Home Makala KAMA TUNAUPENDA MUUNGANO, TUFUTE KERO ZAKE

KAMA TUNAUPENDA MUUNGANO, TUFUTE KERO ZAKE

197
0
SHARE

NA RASHID ABDALLAH


“Napenda niwakumbushe wenzangu wa Jamhuri ya Muungano na watendaji wa pande zote mbili,  kwamba mambo yanayohusu  muungano yasifanywe na upande mmoja”, hayo ni maneno ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohammed Shein aliyoyatoa Januari 4 mwaka huu.

Siyo lazima uwe umezaliwa Chake Chake (mji maarufu kibiashara kisiwani Pemba) au umezaliwa Mji Mkongwe (mji wa kitalii) , inahitaji tu uelewa na roho ya kibinadamu ili kukubali kwamba Muungano tulionao umezongwa na kero za muda mrefu.

Nakusudia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, ulioundwa na watu wachache mno hata raia wa mataifa haya wawili hawakushauriwa wala kuulizwa, ikiwa wanataka Muungano au la. Baadae ndipo tulipopata  taifa la Tanzania.

Haukuwa tu ni muungano wa kimya kimya, pia umekuwa ni muungano watu kero na matatizo mengi ndani yake, bila ya kusahau hauweleweki umekaaje kaaje hata ukijaribu kuuweka kitako au  kuusimamisha.

Sisemi haya kwa sababu mimi ni mpinzani wa Mungano, napaswa kueleweka vizuri, kwanza nakubali kwamba kuna faida nyingi tu ndani ya muungano zimepatikana, lakini hatuwezi kuzikataa kero na sintofahamu za muungano.

Elimu yangu ya msingi na upili nimeipata kwetu Zanzibar lakini elimu iliyobakia ikiwemo hii ya uandishi wa habari nimeipata Tanzania Bara, katika mkoa wa Morogoro, hivyo sina kiburi cha kusema muungano hauna lolote hauna chochote zaidi ya hasara,nikisema hivyo nitakuwa mnafiki.

Huko nyuma kuliundwa tume nyingi ili zisimamie kile kinachoitwa kero za Muungano,  baada ya malalamiko kuzidi na kero kuzidi pia, kulikuwa na mambo machache ya muungano lakini yakaongezwa kinyemela hadi yakawa mengi.

Katika tume hizo zipo zilizofanikiwa kupunguza kero za muungano, laini hakuna tume iliyofanikiwa kuondoa kero zote, zilishindwa kwa sababu si kazi rahisi sana punda dume kumgeuza ndama jike.

Ndio maana hadi sasa, punde tu tulipouwanza mwaka mpya, tena kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya urais wake, Dk Ali Mohammed Shein amelilia usawa katika huu muungano.

Rasimu ya Katiba mpya ya Jaji Warioba ndiyo iliyokuwa suluhisho la wazi juu ya changamoto za Muungano, bahati mbaya iliingia katika mikono ya wachumia tumbo, wakaikoroga na mambo yamerudi kama yalivyokuwa.

Rais wa Zanzibar, asingelalamika usawa katika muungano kama hakuna changamoto zinazouzonga muungano hadi sasa, bahati mbaya kachelewa mno kuzungumzia usawa katika muungano.

Mwanasheria kutoka Zanzibar, Awadh Ali Said, anapozungumzia matatizo ya Muungano katika muktadha wa mapato anasema; “suala la mapato linaanguka katika suala la uchumi huku uchumi likiwa si suala la muungano”.

Anaongeza kwamba; “kila mmoja (kati ya Tanganyika na Zanzibar)  ina uchumi wake na mzigo wa kushughulikia  (miundombinu, umeme, maji safi n.k) lakini nyenzo kuu za uchumi ambazo ni sera za fedha, sera za kodi, benki kuu, yote hayo yako upande mmoja (Tanzania Bara)”.

Kinachomshangaza Awadh ni kuwa, uchumi ni wako lakni huna udhibiti wa sarafu yako, huna udhibiti wa sera za kodi na huna uwezo hata wa kukopa lakini mwenzako muliyeungana amedhibiti yote hayo.

Hayo ndio maajabu ya muungano tulionao, hata uwe Mwanza au Bukoba huwezi kukataa changamoto hizi, ndio maana nikasema ni muungano wa ajabu hata ukiuweka kitako au kuulaza bado hauweleweki.

Ni muungano wa shaghalabaghala, sio lazima umalize shahada ya siasa ili kuelewa, muungano wa nchi mbili lakini nchi moja ndio imehodhi kila kitu na nyengine imepewa mamlaka ya ndani tu.

Na tatizo la viongozi wetu wa pande zote, mara nyingi wanaposimama majukwaani hawakazii katika kutatua changamoto za Muungano lakini hukazia kuulinda tu muungano.

Katika maadhimisho ya miaka 53 ya muungano wa nchi hizi mbili, yaliyofanyika Dodoma, rais Magufuli alisema; “Nataka niwahakikishie kuwa, tutaulinda Muungano kwa nguvu  zote , na kamwe asijitokeze mtu yeyote atakaye jitahidi au kujarbu kuuvunja muungano, atavunjika yeye”.

Kwanini viongozi wetu wasile viapo vya kuondoa kero za muungano, kuliko kula viapo kulinda muungano ambao dhahiri-shahiri una mapungufu tele ndani yake, ni kana kwamba unalazimisha kitu kibovu kiendelee tu kubakia lakini kukirekebisha hutaki.

Viongozi wasiokuwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanapozungumzia kero za Muungano huonekana hawana nia njema na muungano, hadi wapo viongozi wa kidini Zanzibar waliolia na huu mungano, wakaishia kupachikwa kesi ya za ajabu ambazo imeshindikana kuwapata na hatia wa miaka mitano  sasa.

Mwezi Mey mwaka juzi, Mbunge wa CCM wa Jimbo la Kijito Upele, Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha alilalamika Bungeni akisema;

“Tumezungumza kwa muda mrefu suala la kugawana mapato kati ya serekali ya mapinduzi Zanzibar na ya Muungano.. naonba suala hili lifike mwisho limalizwe”.

Aliyazungumza haya kwa sababu  kulikuwa na tatizo, hata yale mapato ambayo paliwekwa  makubaliano kuwepo na mgawanya fulani kwa pande zote, bado Zanzibar ilikuwa haipati.

Huyu ni mbunge wa CCM ambaye amewahi kuwa waziri katika serekali ya Muungano.Kama angekuwa ni mbunge wa chama chengine tungesima analeta  upinzani lakini ni wa CCM,  ambayo ndiyo imeshika mpini pande zote.

Ili kuwa na Muungano wenye afya, hatuwezi kuzikataa changamoto zake kwamba zipo, na Dk. Shein kachelewa sana kujitutumua kuzungumzia usawa wa muungano, wakati mambo yameharibika muda mrefu sana.

Kinachoumiza ni kwamba rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli anaonekana hana hata ile nia ya kuweka mambo sawa katika muungano, anachokazia yeye ni kuulinda tu.

Siku Dk. Harrison Mwakyembe, wakati akiwa  Waziri wa Katiba na Sheria, alipoutambulisha umma kuwa mchakato wa upatikanaji wa  Katiba mpya haikuwa kipau mbele kwa rais Magufuli, kilikuwa ni kielelezo cha wazi kwamba utatuzi wa hizi kero umeshatiwa kapuni mazima.

Ili kuufanya muungano kuwa na afya na ubaki imara kwa pande zote, la muhimu ni kuutoharisha ili usiwe na harufu ya dhulma kwa upande mmoja, kuliko kutishana kuulinda tu.

Ukimuuliza mwanandoa yeyote, lipi bora kati ya kulinda kwa nguvu zote ndoa yenye matatizo au kutumia nguvu zote kuondoa matatizo. Ni wazi kila mwenye akili atatumia nguvu kufuta matatizo yaliyo kwenye ndoa.

Janury 4, mwaka huu Dk Shein alipozungumzia usawa katika Muungano,   katika ufunguzi wa  jengo la Takwimu mjini Zanzibar, pia alisema; “si busara kwa mambo ya muungano kufanywa upande mmoja tu au upande mmoja kuonekana unajivutia wenyewe kila kitu, hali hiyo inaweza kuleta madhara makubwa katika utendaji wa masuala ya muungano.”

Haya maneno hayapaswi kuchukuliwa kwa wepsi, ni ishara kwamba bado kuna shida katika muungano wetu, nguvu za kuondoa haya matatizo ya muungano ndizo zinazohitajika.

Ingawa kwa sababu ya kulinda matumbo yao, viongozi wengi wa SMZ huchelewa kuzungumzia jambo hili, lakini bado kuna nafasi ya kuhakikisha mambo yanawekwa sawa, ikiwa kweli tuna nia njema na muungano.