Home Habari LOWASSA HAKUSTAHILI KUBAKI CCM, HAKUTAKIWA KWENDA CHADEMA

LOWASSA HAKUSTAHILI KUBAKI CCM, HAKUTAKIWA KWENDA CHADEMA

788
0
SHARE

 

NA VICTOR MAKINDA

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyayi Lowassa, ni mwanasiasa nguli hapa nchini anayepita katika vipindi vigumu vya mtanziko wa kisiasa. Hakuna ubaya ambao hauna uzuri, hivyo ninaamini kuwa Lowassa anapita katika vipindi vibaya na pia vipindi vizuri katika safari yake ya kisiasa.

Kimtazamo Lowassa ni mwanasiasa anayeipenda siasa, amekulia ndani ya siasa, anazeekea kwenye siasa. Kama kuna mafanikio yoyote aliyoyapata iwe ni kisiasa au kiuchumi yana muunganiko na siasa.  Vile vile kama kuna anguko lolote alilolipata ni kwa sababau ya siasa.

Ukweli Ulivyo Lowassa anajua vyema namna ya kuzichanga karata za kisiasa isipokuwa karata zake hazichangiki na hazichangamani na karata za siasa zinazofanywa na vyama  vya siasa, kile alichokuwepo (CCM) na hiki alichopo (chadema).Je  Lowassa anakosea namna ya kuzichanga karata za kisiasa? Kwa nini anakosea? Au anapatia na kisha anakoseshwa na wenye husda na mafanikio yake kisiasa?

Lowassa ndani ya CCM

Kama nilivyokwisha tangulia kueleza  awali kuwa safari ya Lowassa kisiasa ni ndefu. Amekwisha wahi kupanda ngazi na kushuka katika vipindi na nyakati tofauti. Lakini Lowassa amesalia kuwani mwanasiasa asiyekata wala kukatishwa tamaa.

Itakumbukwa kuwa licha ya nafasi alizoshika serikalini katika wizara mbali mbali Lowassa alipanda ngazi hata kufikia hatua ya Uwaziri Mkuu. Cheo ambacho kwa mujibu wa katiba yetu ni cheo kikibwa cha tatu kutoka juu. Yaani cheo kilichokuwa juu yake ni Makamu wa Rais na Rais.

Kwa mwanasiasa yeyote awaye kupanda ngazi ndio tamanio kuu.Mwanasiasa kamwe hatamani kushuka ngazi. Fikra za mwanasiasa yoyote ni kushika hatamu za uongozi tena ni kwa nafasi za juu kabisa za uongozi.

Lowassa kama wanasiasa wengine hatoki nje ya tamanio hilo kuu. Tamanio la kushika hatamu za uongozi wa juu. Hii ndio sababu hata baada ya chama chake cha zamani CCM, kukata jina lake sambamba na majina mengine ya wana CCM waliowania nafasi ya kupeperusha bendera ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, Lowassa hakuridhishwa na maamuzi hayo.Aliamua kukihama chama chake kilichomkuza na kumlea kisiasa hata kumwamini na kufikia hatua ya kuwa Waziri Mkuu na kuhamia Chadema.

SAKATA LA RICHMOND NA ANGUKO LA LOWASSA

Siasa ni mchezo mchafu. Ndivyo wanavyosikia kusema wanasiasa walio wengi. Inasemwa hivyo kwa kuwa katika ulingo wa siasa  kuna ushindani mkubwa kuliko ulingo michezo. Siasa sio mchezo bali inafananishwa na mchezo kwa kuwa kuna ushindani ambapo kushindwa na kushinda ni matokeo tarajiwa kama ilivyo kwenye michezo. Ndani ya ulingo wa siasa kuna kila aina ya husda, ghirba, propaganda, uonevu, kupakana matope baina ya makundi hasimu na kijino pembe.

Lowassa alipambana sana kisiasa chamani CCM akikabili hayo yote, alikuwa kada mtiifu mwaminifu aliyeaminiwa chamani na serikalini. Mwaka 2005 baada ya uchaguzi mkuu uliomwingiza madarakani rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete, nyota ya Lowassa iling’ara mno. Ni baada ya Kikwete kumteua kuwa waziri mkuu wake. Lowassa aliitendea haki nafasi ya uwaziri mkuu. Alichapa kazi kufa na kupona kwa juhudi na maarifa. Sote tu mashahidi juu ya namna Lowassa alivyokuwa mtendaji na mfuatiliaji makini wa shughuli za serikali. Waliofanya kazi chini yake kamwe hawawezi kumsahamu kwani viti vyao vilikuwa havikaliki pindi Lowassa alipokuwa akifanya ziara katika maeneo yao ya kazi.

Utendaji wake ulimpa sifa lukuki ndani na  nje ya chama chake CCM. Hali hiyo ilipelekea husuda ndani ya chama chake CCM na serikalini. Wapinzania wake ndani ya chama  walionadalili kuwa kung’ara kwa nyota ya Lowassa kiutendaji kungeli mrahishia kupanda ngazi na hata kumuwia rahisi kumrithi Jakaya Kikwete. Huo ndio wakati walioutumia kufanya kila lililowezekana kuhakikisha kuwa Lowassa anashuka ngazi na sio kubaki au kupanda ngazi. Hapa palitumika proganda, hilana kila aina ya ghirba kumwangusha.

Sakata la zabuni ya kufua umeme wa dharua,Richmond ilitumika kama kete ya kumwangusha kutoka katika nafasi yake ya uwaziri mkuu.

Ninakumbuka, akihutubia bunge, siku aliyojiudhuru nafasi hiyo ya Uwaziri Mkuu, Lowassa alisema “Tatizo ni Uwaziri Mkuu wangu”. Kauli hii inadhihirisha kuwa katika serikali aliyokuwa akiiongoza alikuwa na maadui wengi waliopania kumwangusha kwa namna na mbinu yoyote ile. Maadui hao hawakuwa serikalini tu bali hata kwenye chama chake, Chama Cha Mapinduzi, CCM.

Baada ya sakata la Richmond,kundi na makundi hasimu dhidi yake waliendelea kufanya kila aina ya propaganda kuibadili taswira yake safi na kumwita majina yote mabaya kwa lengo la kuzidi kumchafua. Ufisadi kila ulipohubiriwa ulimtaja yeye kaka kielelezo na mtu anayetazamwa kuwa ni fisadi. Cha ajabu hakuna mwanachama iwe ni wa CCM au wa upinzani, aliyethubutu kumfungulia kesi katika mahakama yoyote kwa tuhuma za ufisadi. Sakata la Richmond liliwapa mwanya wapinzani wa Lowassa wa ndani na nje ya CCM kumshambulia kwa kila namna waliyoitaka.

UKIMYA WA LOWASSA

Kosa alilolifanya Lowassa ni kunyamazia kimya tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake. Kwa zaidi ya miaka nane tokea kipindi alichojiudhuru uwaziri mkuu mpaka kipindi anakihama chama CCM, Lowassa hakuwa amewahi kujibu tuhuma yoyote na hakuwa amewahi kutoa ufafanuzi wa kauli yake aliyotoa bungeni wakati anajiudhuru  ya kwa nini ‘‘Tatizo ni uwaziri mkuu wake’’?. Hapa alipaswa kueleza kwa nini tatizo ni uwaziri mkuu wake, nani na nani hawakutaka yeye awe waziri mkuu. Walifanya nini kuhakikisha kuwa anaipoteza nafasi hiyo ya uwaziri mkuu.

Kama nilivyosema awali Lowassa anajua kuzichanga karata za kisiasa ila karata zake hazichangamani. Nadhani Lowassa alidhani kuwa kunyamazia kimya tuhuma kutamuweka mahali sala zaidi. Kinyume chake kunyamaza kwake kuliwapa fursa maadui zake wa kisiasa chamani CCM, serikalini na hata vyama vya upinzani kumrushia kila aina ya kashfa kwa lengo la kuchafua taswira yake kisiasa.

Kwa hulka ya wa Tanzania ni watu wa kuamini kila kisemwacho pasipo kuhoji wala kutafakari. Sumu iliyoenezwa juu yake ilifanikiwa kuwaingia baadhi ya waTanzania kutia ndani viongozi wa CCM na hata upinzani wakaamini kilichosemwa na mahasimu wake.

Tunakumbuka mengi mabaya yaliyowahi kutamkwa na viongozi wa CCM na wa upinzani hususani wa Chadema juu ya Lowassa kipindiakiwa CCM. Itaendelea