Home Habari JUMUIYA YA WAZAZI CCM YABEBA DHAMANA

JUMUIYA YA WAZAZI CCM YABEBA DHAMANA

455
0
SHARE

Na Susan Uhinga, Tanga.

“ NI jukumu letu kama wazazi kuhakikisha vijana wetu wanafaidika na miradi mikubwa kama hii, halitakuwa jambo jema kama sisi tutakaa kimya na kuuacha mradi huu uwanufaishe wageni.”

Hiyo ni kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edmund Mndolwa.

Mndolwa alikuwa akizungumzia mradi mkubwa wa kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.

Katika mahojiano maalum na gazeti hili, Mndolwa ambaye amechaguliwa kushika wadhifa huo Desemba 12, mwaka jana, alisema mradi huo ni fursa adimu na muhimu kwa Watazania hasa vijana.

Akiwa wilayani Korogwe kwenye ziara maalum ya kujitambulisha na kuangalia uhai wa Jumuiya hiyo, Mndolwa alisema ni vema vijana wa mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla wakaamka na kuanza kuitendea haki fursa hiyo.

Alisema vijana wanatakiwa kujiandaa na miradi mikubwa inayotekelezwa na Seikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, ili waweze kunufaika na fursa zilizomo katika miradi hiyo.

Hata hivyo alibainisha kuwa kujiandaa kwao kuendane sambamba na uwezo wa kushindana na soko la Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na kusaka utaalamu.

Mndolwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CC), alisisitiza haja ya vijana kuhakikisha wanakuwa wa kwanza katika kuuhudumia mradi huo kwenye Nyanja zote, ili kuepusha kuwapa nafasi wageni kuwa wa kwanza.

Kiongozi huyo alisema ni wajibu wa viongozi wa chama hicho kuhamasisha vijana kujiandaa na fursa mbalimbali za miradi mikubwa inayotekelezwa na serkali kwa lengo la kuwasaidia wananchi waweze kupambana na umasikini wa kipato.

Alisema vijana wanatakiwa kuhakikisha wanapata elimu za uhakika zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu kwenye miradi yote mikubwa inayoendeshwa na Serikali.

“Tuko katika kampeni ya Tanzania ya viwanda, hili haliwezi kufanikiwa kama vijana wetu watakuwa hawana elimu na utaalamu wa kutosha juu ya suala hili la kuendesha viwanda.

“Kama vijana hawataziona fursa ziolizopo na zinazokuja na kuanza kuzitengenezea mazingira rafiki sasa, upo uwezekano wa vijana wengi kuja kuwa walalamikaji, kuliko watendaji,”alisema.

Alisema Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa elimu kwa vijana wa Kitanzania imeweza kuhakikisha elimu inatolewa bure katika ngazi ya msingi na sekondari lengo likiwa ni kuwaanda vijana waweze kupata elimu ambapo serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya shule.

Alisema kwamba vijana wanaoandaliwa vizuri kielimu wanaweza kumudu changamoto za ajira kwa kuwa wanaweza kuendana na uwepo wa fursa mbalimbali zilizopo katika miradi inayotekelezwa na serikali.

Mradi wa bomba la mafuta ni mkubwa hivyo vijana wanaweza kunufaika kwa kushiriki kazi za moja kwa moja lakini pia hata kufanya ujasiliamali katika maeneo ya miradi hiyo ambapo utaweza kuhudumia mambo mbalimbali ikiwemo suala la chakula na malazi.

Vijana wanatakiwa kujiandaa  hasa kielimu ili waweze kuendana na uwepo wa  fursa hizo kwani bila elimu wanaweza kujikuta wanakwama na kuishia kuchungulia na kubaki wanalalmikia fursa hizo kwenda nje.

Wazazi nao wanajukumu la kuhakikisha wanasimamia maendeleo ya elimu kwa vijana wao kwani jukumu la kujenga uchumi ulio bora ni la kila mtazania .