Home Latest News UZOEFU WA MBOWE KATIKA SIASA TISHIO KWA WATAWALA

UZOEFU WA MBOWE KATIKA SIASA TISHIO KWA WATAWALA

891
0
SHARE
Rais John Magufuli (kulia) akisalimiana na Freeman Mbowe.
NA INNOCENT EZEKIA

Nikiwa mwanafunzi wa Kidato cha Tano, zaidi ya miaka 12 iliyopita, jina la Freeman Mbowe lilisikika sana, ikiwa ni pamoja na majina ya wanasiasa wengine kama Prof Mark Mwandosya, Jakaya Mrisho Kikwete, Dk. Salim Ahmed Salim.

Nikajikuta nimekuwa mfuatiliaji mkubwa wa siasa za hapa Tanzania. Nikawa mnunuzi wa magazeti yanayoandika mambo ya siasa—hasa gazeti la Rai (Nguvu ya Hoja) na The Guardian.

Kuna wenzangu watu walioniona kama kichaa, hasa wanafunzi wenzangu, na wengine walinishangaa, lakini kuna wengine walipenda aina ya maisha niliyochagua, nadhani popote pale walipo watakuwa mashuhuda wa huuu ujumbe.

Kutokana na kufuatilia sana mambo ya siasa nikiwa mwanafunzi, kukawa na utani wa hapa na pale juu ya baadhi ya wanasiasa, lakini Mwalimu wangu mmoja maarufu sana wa somo la jiografia—Mwalimu  Matovu, siku moja niliuliza swali, baada ya kunijibu akasema kuwa huyu bwana anauliza kama Mbowe. Ndio Mwanzo wakubandikwa jina la  Mbowe. Mwanzoni ilinipa shida, lakini baadaye nikazoea na kulichukulia kawaida. Hiyo ilinifanya nianze kumfuatilia huyu mtu aitwae Mbowe, nimsome nifuatilie mikutano yake, maandiko yake na zaidi nimuone uso kwa uso—kitu  ambacho nilifanikiwa kutimiza nilipokutana naye ana kwa ana. Baada ya kumfuatilia kuanzia anavyojenga hoja na kutumia jukwa ipasavyo, nilikubali moyoni kuwa jina walilokuwa wamenipa wanafunzi wenzangu,  lilikuwa nikubwa mno na zito sana kwangu kulibeba.

Lengo sio kutoa historia yangu na ushabiki wangu kwa huyu mwanasiasa, hiyo nitafanya wakati mwingine, bali nataka kuendeleza hoja ya uwenyekiti wake unavyovuma kwa kasi ya ajabu miongoni mwa wa wadau wa siasa za hapa nchini.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepitia mikononi mwa wenyeviti watatu hadi sasa, tangu mwaka 1992 wakati wa kamati ya kwanza yakuanzisha chama hicho hadi leo 2017, ikiwa ni pamoja na waasisi wawili aliyekuwa Gavana wa Kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania, Edwin Mtei, aliyekuwa Naibu Gavana wa BoT, Bob Mohamed Makani (marehemu).

Kwa nini waasisi wa chama hiki walikuwa wafanyakazi wa zamani wa Benki Kuu, hilo nalo sio mahala pake leo, na sasa Freeman Mbowe, katika awamu hizo tatu za uongozi wa hawa wanamageuzi, kulitokea mabadiliko makubwa ya kimuundo na namna ya kuwafikia watu na kujenga ushawishi mkubwa kwa jamii ya Kitanzania, ili waweze kuaminiwa na waweze kuchaguliwa na kushika hatamu za dola. Mageuzi makubwa sana yameonekana katika kipindi cha Mbowe  katika maeneo yafuatayo:

Madadiliko ya rangi za bendera kutoka rangi moja ya blue bahari hadi kuwa na rangi zaidi ya moja, nyeupe, nyekundu, blue na nyeusi. Wanasaikolojia wanajua athari za rangi katika ushawishi au kumvutia mtu, ubunifu mkubwa uliofanywa wakubadili rangi ulikuwa ni miongoni mwa mbinu bora zakuteka akili za watu katika muonekano mpya wa chama, na kwa kiasi kikubwa mbinu hiyo imefanikiwa sana kwani mchanganyiko wa bendera za chama hiki zinavutia kwa macho.

Uvaaji wa nguo maarufu kama Gwanda, hili nalo ni moja ya ubunifu wa hali ya juu kwa watalaamu walioamua kuja na vazi hilo, kwani limekuwa kama alama ya chama. Mtu awaye yote akionekana amevaa vazi lenye nasaba na gwanda, watu humtafsiri haraka haraka kuwa ni mwana Chadema. Huo ni ubunifu mkubwa sana uliofanywa na wana mkakati chini ya uongozi wa Freeman Mbowe na hivyo kupelekea vijana kujinasibu kwa mavazi hayo na hata madukani mavazi hayo yanauzwa kwa bei ghali. Huo ni mwendelezo kwa kujiwekea utambulisho kwa Chadema popote pale panapokuwa.

Tatu, cheo cha Kamanda na ukamanda, kwa mara ya kwanza mwaka 2005, Chadema kilisimamisha mgombea katika nafasi ya urais, na Mbowe ndiye aliyechaguliwa kupeperusha bendera ya chama hicho. Alitumia njia kadha wa kadha kuwafikia wapiga kura, lakini njia iliyokuwa ya burudani ni njia ya anga—akaitwa Kamanda wa Anga, na vijana wanana Chadema wakawa wanajinasibu kama Makamanda na hata neno kamanda likaanza kutumika kama neno la salaam. Sasa neno hilo linaishi miongoni mwa vijana wengi na limekuwa kivutio kwa vijana wengi wakiwa wanajinasibu kama wapamabanaji—makamanda hodari katika siasa za Tanzania.

Nne, vijana wengi hujiunga na siasa hasa za upinzani, mathalani wasomi wa vyuo vikuu, ndio wakati ambao vijana kama Zitto Kabwe, walipewa nafasi kubwa ya kufanya siasa na walijulikana vilivyo, kwani vijana walipata nafasi kubwa sana, hivyo kushawishi vijana wenzano kujiunga na Chadema.

Kuomgezeka kwa uwakilishi bungeni, na katika mabaraza ya uwakilishi ya wilaya, miji manispaa, majiji kwa mikakati na mipango mikubwa uongozi wa Mbowe na wenzake, tofauti na awamu za viongozi waliotangulia, ambapo uwakilishi ulikuwa mdogo sana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uwakilishi katika serikali za mitaa. Haya matunda sio ya kubeza hata kidogo.

Sita, ongezeko la wanachama na kusambaa kwa chama karibu nchi nzima, chama kilionekana  kama chama cha eneo fulani tu , lakini leo ukitembea hata katika vijiji vya ndani ndani, utaona bendera za Chadema zinapepea, na kuna watu wanajua habari za chama hicho.

Mwenyekiti Mbowe

Kwa muda mrefu kumekuwa na hoja kutoka kwa wana CCM kwamba kwa nini Mbowe amekuwa mwenyekiti kwa muda mrefu kama kwamba ni mfalme na kwa nini hataki kupisha watu wengine wakiongoze chama hicho.

Je, CCM wanakitakia mema Chadema? Jibu ni wazi ni hapana. Wanafanya hivyo ili kukiondolea Chadema uongozi wenye uzoevu chini ya Mbowe. Mambo yafuatayo yameongeza shida katika chama tawala—ruzuku ya chama tawala imepungua baada ya Chadema kuongeza viti vingi bungeni na katika mabaraza ya serikali za mtaa kufikia hata baadhi ya maeneo nyeti na mikoa mikubwa, kuwa chini ya upinzania, mathalani, Jiji kubwa la kibiashara—Dar es Saalam na majiji ya Mbeya, Arusha, na manispaa za Moshi na Bukoba. Hapa lazima Mbowe apingwe na aonekane king’ang’anizi ndio maana wanamfananisha na mfalme. Nia ni kuwafanya wana Chadema wamwone hafai wamtupe chini, ili iwe rahisi kwa cha tawala kurejesha ufalme wake.

Mbowe ni kiongozi mwenye misimamo usioyumba—hasa  kwa nafasi yake kama Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni. Hili nalo nikikwazo kikubwa kwa chama tawala. Wanafikiri kwamba kuwa na mtu imara na jasiri kama Mbowe, kutaendeleza msuguano mkubwa kutoka kambi ya upinzani na kwa jinsi upinzani unavyosimama kwa umoja, imekuwa vigumu sana kuwagawa chini ya uongozi wa Mbowe. Kuondoka kwa baadhi ya Wabunge kutoka Chadema ni mbinu moja wapo ya kumdhoofisha Mboye kisiasa.

Mbowe amekuwa kiungo muhimu sana katika umoja wa Katiba ya wananchi ( Ukawa), pamoja na baadhi ya wenyeviti wenza kuchechemea, yeye ameendelea kusimama imara, hivyo kwa vyovyote ni mtu asiyetakiwa na chama tawala—maanan ni sehemu ya kikwazo cha maslai ya chama tawala

Mbowe ni mjuvi wa siasa za majukwaani, ni miongoni mwa wanasiasa wachache sana hapa nchini, wanaojua kujenga hoja mujarabu wawapo jukwaani, ni mzungumzaji mzuri sana, hivyo kumzima kwakupiga kelele kuwa  hafai, ni ndio kiwango cha uzito wake katika kujenga hoja na ni mwiba kwa CCM. Inabidi aondolewe katika majukwaa ya kisiasa kwa namana yoyote ile. Kuhamahama kwa wanachama hasa kutoka Jimbo la Hai analoliwakilisha bungeni, wanachama wa Chama cha Mapinduzi wanamnyooshea vidole Mbowe kwamba ndiye chanzo cha wanachama kikimbia Chadema.

Lakini pia ni jambo la kujiuliza toka lini CCM kiliamua kupigia kelele uwenyeviti wa Augustine Mrema wa TLP, John Cheyo wa UDP na akina Dovutwa, Prof Lipumba na wengine wa aina hiyo.  Jibu,ulalo kichwani mwako. Akili za kuambiwa changanya na zako.

Lakini hii haina maana kwamba Mbowe hana mapungufu. Yeye ni binadamu kama binadamu wengine anayo mapungufu na tena yawezekana nayo yanachangia chama kutokwenda kwa kasi kama ilivyokuwa imekusudiwa.

Mbowe anazo changamoto ambazo anapaswa kuzifanyia kazi. Chadema kisiendelee kuamini katika mbinu zilezile katika siasa za ushindani. Hiyo inawapa mwanya washindani kupitia mkondo huo uliozoeleka. Ni kama timu shindani ambazo makocha wanasomana mbinu na timu moja ikiendelea na mtindo mmoja katika mechi zake zote—isitegemee kushinda kila mechi.

Mbowe ni mwanadiplomasia aliyepitiliza, na huu umekuwa ni  mwanya wa washindani wa chama chake kupenya katika tundu la udhaifu huo, na udhaifu huu umekuwa na manufaa chanya kwa chama tawala. Mbowe anaamini katika mzungumzo na huwa anaahirisha mipango mikubwa ya chama katika hatua za kuchukua kukabiliana na dhuluma ya aina yoyote. Hii inakipotezea nafasi chama chake katika medani ya ushindani. Udhaifu huu umekuwa ni mtaji kwa chama tawala na wao wanalijua hilo.

Mbowe bado ni muumini wa kikundi cha watu wachache miaka nenda rudi, moja ya maeneo magumu na yasiyopendwa na viongozi wengi wa Chadema hasa wale wanamzunguka Mwenyekiti—wamekuwa walewale na mawazo yaleyale—hivyo  kuendea kuwaamini kwa kila kitu, wanachukua udhaifu huo wakuaminiwa na kutenda ndivyo sivyo, na kuwaumiza wapenzi wa chama chao walioko sehemu mbali mbali nchini na nje.

Mwisho bado Mbowe ni muhimu sana kwa maendeleao ya upinzani Tanzania, hivyo asibezwe kwa  juhudi kubwa alizofanya na anazoendelea kuzifanya katika kuujenga upinzani imara nchini.

 Mungu ibariki Tanzania na viongozi wake wote

         innomutas@yahoo.com/0752936731