Home Makala WANANCHI WA TARAFA YA RUHUHU WAMEACHWA UKIWA

WANANCHI WA TARAFA YA RUHUHU WAMEACHWA UKIWA

102
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA


RUHUHU ni miongoni mwa Tarafa zinazounda Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa. Wilaya hii ni miongoni mwa zingine kama Songea Vijijini, Songea Mjini, Mbinga, Namtumbo, Tunduru zilizopo mkoani Ruvuma. Wilaya ya Nyasa ilianzishwa rasmi mnamo Machi 2012 baada ya kugawanywa wilaya ya Mbinga. Eneo la wilaya ya Nyasa liko kando la Ziwa Nyasa.

Tarafa ya Ruhuhu ipo kwenye mwambao huo, ikiwa ni miongoni mwa maeneo yaliyoachwa nyuma kimaendeleo na kiuchumi. Tarafa hiyo inazo Kata za; Mbaha, Lituhi, Ngumbo na Liwundi.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka wa 2012, Kata ya Mbaha ilikuwa na wakazi wapatao 6,972. Ni Kata ambayo ndiyo mwenyeji wa Shule ya Sekondari ya Monica Mbega iliyoanzishwa rasmi mwaka 2006. Jina la shule hiyo lilitokana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Monica Mbega kabla ya kuondoka.

Wananchi wa Tarafa hii wanakabiliwa na changamoto nyingi mno hali ambayo inadhoofisha ukuaji wa uchumi. Changamoto hizo zinatokea katika nyakati tofauti na kuziba mianya ya kujipatia pato kutokana na huduma kadhaa wa kadhaa kuwa dhaifu.

SEKTA ELIMU HOI

Kwa mujibu wa Ripoti ya Shule ya Sekondari ya Kata ya Monica Mbega kwa wazazi na walezi ya Julai 2017 ilisema jumla ya wanafunzi 41 wa kidato cha cha kwanza walikuwa hawajasoma masomo manne ya Biology, Physics, Book Keeping na Commerce. Nilipowauliza baadhi ya wanafunzi kuhusiana na suala hilo walidai kuwa kutosoma kwao masomo hayo ni kutokana na shule hiyo kutokuwa na Walimu wa masomo husika.

Ndiyo kusema wanafunzi 41 waliongia kidato cha pili mwaka 2018 katika sekondari hiyo hawafahamu lolote kuhusiana na masomo hayo yaliyotajwa, hali ambayo inawadhoofisha ukuaji wao wa kitaaluma. Kwamba tunapoteza wataalamu na kuwafunza watoto wetu elimu duni.

Aidha, kabla ya serikali kusitisha kuajiri tatizo lilikuwepo. Mwaka 2017 Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitangaza ajira za walimu wa shule za msingi kwa walimu ambao wamemaliza masomo yao mwaka 2014/2015 katika ngazi ya cheti (III A). Kwamba hapa serikali ilitoa ajira za walimu.

Aidha, mwaka huo huo Ofisi ya rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilitoa orodha ya walimu wa Shahada na Stashahada waliopangiwa vituo vya kazi katika shule za Sekondari mbalimbali nchini. Lakini hakukuwepo na Mwalimu aliyekabidhiwa jukumu la kufundisha wanafunzi wa Sekondari ya Monica Mbega katika masomo tajwa hapo juu. Natambua serikali inaweza kujitetea kuwa hiyo ni awamu ya kwanza, lakini je kuanzia mwaka 2006 hadi hivi leo haikufahamu matatizo ya shule zake za Kata ikiwemo Monica Mbega? Mazingira ya aina hii hayatodautiana na hali ya shule za zingine zilizopo Kata ya Ngumbo na Liwundi ndani ya Tarafa hiyo.

TAABU YA MAWASILIANO, MIUNDOMBINU NA UCHUKUZI

Hili ni eneo ambalo linaleta simanzi zaidi. Kampuni za Simu nchini hazijafanya jitihada za kutosha kuwapata wateja wapya katika Tarafa hii pamoja na kutimiza sheria na matakwa ya serikali kufikisha huduma za mawasiliano vijijini.

Nakiri kuwa kampuni hufuata faida, lakini kwa tofauti iliyopo kati ya miaka 1990 na sasa ni dhahiri kiwango cha wananchi kutumia simu za mkononi kimeongezeka. Tatizo linakuja mawasiliano ni hafifu mno.

Upande wa barabara nimewashuhudia ukarabati ambao ninaweza kusema ni sawa na kumpa mgonjwa vidonge vya kutuliza maumivu (Panadol) badala ya Mseto (tiba). Ukarabati unaofanywa ni kwa maeneo korofi lakini hali halisi ya barabara si nzuri. Ninakumbuka alipokuwa waziri wa Ujenzi,  Dkt. John Magufuli, alisema kuwa Serikali itajenga barabara kwa kiwango cha lami kuunganisha Wilaya ya Mbinga hadi Wilaya ya Nyasa itakayokuwa na urefu wa Kilometa 67.

Dkt. Magufuli aliyasema hayo alipokuwa anahutubia mamia ya Wakazi wa Nyasa kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa miguu Mbamba bay, mara baada ya Rais Jakaya Kiwete kufungua Madaraja pacha ya Ruhekei A, B na C yaliyogharimu kiasi cha Tsh. bil.4.

“Mhe. Rais napenda kutamka hapa kuwa kama tumeweza kujenga mtandao wa barabara za lami zaidi ya km. 11,000 nchi nzima hatuwezi kushindwa kujenga km. 67 kwa kiwango cha lami. Dkt. Magufuli aliongeza kuwa tayari Wizara ya Ujenzi ilitenga fedha kiasi cha Shilingi Bil. 2.3 katika mwaka wa fedha 2014/15 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo katika kiwango cha lami,”

Aidha, Novemba 29, 2017 pia nimepokea taarifa ya Kikao cha Bodi ya Barabara mkoani Ruvuma ambacho kilitangaza mkandarasi kampuni ya Chicco kupewa zabuni ya ujenzi wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay. Lakini hakuna maelezo yoyote juu ya barabara za Mbamba-Lituhi wala Lituhi-Kitai hadi sasa hali ambayo inazidi kuwaweka gizani wananchi wa tarafa ya Ruhuhu. Halimashauri nayo haina jawabu. Inatuliza maumivu badala ya kutibu.

Miradi mingi inaelekezwa kwenye Tarafa ya Ruhekei huku wananchi wa Ruhuhu wakibaki wakitaabika. Barabara ya Lituhi kwenda Songea ni miongoni mwa barabara kuu tatu za Jimbo la Nyasa, lakini kinachoendelea huko ni ukarabati, kurundikwa vifusi na wananchi kubugia vumbi. Barabara ya Lituhi kwenda Mbamba Bay inatakiwa kufanya mapinduzi makubwa kuliko “kutumia mbinu ya Panadol”. Daraja kubwa na refu lililopo kijiji cha Liweta likisombwa na maji maana yake mawasiliano hayatakuwepo hivyo kuleta madhara kwa wananchi.

Kwa wananchi wa Ruhuhu mawasiliano ni tabu. Barabara ni tabu. Bandari zilizopo ni tatu; Lundu, Mkili na Ndumbi. Lakini Ndumbi imechaguliwa kujengwa bandari kubwa kwasababu ya jiografia yake karibu na mji wa Lituhi ambao utaunganisha na Manispaa ya Songea. Je kwa mazingira ya barabara hiyo mizigo kutokana bandari itapita wapi? Kwanini wananchi hawa wameachwa ukiwa?

HITIMISHO

Katika mazungumzo yangu yasiyo rasmi na diwani Kata fulani jimbo la Nyasa ambaye yupo karibu na Mbunge wa Jimbo hilo na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, aliniambia,

“Ni kweli kuna nakisi Tarafa ya Ruhuhu haipewi kipaumbele kama ilivyo tarafa ya Ruhekei. Hoja yako ya Tarafa ya Ruhuhu ni sahihi kabisa haina chembe ya uwongo, kutokana na kutokuwa na mradi mkubwa wa kijamii ukiondoa Bandari ya Ndumbi na Lile daraja la Ruhuhu, lakini naona Mbunge anawaza kitu upande huu wa Ruhuhu. Tuendelee kushirikiana.,”

Je tuendelee “kuenenda” kwa imani huku muda unayoyoma na wananchi hawana pa kushikilia?