Home Habari VIONGOZI 1,000, NDUGU ZAO KUBANWA NA SEKRETARIETI YA MAADILI

VIONGOZI 1,000, NDUGU ZAO KUBANWA NA SEKRETARIETI YA MAADILI

538
0
SHARE
NA FRANCIS GODWIN, IRINGA

ZAIDI ya viongozi 1000 wanatarajiwa kuhojiwa na Sekretarieti ya Maadili ya  Viongozi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, pamoja na ndugu zao wa karibu ambao wana mali zilizo nje ya uwezo wa vipato vyao.

Mbali na kuwahojiwa, pia watumishi wa umma ambao kila mwezi hutoka patupu bila  kupokea chochote katika mishahara  yao kutokana na madeni mengi, nao watafikishwa katika Tume hiyo kujieleza namna wanavyoweza kuishi bila mishahara.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kanda, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Nyanda za  Juu Kusini, Erick Mbembati, wakati akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa maaadhimisho ya Siku ya Maadili, mkoani Iringa.

Alisema jumla ya viongozi 500 wamekwisha hojiwa kuhusiana na maadili na  sasa ni zamu ya viongozi zaidi ya 1,000 ambao wamekuwa hawatoi taarifa za kweli, hivyo kutokana na hali hiyo wamekuwa wakizifanyia uhakiki taarifa hizo kwa kuzifanyia uchunguzi zaidi ili kujua  ukweli wa taarifa wanazotoa watumishi  hao.

Hata hivyo, alisema baada ya Rais Magufuli kusaini mabadiliko ya sheria hiyo, hivi sasa wanao uwezo wa kumuita kiongozi yeyote kwa hati maalumu, kufika mbele ya Tume kwa gharama zake na kuhojiwa.

“Kuna mchakato wa kuandaa sheria ya  mgongano wa kimasilahi ambayo iwapo  itapitishwa na Bunge, basi itasaidia  zaidi kuweza kufanya kazi hiyo ya uhakiki  wa mali za watumishi wa umma bila kuwepo  kwa chembe ya mgongano wa kimasilahi.

“Tatizo kubwa lililopo sasa ni mgongano wa  kimasilahi ya mtu binafsi na masilahi ya umma kwa kuacha yale ya umma na  kutimiza masilahi binafsi,“ alisema.

Mbembati alisema sheria hiyo iliyosainiwa na Rais Magufuli Julai 7, mwaka 2016, inawapa nafasi ya kuwabana rafiki na ndugu wa karibu kwa mali wanazomiliki ama mihamala ya kifedha  inayopitishwa kwa rafiki na jirani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, aliwataka watumishi wa  umma kujitambua ili kuelekea katika uchumi wa kati.

Alisema maadhimisho hayo mkoani  Iringa yaliyobebwa na kauli mbiu: ‘Wajibika piga vita rushwa, zingatia maadili, haki na utawala bora kuelekea  uchumi wa kati’ –ni vyema kila mmoja  kuzingatia na pale ambapo walijikwaa, basi  kujirekebisha.

“Rais Magufuli amekuwa mbele katika  mapambano dhidi ya rushwa na kuona Taifa   linapiga hatua katika nyanja mbali mbali  ikiwemo ya viwanda, hivyo kwa pamoja   hatuna budi kuungana kutekeleza majukumu  yetu na kufanya kazi na kujiepusha na rushwa pamoja na maadili yasiyofaa kwa  watumishi wa umma,” alisema.

Mkuu  huyo wa mkoa  pia aliwaomba viongozi wa dini kutumia nafasi zao kutoa  elimu kwa waumini wao dhidi ya rushwa,  pamoja na ukuzaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja pamoja na kuwajenga vijana katika  uadilifu, ili kukuza uchumi wa viwanda  na  kuwaepusha vijana na ulevi uliopindukia.

Mwakilishi wa Kanisa la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Emma  Mwalusamba, alisema changamoto ya maisha ya sasa, ni watu wengi kutokuwa na hofu ya Mungu na ndio sababu ya mambo kwenda  ndivyo sivyo.

Alisema kuwa maadili katika jamii  yanaendelea kumomonyoka, kutokana na watu kutokuwa na hofu ya Mungu na  kukosa upendo miongoni mwao, hivyo kuna haja ya kila kiongozi na kila mmoja,  kujitathimini katika utendaji kazi,  kuepuka kuomba rushwa kwa wale  wanaohitaji huduma.

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Iringa, Aidan Ndomba, alisema rushwa inatokea pale ambapo mtu mwenye kuhodhi madaraka, anatumia uwezo wa kuamua jambo kwa vile anayo sheria, kanuni inayompa mamlaka, lakini hufanya hivyo pasipo  kuweka wazi sababu za kutoa uamuzi huo,  wala kutokuwa tayari kuelezea sababu za  kufanya hivyo.