Home Latest News UJUMBE WA ASKOFU SHAO UFANYIWE KAZI KIVITENDO

UJUMBE WA ASKOFU SHAO UFANYIWE KAZI KIVITENDO

691
0
SHARE
NA RASHID ABDALLAH

Watu waliofunika nyuso wakiwa na silaha za moto na jadi, katika gari KM 155 ya Serekali, wakipita maeneno ya mjini Zanzibar.

Kwa wale tunaoamini uwepo wa Mungu, tunakubaliana wakati mwingine Mungu hufanya mambo kwa makusudi maalumu. Yawezekana mwanzo tukachukizwa na tukio fulani, mwisho tukaona makusudio ya Mungu, ikakubidi tufunge midomo,  au ufurahie.

Katika Krismas iliyoisha, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), lilitangaza misa ya Krismas kitaifa itafanyika Zanzibar, sio jambo lililozoeleka lakini hatimaye misa ilifanyika.

Ni katika Jimbo Katoliki Zanzibar, kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Minara Miwili hapa Unguja, ndipo waumini wa Kikatoliki walipokusanyika kwa ajili ya maadhimisho ya siku hiyo.

Pengine kila mtu alipokea kwa mtazamo tofauti misa kitaifa kufanyika Zanzibar, lakini naamini hakuna aliyechukizwa na ujumbe uliotolewa na muongoza misa wakati akizungumza na waumini wake.

Askofu wa Jimbo hilo, Mhashamu Augustino Shao, ambaye ndiye aliyeongoza misa hiyo, alisema: “Kutakuwa na amani ya kweli kama kutakuwa na haki ya kweli, na hakuna amani bila ya haki ya kweli, na haki ni katika maelewano hayo”.

Mungu alitaka ujumbe huu uwafikie wale ambao hawaheshimu haki za wengine, ukiwa unatolewa katika ardhi yao. Kihistoria siasa za Zanzibar huwa ni chanzo cha machafuko na mvurugano, zaidi hutokana na haki kutoheshimiwa.

Turudi nyuma kidogo: Januari 27, mwaka 2001, kulitokezea mauaji Zanzibar, makumi ya watu waliongia barabarani kufanya maandamano ya amani, walipigwa risasi na kuuawa.

Wengi walikuwa ni wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), walioamua kupaza sauti zao kwa kile walichodai kutokea wizi katika Uchaguzi Mkuu  wa mwaka 2000, hivyo waliamini haki haikutendeka.

Badala ya vikosi vya usalama kulinda waandamaji, waliotumia haki yao ya kikatiba kufanya hivyo, lakini ikawa kinyume chake, walitumia risasi kupambana nao, watu wengi walikufa kisiwani Pemba na wengine wakakimbia na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani.

Hadi sasa wapo wakimbizi wa Kizanzibari ambao wanaishi Mombasa na Somalia, pia wapo waliotumia nafasi ya machafuko kukimbilia mbali zaidi. Chanzo kilikuwa ni siasa chafu ambazo hazikutenda haki.

Sitaki kulazimisha maneno ya Askofu Shao kwamba yalikuwa yanalenga moja kwa moja kuzungumzia matukio kama haya, ila naamini Askofu Shao alikuwa anazungumzia ‘amani ya kweli na haki’.

Hata kama hakutoa matukio hayo kama mifano hai, lakini matukio ya mifano hai yapo katika nchi ya Zanzibar, matukio ya kukosekana kwa haki hatimaye amani ya kweli inaondoka.

Askofu Shao alikuwa anahimiza amani ambayo inapatikana zaidi pakiwepo haki, mimi nahimiza hicho hicho, lakini nitakuwa na mifano hai ili kuonyesha vipi amani hukosekana pakikosekana haki.

Katika historia za chaguzi za Zanzibar, nyingi ya hizo lazima mutashuhudia majeruhi, vurugu na matukio mengine ambayo hayana na ulazima wa kutokea.

Zanzibar hukosekana haki hadi kufikia hatua ya amani kuchafuka na jirani akagoma kumzika jirani yake, au ndugu akakacha kuhudhuria harusi ya ndugu yake, haya yote hujitokezea kwa sababu ya dhulma inayotengwa kwa mwanvuli wa siasa.

Kila mtu anaelewa nini kilitokea Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, pale waangalizi wote walipokubali uchaguzi ulikuwa huru na haki. Bahati mbaya katika jaribio lililofanikiwa na kuipindisha haki , Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) , Jecha Salim Jecha, akafuta matokeo ya uchaguzi.

Ni tukio lililotikisa uimara wa amani yetu , Mungu kasaidia tukaendelea kuishi kwa hamkani, lakini pakafumuka chuki za wafuasi wa vyama vikubwa vya kisiasa—CUF ,na CCM kuchukiana kupita mipaka.

Na ndio athari ya kuzikanyaga haki za wengine, hata kama vita vya silaha havikufumuka, lakini mtetereko lazima utakuwepo, maanake hakuna amani bila ya haki ya kweli.

Alhamisi ya tarehe 4, Febuari ya mwaka 2017, wakati joto la uchaguzi likiwa bado linawaka Zanzibar, watu waliofunika nyuso zao wakiwa na silaha za jadi na moto, walipita katika  maeneo ya Kilimani Mjini Zanzibar, wakiwa katika gari lenye namba za usajili KM 155.

KM ni kifupi cha KMKM-Kikosi Maalum cha Kuzuwia Magendo. Ufupi ni kwamba ni gari la kikosi cha Serekali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kinacholinda rasilimali za Zanzibar kupitia ardhini na baharini.

Mchana kweupe, Alhamisi ya siku hiyo, watu ambao wafunika nyuso—almaarufu Mazombi), walikuwa wamefunika nyuso, hadi kufika jioni walikuwa tayari wameshaharibu na kujeruhi watu katika maeneno kadhaa walimopita.

Kesi kama hizi za wafunika uso kupita na silaha za moto mitaani wakati nchi haiko katika vita, wala makundi ya waasi, tena wanakuwa na gari la Serikali, na nyuso wamefunika, inakuwa ngumu sana kumuaminisha mtu kwamba Serikali haihusiki au haiwajui watu hawa!

Askofu Shao alikuwa na kila sababu ya kuhimiza haki akiwa katika ardhi ya Zanzibar, kwa sababu hadi sasa tuna mkwamo wa kisiasa kwa sababu ya haki za wengine kuchezwa danadana.

Nimeambatanisha picha ya Mazombi hao katika makala haya, ili muelewe kwa upana ninachokusudia kukisema. Sio hadithi za kutunga, wala picha za waasi wa Afrika ya Kati, ilikuwa ni Zanzibar na hali hujitokeza hivyo hivyo kila uchaguzi mkuu ukaribiapo.

Ipo haja kubwa kwa viongozi wegine wa dini na taasisi nyengine kuendelea kuhimiza haki katika visiwa hivi, kwa sababu wakati mwengine ni jambo linalopuuzwa, na kuishia kuigharimu Zanzibar kama Januari 27, 2001.

Ikiwa haki ya aina yoyote ambayo inamhusu binadamu itavunjwa, huhatarisha uimara wa amani yenyewe, hatuwezi kujigamba tuna na amani, wakati kuna vitendo vya ajabu ajabu vinafanyika.

Disemba 11, mwaka 2017, Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Awadh Ali Said, alipokuwa akizungumza na chombo kimoja na habari , alisema: “Mvunjaji mkubwa wa haki za binadamu, ni Serikali kwa sababu maisha ya binadamu yametawaliwa na utaratibu wa kiserikali”.

Awadh anasema: “Taasisi kama polisi, mahakama na nyengine, ambazo husimamia haki za binadamu, zinastahiki kuundwa katika utaratibu utakao wafanya  kuwa huru na kufuata weledi na maadili ya kazi zao”.

Awadh amelizungumzia jambo hilo katika upande mmoja,  upande mwengine ni sawa na kusema; hizi taasisi ambazo ni za kiserekali na zinasimamia haki za binaadamu zikitumika vibaya, zitakuwa zinakanyaga hizo haki badala ya kuzisimamia.

Natamani tuuwanze mwaka mpya kila mmoja akielewa nama ya kuchunga haki ya mwengine, sio kwa serekali tu hata mtu mmoja mmoja ambaye anaamini hamtendei haki mwingine, basi ifike wakati wa kujirekebisha ili tuishi kwa amani.

Tusisahau amani ya moyo ambayo nayo ina umuhimu wake, wapo wasiochafua amani ya taifa,  lakini huchafua amani ya mioyo ya wengine, pengine kwa vitendo vyao vibaya dhidi ya wengine, pia nao wanatakiwa kuacha.

Kwa sababu wakili Awadh anasema zipo kesi za watu kuvamiwa katika majumba yao,  usiku wa manane,anatolewa nje na kupigwa, wegine hujeruhiwa vibaya, hadi wegine hufariki.

Ingawa ujumbe wa Askofu Shao aliutoa akiwa Zanzibar, ila Tanzania nzima inapaswa kuubeba ujumbe wake kwa kuufanyia kazi kivitendo. Katika ngazi za serekali na hata mtu mmoja mmoja.

0657414889