Home Habari LOWASSA AIBUA UTATA

LOWASSA AIBUA UTATA

845
0
SHARE

NA JOHANES RESPICHIUS


 HATUA ya Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli pamoja na kumwagia sifa kimeibua utata ndani na nje ya chama chake. RAI linaripoti.

Lowassa alikutana na Rais juzi Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo alimpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya hasa ya kutoa elimu bure,   mradi mpya wa uzalishaji wa umeme kutoka maporomoko ya mto Rufiji (Stigler’s Gorge), ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge).

Lowassa alisema vitu vyote hivyo ni vilivyofanywa na Rais ni vizuri na vinazalisha ajira kwa vijana.

“Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Rais, tumezungumza  nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo.

“Jambo la msingi sana amejenga ajira kwa kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stigler’s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine elimu ni muhimu sana hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili lazima lisemwe vya kutosha kwa kweli nakushukuru Rais…” alisema Lowassa.

Kwa upande wake Rais Magufuli alimpongeza Lowassa kwa kutambua kazi inayofanywa na Serikali huku akisema kuwa  Lowassa ni mmoja wa viongozi ambao kwa wakati wao walitoa mchango mkubwa kwa nchi.

Mbali na hilo Dk. Magufuli alisema Lowassa ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha Urais kupitia Chadema hakuwahi kumtukana.

“Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza, kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.

“Ametaja miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stigler’s Gorge utakaogharimu zaidi ya Sh. trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu bure, amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za hospitali na mengine” alisema Dk Magufuli.

Kauli ya Lowassa dhidi ya Rais na ya Rais dhidi ya Lowassa inaonekana kuibua utata, kutokana na baadhi ya makada wa Chadema kumuona msaliti huku wengine wakimpongeza.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Profesa Mwesigwa Baregu, alisema hajui lengo la Lowassa na kwamba kuna mambo hakumwelewa vizuri kwa sababu Chadema inaamini katika demokrasia ya kweli.

“Ni mapema sana kujua alikuwa na lengo gani kwenda kule, lakini kwa yale aliyoyasema mengine sijamwelewa vizuri kwa sababu tukisema Chama cha Demkokrasia tunamaanisha demokrasia ya kweli.

“Pia tunaamini ili maendeleo yaje lazima demokrasia iwepo kwahiyo sielewi Lowassa kama aliyoyasema ndiyo waliyoyazungumza akiwa ndani au labda kuna mengine zaidi, maana Rais alisema kwamba wamezungumza mengi kila mmoja alisema ya kwake, sasa hayo mengine ndiyo hatujayajua kama alikuwa anasema kwa kuwa maendeleo yamekuja lazima demokrasia ikandamizwe.

“Mpaka sasa watu wengi watakuwa katika hali ya sintofahamu kwahiyo ni vizuri yeye mwenyewe akatoka hadharani akawaambia watanzania ambao walimpigia kura alipogombea urais mwaka 2015 akafafanua hayo matembezi yake yalikuwa na lengo gani, je, wameyafikia au la na tutegemee nini,” alisema Profesa Baregu.

Alisema kama lengo lake ni kutaka kurudi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) anaweza kurudi tu kwani hakuna kitu kilichomzuia maana yeye ni mtu mkubwa na ana watu wengi wanaomuamini si lazima aende kwa kinyemelea, angetoka moja kwa moja kama anahama Chadema ajitangaze kama wengine wanavyofanya.

Kwa upande wake Profesa Gaudence Mpangala, alisema haijulikani Lowassa amekwenda kuongea nini na Rais.

“Hatujui nini amekwenda kuzungumza na rais,  labda ni mambo yake binafsi au ni dhamira ya kurudi CCM.

“Ila kama ni mazungumzo ya kurudi CCM atakuwa amejidharau sana kwa kuwa ametoka CCM akapewa nafasi kubwa ya kupeperusha bendera ya upinzani na sasa kama akirudi huko atakuwa amejishushia heshima mwenyewe.

“Anatakiwa kuweka wazi aliyozungumza ingawa hayo aliyosema kuwa kumpongeza rais kwa utendaji wake si afya kwa upinzani hasa ukizingatia kuwa wapinzani wamekuwa wakilalamikia mambo mengi dhidi ya serikali iliyopo madarakani.

Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kwa upande wake alisema anapaswa kujiridhisha kabla ya kusema lolote juu ya uamuzi na kauli za Lowassa.

“Kabla ya kutoa maoni nataka nijiridhishe na mambo fulani kwanza kwa sababu taarifa ya tukio hilo sijaitathmini vizuri.”

CHAMA HAKINA TAARIFA

Wakati kukiibuka utata huo, kauli ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe , imedhihirisha wazi kuwa chama hakikuwa na taarifa ya ziara hiyo ya Lowassa kwa Rais.

Dk. Mashinji alisema  hakuwa anafahamu kitu chochote juu ya ziara hiyo kwani yeye juzi alikuwa safarini akitokea mkoani Mbeya.

“Niko safarini kwahiyo hata sijui lolote, lakini pia ofisi yangu haikuwa na taarifa yoyote, hivyo niseme tu sijui lengo lilikuwa nini na walikuwa wanazungumza nini labda anaweza akawa amewasiliana na viongozi waliopo ofisini kwasababu mimi sikuwepo,” alisema Dk Mashinji.

Kwa upande wake Mbowe, alisema kauli iliyotolewa na Lowassa katika ziara yake ya Ikulu juzi kama kweli ndicho walichozungumza sio msimamo wa chama kwani wao hufanya maamuzi kupitia vikao na kutoa maazimio ya pamoja baada ya kujadiliana kwa upana.

“Katika siku za karibuni tumekuwa na malalamiko mengi dhidi ya Rais na Serikali yake hasa namna anavyominya demokrasia, anavyominya uhuru wa Bunge na Mahakama, namna zoezi haramu la kujaribu kuwarubuni viongozi ili kuua upinzani unavyofanyika, uchumi unadidimia na kadhalika.

“Tunashindwa kujua anapata wapi ujasiri wowote ule wa kuweza kuisifu serikali ya awamu ya tano, kwahiyo huo si msimamo wetu na kama kuna maelezo yoyote mengine muhusika anaweza akaieleza dunia.

“Amezungumzia kuongezeka kwa ajira licha ya kutotoa idadi ya hizo zilizoongezeka japo imelinganishwa na ujenzi wa reli ya kati zinaweza kuongezeka, kuna tatizo kubwa la ajira na kuna ongezeko kubwa la vijana hawana ajira, lakini kuna kampuni, biashara na benki zinafungwa kwahiyo ajira zinapungua.

“Nisikitike kwamba sisi tuna kilio kikubwa, tunaendelea kumtibu Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi, unashindwa kuelea inakuwa kiongozi katika chama anatoka na kumsifia Magufuli wakati tunauguza, msaidizi wangu Ben Saanane amepotea, viongozi wetu wameuawa na wengine wamefungwa na wabunge wanafukuzwa bungeni kwa makosa ya kubambikiziwa,” alisema Mbowe.

Akizungumzia kuhusu baadhi ya viongozi kukihama chama hicho, alisema kuwa suala la wanasiasa kuhama sio jambo geni hapa nchini kwamba kazi ya kujenga upinzani sio tukio la siku moja bali ni mchakato wa muda mrefu hivyo lazima lipitie vipindi mbalimbali ili kufanya mchujo na watu wachache wenye dhamira ya dhati kusonga mbele.

Hata hivyo baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za nchi hii wanaupongeza uamuzi huo wa Lowassa kwa kudai kuwa unafungua ukurasa mpya wa siasa za upinzani nchini.

MARA YA PILI

Hii ni mara ya pili kwa Lowassa kukutana na Rais Magufuli tangu aingie madarakani, mara ya kwanza ilikuwa ni Septemba 1, 2016 jijini Dar es Salaam, kwenye misa maalum ya miaka 50 ya ndoa ya Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Katika makutano hayo ambayo yalikuwa ni ya kwanza kwa Rais kukutana ana kwa ana na Lowassa, Dk. Magufuli alisema kuwa kwake ni muujiza kwani hajwahi kupeana mkono na Waziri Mkuu huyo wa zamani kabla na hata baada ya kampeni za urais mwaka 2015.

“Na mimi nikiri leo katika siku hii wakati tukiadhimisha miaka 50 ya ndoa yenu na mimi nimepata muujiza ya tofauti kwa sababu leo ndio nimeshikana mkono na Lowassa.

“Tumezunguka kampeni zote, sikuwahi kukutana nae kwa hiyo harusi ya leo ni muhimu sana, muujiza wa ndoa yenu ya kufikisha miaka 50 imekuwa muujiza kwetu pia wanasiasa, ambao nikiri tulikuwa na ushindani mkubwa,”alisema Rais Magufuli.