima madereva kabla hawajaanza safari, kukamata uzidishaji, ubebaji wa abiria na mizigo kwa njia ya hatari ikiwa ni pamoja na kukagua leseni.

“Jitihada hizo zimesababisha kupungua kwa makosa ya pikipiki  kutoka 28,423 mwaka juzi hadi 22,589 mwaka jana, hiyo inaonesha ni kwa kiwango gani wadareva ambavyo wameanza kutii sheria bila shuruti.

“Makosa yanayotokana na ubovu wa vyombo vya moto, mwaka jana yamefikia 45,931 kutoka 38,648 mwaka juzi, ongezeko  la makosa 7,283, sawa na aslimia 16. Makosa ya mwendo kasi mwaka 2016 yalikuwa 37,011 lakini kwa mwaka 2017, yamepungua hadi 33,836,” anasema Kamanda Musilimu.

Aidha, anasema makosa ya ulevi yalipungua kutoka 38 mwaka jana hadi 17 mwaka 2017, ikiwa ni pungufu ya makosa 21 sawa na asilimia 16. Kwa upande wa uendeshaji wa hatari, kulikuwa na makosa 7,994 ukilinganisha na 6,028 mwaka 2016.

Anasema kwa mwaka huu, Kikosi hicho kimejipanga vizuri ili kuhakikisha ajali zinadhibitiwa kwa kiasi kikubwa, ili kurejesha imani kwa abiria ambao wamekuwa na hofu ya kutumia usafiri wa mabasi wakiogopa ajali.

“Tunatekeleza haya kupitia oparesheni yetu kabambe ya Kamata ambayo tayari imeanza kuzaa matunda na nidhamu kwa watumiaji wa vyombo vya moto imeanza kurudi—madereva wengi wameanza kuwa makini na kuzingatia sheria za barabarani na utii wa sheria bila shuruti wamapoendesha magari.

“Pia nitumie nafasi hii kutoa wito kwa madereva kufuata sheria za usalama barabarani, kwani dereva ambaye hatazingatia sheria na kufuata sheria bila shuruti, tutamshurutisha na hatabaki salama,” anasema Kamanda Musilimu.

Ripoti ya Polisi inaonyesha kwa kiasi gani bado jitihada kubwa baina ya wadau mbalimbali inavyohitajika ili kunusuru maisha ya vizazi na nguvu kazi ambayo imekuwa ikipotea kila kukicha kutokana na ajali za barabarani.

Ipo mifano mingi ya watu ambao walikuwa wazima, lakini sasa wamekuwa na ulemavu wa kudumu, huku idadi nyingine kubwa ikipoteza maisha—jambo ambalo mbali na kuondoa nguvu kazi ya taifa, lakini zimeacha wajane na yatima wengi ambao wengi wao wanaishi katika maisha duni na ya dhiki.

Hivyo basi, umefika muda wa kila mtumiaji wa chombo cha moto awe dereva au abiria na hata mtembea kwa miguu, maana ajali inapotokea huwahusisha wote—kuhakikisha  wanazingatia sheria ili kuepuka janga hilo ambalo ni dhahiri kwamba kila mtu akisimama katika nafasi yake, linaweza kuwa historia na watu wakaishi salama.

Pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali pamoja na wadau wengine, ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, katika mwaka 2017, tatizo hili limeonekana kuwa bado changamoto, hivyo wanapaswa kuja na mbinu nyingine zaidi kuhakikisha katika mwaka huu, ajali zinapungua kama sio kuisha kabisa.