Home Habari LISSU ATWISHWA MZIGO CHADEMA

LISSU ATWISHWA MZIGO CHADEMA

622
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


MISIMAMO ya kisiasa ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) dhidi ya Serikali hata baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana, inamfanya kuonekana kuwa mwanasiasa wa kweli wa upinzani anayeweza kupeperusha bendera ya urais wa chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu ujao. RAI linachambua.

Kauli na maandiko ya baadhi ya makada na viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, zinadhihirisha wazi kuwa kwa sasa ni Lissu pekee, mwenye uwezo wa kuhimili vishindo vya siasa za sasa nchini.

Pamoja na Lissu kuwa hospitali kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, ukweli unasalia kuwa amekuwa mhimili mkubwa wa siasa za upinzani hasa kwa Chadema kutokana na tukio lake kubeba huruma ya wananchi wengi, lakini pia kauli zake mara baada ya kuanza kuongea na kuonekana kuipinga Serikali zaidi.

Mwanasiasa huyo alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka jana, ambapo alikimbizwa nchini Kenya kwa matibabu na hivi karibuni alipelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Lissu (50) anatafasiriwa kama mwanasiasa wa upinzani asiye na uoga na mwenye utayari wa kujitoa kwa ajili ya kupigania haki.

Tukio la kushambuliwa kwake linatazamwa na wachambuzi wa kisiasa kama tukio lililomuongezea wigo mpana wa umaarufu ndani na nje ya nchi hali iliyomuongezea sifa na  kustahili kupeperusha bendera ya upinzani kwenye mbio za urais.

Aidha, ukosoaji wake  ambao umemweka matatani na kufunguliwa kesi nane za uchochezi, unadaiwa  kumweka katika nafasi nzuri ya kuwa mwanasiasa pekee  wa upinzani anayeweza kusema bila hofu.

Tayari baadhi ya makada wa Chadema kupitia kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii wameshaanza kuibua hoja ya kumtwisha mzigo wa Urais Lissu.

Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala  mapema wiki iliyopita kwenye ukurasa wake wa instagramu aliweka picha aliyopiga na Lissu  alipokuwa hospitalini mjini Nairobi na kuandika kuwa ‘My President in 2020”, akiwa na maana ya  Rais wangu 2020.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wafuasi wake katika mtandao na siku chache baadaye kada mwingine wa Chadema ambaye pia ni Meya wa Ubungo, Boniface Jacob aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa ‘Nitaumia tu siku nitakayoambiwa Tundu Lissu anahamia CCM, hizi takataka zingine bebeni zote’.

Jacob alikuwa akijibu hoja ya Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole aliyetoa taarifa ya kusubiri kumpokea kigogo mkubwa kutoka ndani ya chama hicho.

Pamoja na mambo mengine baadhi ya wachambuzi na wanasiasa waliozungumza na RAI hawakusita kuunga mkono hoja ya Lissu kukabidhiwa mikoba ya urais ifikapo mwaka 2020 kwa kuwa wanaamini kuwa afya ya Mnadhimu huyo mkuu wa Kambi ya upinzani bungeni, itakuwa imeimarika.

Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye juzi aliliambia RAI kuwa haoni sababu ya Lissu kutopewa nafasi iwapo wanachama watampitisha na kupewa baraka.

“Habari ya urais ni nyingine, ila habari ya kujenga nguvu ya upinzani ni kweli Lissu amesaidia sana, sasa wakati utakapofika, chama kina utaratibu wake, kama chama kitaona kwamba ndiye atakayeonekana, basi atabeba bendera na hakika chama kitafanya hivyo na kitampa yeyote ambaye ataonekana anaweza kukivusha chama kwa sababu lengo ni hilo.

“Kwa sasa Tundu Lissu ni mmoja wa wanachama wanaofanya vizuri kwa hiyo sioni sababu ya kutopewa nafasi iwapo mwenyewe atapenda kugombea na kwa utaratibu uliowekwa wanachama wakaona anafaa… sioni kwanini asiwe,” alisema Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Aidha, hoja ya Sumaye iliungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCCU), Profesa Gaudence Mpangala ambaye alisema Lissu anastahili kwa kuwa tayari amejipatia umaarufu ndani ya nchi na duniani kwa ujumla.

“Suala la urais ni taratibu za chama lakini ni ukweli usiopingika kuwa Lissu amejijenga vema ndani na nje ya nchi, hata hili tukio la kujeruhiwa nalo limemuongezea umaarufu sana. Kwa hiyo chama kama kitaona anafaa ni jambo jema, kwa kuwa sasa anatambulika kitaifa na kimataifa kutokana na ukosoaji wake.

“Amekuwa mmoja wa wanasiasa wa upinzani ambao wanakosoa kwa hoja na ukweli bila kuogopa jambo ambalo limekuwa nadra kwa wapinzani wengi kufanya hivyo. Kwa maana hiyo kutokana na umaarufu aliojizolea na ujana alionao sioni sababu inayoweza kumkwamisha kupeperusha bendera ya upinzani,” alisema Mpangala.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu naye aliunga mkono suala hilo na kuweka wazi kuwa Lissu yupo kwenye nafasi nzuri ya kuwa mgombea urais.

“Tunamwombea Lissu afya yake iweze kuimarika na kama alivyosema kwamba atasimama na atatembea na ataendeleza mapambano Tanzania, hivyo kama akijaliwa kugombea sina mashaka naye.

“Bila shaka yeye ni kiongozi wa juu katika chama na kama mwanachama anaweza kugombea nafasi yoyote ikiwamo urais, muda ukifika wa kumtafuta nani anaweza kuwa kiongozi bora na kuteka nyoyo za Watanzania ili kuweza kuvuta kura na kukidhi matakwa ya wananchi akigombea nadhani yuko katika nafasi nzuri.

“Kutokana na madhara haya yaliyompata na watu wengine wameshaanza kusema kwamba Mungu ana mpango naye wakiwa wanafikiria aje kuwa Rais, hamu yangu ni kuona Lissu anapona,” alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji alisema kwa kuwa watu huwa na matarajio yao kwa Rais kulingana na matatizo yaliyopo, leo Lissu anaweza kuonekana anafaa lakini baada ya muda akaonekana hafai kwa sababu urais ni kazi ngumu.

“Kitu cha kwanza ni yeye mwenyewe kujiona kama anaweza halafu na sisi watu wa pembeni ambao tunafikiri kuwa anaweza, hapo ndipo tunamwambia kuwa anaweza mwishowe wananchi wamuweke katika nafasi hiyo. Ukishakuwa Rais hakuna mtu wa kusema kuwa huwezi kwa sababu nchi ina Rais mmoja,” alisema.

Kutokana na umaarufu wa Lissu hata Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru ambaye amelazwa katika hospitali ya Muhimbili baada ya kung’atwa na mbwa ameonekana kumkumbuka Lissu na kusisitiza mapambano yanaendelea.

Kigunge alimkumbuka Lissu baada ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe  akiwa amefuatana na Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa kamati Kuu, Edward Lowassa walipomtembelea juzi katika hospitali ya Muhimbili.

“Vipi kuhusu Tundu Lissu? Nimeona mimi jinsi wanavyonifanyia hapa (madaktari) nimewauliza mimi tu niliyeng’atwa na mbwa mnanifanyia hivi Lissu mmemfanyaje maana majeraha yake yalikuwa makubwa” alihoji Kingunge

Hata hivyo, baada ya Mwenyekiti wa Chadema kumueleza Mzee Kingunge juu ya hali ya Lissu kwa sasa ilimpa faraja mzee huyo na kusema kuwa ‘Aluta Continua’.