Home Latest News VYA KAIZARI NA VYA MUNGU VINAPOTIFUANA KISIASA

VYA KAIZARI NA VYA MUNGU VINAPOTIFUANA KISIASA

560
0
SHARE
Askofu Zakaria Kakobe
Na Joseph Mihangwa

“Rushwa inalitafuna taifa letu; sasa [imekuwa] ni kama kitu cha kawaida; uchu wa madaraka na sera za ubinafsi zimetawala toka juu mpaka chini; mshikamano wa kitaifa umeangamizwa, Wabunge hawapendani bungeni; uadui kati ya Wabunge umeruhusiwa kuvuruga demokrasia ya uwakilishi, kana kwamba upinzani ni dhambi; Viongozi [dhaifu] hawataki kung’atuka madarakani, kwa hofu ya kukosa ulaji”.

Haya ni maneno ya Mchungaji mmoja wa dini katika moja ya mahubiri yake miaka minne iliyopita wakati wa kuadhimisha ibada Kanisani.

Kisha akaendelea kusema: “Ufa kati ya walio nacho [matajiri] na wasiokuwa nacho [masikini], unazidi kupanuka; tumeua Azimio la Arusha lililohimiza upendo, usawa, haki na maendeleo kwa wote; badala yake tumeleta Azimio la Zanzibar [1992]. Sasa tumehama kutoka Azimio la Arusha kwenda Azimio la Rushwa”; rushwa inalitafuna Taifa na watu wake, kinyume na mapenzi ya Mungu”.

Akaendelea kusema: “Utamaduni na maadili ya taifa yameangamizwa, eti tu kwa sababu utandawazi haukwepeki! Mbona mimi moyo wangu haujatekwa na utandawazi huo?  Tanzania sasa si kisiwa cha amani tena, bali ni kisiwa cha maovu, maovu ya Sodoma na Gomora”.

Kwa ujasiri mkubwa wa ulimbwende na kujiamini, aliendelea, “Serikali imeshindwa kushughulikia maovu haya.  Taifa linaelekea wapi?  Lazima tukemee yote haya.  Na [mimi] sitabadili msimamo [wangu] huu, mpaka nitakapoona mambo yamekuwa shwari. Siogopi kusema hivyo, eti [kwa sababu] kuna mashushushu [watu wa Usalama wa Taifa] hapa; simwogopi mtu, mimi na kazi yangu; naongea kwa uhuru wote kama mtu wa Taifa huru la Mungu.  Lazima tuhubiri habari njema kwa jamii”.

Kwa uelewa wa wengi, na kwa kuzingatia Katiba ya nchi yetu inayosema kwamba dini ni suala la mtu binafsi, tunaweza kuuliza: “Tangu lini dini na siasa zikawa chanda na pete?  Je, haikuandikwa kwamba “Cha Kaisari mpeni Kaisari, na cha Mungu mpeni Mungu?”.  Je, huko si kuchanganya dini na siasa?

Lakini mambo haya hayakuanza na mahubiri hayo, kwani miaka kadhaa kabla ya hapo, Baraza la Maaskofu Tanzania [TEC], katika ujumbe wake wa Kwaresma uliopewa jina “Heri Kutoa Kuliko Kupokea”, nalo lilitoa tamko kama hilo juu ya hali na hatima ya nchi katika mfumo wa soko huria na siasa ya vyama vingi, kwa kubainisha kukithiri kwa mfumo wa uchumi usiojali, mmomonyoko wa maadili, wizi na rushwa, utapeli na uharibifu wa mazingira.

Vivyo hivyo, Baraza la Makanisa [CCT], nalo lilibainisha mambo kama hayo kwa kulaani na kukemea hali ya kuongezeka kwa siasa za kujuana [Politics of Patronage], mshikamano kati ya matajiri wakubwa na kada ya watawala dhidi ya wanyonge; tofauti ya umilikaji mali na utajiri wa nchi, kati ya wenyeji na wageni; kukosa kazi kwa vijana, ujambazi, ujangili, rushwa, madawa ya kulevya, umalaya na maovu mengine katika jamii.

Matamko haya yanaweza kuonekana kama ya kuwashambulia utawala, na pengine yanaweza kuonekana kupingana na maandiko ya dini yanayotaka wafuasi wake waamini  kwamba “Watawala wote huwekwa madarakani na Mungu,  na hivyo kupinga ya watawala ni kupingana na mpango wa Mungu” .

Hivi karibuni, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, imezionya taasisi za dini kuzingatia madhumuni ya kusajiliwa kwake na mipaka ya kazi zake.  Japo onyo hilo halikufafanua nini kilichojiri hata kutolewa kwa kauli hiyo, lakini imetokana na Viongozi wa dini kuikosoa Serikali mara kwa mara, na kilele chake ilikuwa Krismasi mwaka huu.

Kama hivyo ndivyo, yanazuka maswali mengi kuliko majibu kama vile:  Kwa nini taasisi za dini huziandama na kuzitahadharisha Serikali?.  Nini nafasi ya dini katika nchi na utawala?

Katika mjadala huu, nitatumia neno “Kanisa” kumaanisha waumini wa dini zote za kweli, na si jengo la kuabudia pekee. Waumini au Kanisa hushiriki katika shughuli zote za kiserikali na kijamii, ikiwa ni pamoja na kuwachagua viongozi, kulipa kodi, na hivyo wanaguswa na mambo yote ya kijamii kama watu wengine katika maisha yao.

Ndiyo maana, viongozi huapa kwa misahafu kabla ya kushika madaraka na kuahidi kutenda haki kwa jamii kwa imani kwamba “Mungu wa Misahafu ni Mungu wa Haki na Upendo.” Viongozi huapa kuwatumikia watu wa Mungu ndani ya Taifa la Mungu.

Tunaposema—cha Kaisari mpeni Kaisari, na cha Mungu mpeni Mungu, haina maana ya Kanisa kutowasemea wanyonge wanaokandamizwa; wala kwamba,  Kanisa halina haki au uwezo wa kuzikemea taasisi zinazosababisha unyonge huo.  Lakini, ni kipi hiki “cha Kaizari” na ni kipi “cha Mungu” kwa maana hii?.

Alipoonyesha fedha na kuainisha aina mbili za utii, kwa Mungu na kwa Kaizari, Yesu Kristo alikuwa akiwaambia wasikilizaji wake kuwa wasichanganye mambo; wala kubadilisha utii wao kwa kumpa Mungu heshima ambayo ni ya mwanadamu na kinyume chake.  Kufanya hivyo ni kuvuka mipaka, kwani kila mmoja ana mahali pake katika maisha ya wanadamu.  Baya zaidi ni kuwalinganisha hawa wawili—Kaisari na Mungu, kwa mlingano ulio sawa–huku ni kupotoka; huko ndiko kuabudu watawala na serikali, kana kwamba wao hawakosei, licha ya udhaifu na mapungufu ya kila aina. Kufanya hivyo, ni kuifanya serikali au mfumo wa kiserikali, usiwe mfumo ulioundwa na wanadamu kwa kutumia akili na ujuzi waliopewa na Muumba wao mwenyewe.

Pamoja na kwamba Kanisa halipaswi kujiunga au kujiaasisi kama chama cha siasa, lakini halina budi kushiriki kikamilifu kuwaambia wananchi wote—maana ya haki na ukweli na kuitetea haki na amani kwa dhati na kupinga yote yanayotendwa ama na kiongozi mmoja mmoja, au kwa ujumla kama serikali; na kwamba, kwa maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere:  “Kanisa likubali kuwa maendeleo ya watu maana yake ni maasi.  Katika historia, watu hufikia hatua ya kuyakataa mambo yanayowabana katika uhuru wao kama binadamu.  Kanisa lisiposhiriki kwa vitendo katika mapambano ya kuondoa utaratibu wa maisha na wa uchumi unaowadidimiza watu kwenye umasikini, uonevu na unyonge, basi Kanisa haliwezi kuwa na uhusiano na maisha ya binadamu, na dini itakuwa kama ni mkusanyiko wa imani za ushirikina zinazokubaliwa na wenye hofu tu”.

Mwalimu anaendelea:  “Lazima idhihirike kwamba Kanisa linashambulia wazi wazi mtu  au kikundi chochote  [ikiwamo Serikali na watawala] kinachosaidia kudumisha unyonge huo wa mwili na roho, bila ya kujali misukosuko inayoweza kutokea kwa kanisa au kwa wafuasi wake.  Maana ikiwa Kanisa halipingi maovu yaliyoko, basi kuendelea kuwapo kwake, na dini yoyote, kutamaanishwa na kuendelea kwa dhuluma.”

Kanisa lisipotetea haki, usawa na upendo, na kuyakemea maovu hayo, litakuwa linakosea, kwani hii ni sehemu ya unabii liliokabidhiwa kutimiza. Nani anasema watawala wote na serikali, huwekwa madarakani na Mungu?  Kama ni hivyo je, utawala wa Hitler nao uliwekwa madarakani na Mungu?  Na wa Idi Amini je? Marcias Nguema na Mobutu Seseseko?.

Anachoagiza Mungu na kuweka madarakani sio serikali au utawala wenyewe, bali Mungu anaamuru mifumo wa Serikali inayofaa.  Serikali inayotimiza matakwa ya Uongozi na Utawala Bora na kukubalika, basi serikali hiyo inastahili kuitwa imewekwa na Mungu, nayo itatambuliwa kwa matunda yake.

Ni kwamba, serikali inaposhindwa kutimiza majukumu iliyopewa, serikali hiyo inapoteza mamlaka yake na haki ya kutawala; na hivyo haiwezi kudai kuwa imewekwa madarakani na Mungu.

Hapo, inakuwa ni jukumu la Kanisa kuamka na kuieleza ukweli, siyo kwa sababu Kanisa linataka kujihusisha na mambo ya siasa, au kuingilia kazi za serikali; bali ni kwa sababu lina wajibu wa kusimamia aina ya mfumo bora wa serikali itakiwavyo na inayofaa.

Ni wajibu wa Kanisa kutetea haki katika jamii kwani, ‘Haki huinua Taifa, bali dhambi—kutotenda  haki ni aibu kwa watu wote’. Bila haki hakuna amani; pasipo amani, hakuna utawala unaoweza kudumu; na pasipo utawala bora ni maangamizi kwa taifa.

Maovu ni chanzo cha kuvurugika kwa amani.  Ni Mungu yupi anayependa maovu na vurugu?  Ni jukumu la Kanisa kusimamia mfumo wa aina bora ya serikali itakiwayo na Mungu na watu wake.  Je, Kanisa linyamaze tu wakati jamii inaangamia?

Kulichukulia Kanisa kama adui wa wanasiasa, siasa na watawala, ni kupungukiwa uadilifu, hekima na uwezo wa kufikiri.  Mwalimu Nyerere aliweka utaratibu wa kukutana na viongozi wa dini na wazee mara kwa mara, ili kuzungumzia mustakhabari wa Taifa na jinsi nchi inavyokwenda.

Kwa nini watawala wengi wanawaogopa viongozi wa dini,  na wakati mwingine kuwakemea eti wasichanganye siasa na dini?  Ni kwa sababu unabii unawatisha; wanawaogopa viongozi wa dini wanapotoa unabii.

Kwanza, ni ile hofu ya kunyang’anywa ukuu na madaraka kutokana na ukweli unaotolewa, na pili, wanaguswa na kufadhaika wanapoonywa juu ya dhambi na maovu katika ofisi zao.

Ili kujihami, wanatumia rungu la mamlaka yao waliyokabidhiwa na watu wa Mungu (wapiga kura), “kuwatandika” viongozi wa dini kwa kutoa hotuba kali kali za kujiponya.

Kanisa ni taasisi tata, na kiongozi wa dini anayeogopa kuingia matatani, hafai na ni vyema akajiweka mbali na kazi ya Kanisa.

Je, dini na siasa zinaweza kuchanganywa?. Jibu linategemea maana na aina ya siasa inayozungumziwa.  Kama siasa maana yake ni uwanja wa tamaa mbaya ya madaraka na kujitajirisha binafsi, basi Kanisa haliwezi kuchanganywa na siasa ya aina hiyo. Lakini kama siasa ni njia ya kutafuta utawala wa haki na amani katikati ya watu, hapo Kanisa haliwezi kujiepusha na jambo hilo. Na kwa kuwa Kanisa ni sehemu ya jamii, ni wajibu wake kushiriki katika mambo yanayogusa maisha ya watu kisiasa, kiuchumi na kijamii; na kama anavyosema Mwalimu: “Kanisa litambue kwamba iko haja ya kuleta mapinduzi katika hali za maisha ya watu, na Kanisa lenyewe lichukue sehemu kubwa ya wajibu wa kuyaongoza mapinduzi hayo”.  Bila kupaza sauti, Kanisa litayaongozaje Mapinduzi?

 

jmihangwa@yahoo.com/0713-526972