Home Habari SERIKALI YASHIKILIA MSIMAMO STIEGLER’S

SERIKALI YASHIKILIA MSIMAMO STIEGLER’S

1333
0
SHARE

NA JOHANES RESSPICHIUS

NAIBU Waziri Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa msimamo wa Serikali juu ya kuendesha mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia  nguvu za maji katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji kwenye  eneo la Stiegler’s Gorge  lililopo  Rufiji mkoani Pwani, uko pale pale.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kuwapo kwa taarifa za Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuendelea kuutilia shaka mradi huo kwa madai kuwa unahatarisha maisha ya wanyama pori waliomo ndani ya hifadhi ya Selous ambayo ni urithi wa Dunia.

Unesco ambayo pia inaungwa mkono na baadhi ya mashirika ya kimataifa kama vile Shirika  la kimataifa la uhifadhi wa wanyama pori WWF, imekuwa na mashaka na mradi huo.

WWF lilipata kusema kuwa utafiti walioufanya umeonya kwamba njia inayotumiwa na wanyama pori wakati wanapohamia maeneo mengine itakatwa huku watu 200,000 wanaotegemea eneo hilo kwa kipato wakiathiriwa na mradi huo.

Akizungumzia suala hilo Mgalu alisema kuwa kwa upande wake hajayaona madai hayo ya Unesco na pia hajapewa maelekezo yoyote na  wakuu wake (Waziri/Rais), lakini alisisitiza kuwa msimamo wa Serikali haujabadilika na utekelezaji wa mradi huo unaendelea.

“Sijaona barua hiyo na sijapewa maelekezo yoyote kutoka kwa wakuu wangu hivyo nadhani msimamo uliotolewa tangu mwanzo ni ule ule kwasababu hakuna msimamo mwingine ambao umetolewa na serikali kuhusiana na mradi huo kama ingekuwa na mtazamo mwingine ingesema.

“Na hivi karibuni Wizara ilitangaza tenda.. mchakato unaendelea kwa sababu utolewaji wa tenda ulikuwa wa wazi, hakuna mabadiliko yoyote ambayo yametangazwa na serikali,” alisema Subira.

MRADI HAUNA ATHARI

Wizara ya Maliasili na utalii imekuwa ikiwataka  wadau wa uhifadhi kote nchini kuunga mkono mradi huo utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 2,100 za umeme kwani hauna athari zozote za kimazingira.

Wizara hiyo ilibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo wa umeme ni wa muhimu kwa taifa kwani utasaidia kuharakisha maendeleo ya taifa kuelekea azma yake ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.

Alipokuwa akifunga mafunzo ya askari wa wanyama pori kutoka mamlaka ya Wanyamapori Tanzania –TAWA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Meja Jenerali Gudance Milanzi aliwaambia kuwa  mradi huo wa umeme pamoja na mradi wa bwawa la maji la Kidunda utachukua eneo dogo tu la pori la akiba la Selou lenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 50, 000.
Alisema pori hilo ndilo kubwa miongoni mwa mapori ya aina hiyo ulimwenguni na ukubwa wake ni zaidi ya nchi za Rwanda na Burundi zikiunganishwa kwa pamoja.
Alisema ujenzi wa miradi hiyo hauna tafsiri kwamba Tanzania haithamini masuala ya uhifadhi bali unazingatia uhifadhi wenye manufaa kwa jamii na maendeleo ya taifa na hasa dhamira ya serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kuelekea Tanzania ya viwanda ambayo inahitaji nishati ya umeme itakayoyotosheleza mahitaji ya taifa.

MSISITIZO

Julai mwaka jana mbele ya wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia Tanzania iliiambia dunia kuwa iko tayari kuendelea na mpango huo  kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya Watanzania.

Akiwa katika mkutano wa 41 wa wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia ulioendeshwa na UNESCO, kwenye jiji la  la Krakov nchini Poland, aliyekuwa kiongozi wa msafara huo, Meja Jenerali Milanzi aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa mpango huo ulikuwepo katika ajenda ya Serikali ya Tanzania tangu miaka ya 1960’s na kwamba ukubwa wa eneo litakalotumika kutekeleza mradi huo ni asilimia tatu tu ya eneo lote la pori hilo.

Aliongeza kuwa, “Itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 1982 wakati pori hili (Selous) limewekwa katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhifadhi wa Asili (IUCN) liliutambua mradi huo wa Stiegler’s Gorge kutokuwa na madhara makubwa katika uharibifu wa mazingira ukizingatia ukubwa wa pori hilo na eneo litakalotumika kujenga mradi huo”.

Aliwaeleza wajumbe hao kuwa, Serikali ya Tanzania inatekeleza sera ya kujenga uchumi wa viwanda hali inayopelekea kuwa na mahitaji makubwa ya nishati ya umeme hivyo kwa kuzingatia vyanzo vilivyopo imekuwa ni muhimu sasa kufikiria tena ujenzi wa mradi huo kama chanzo kingine muhimu cha nishati kuwezesha kufikia azma hiyo.

Alisema mradi huo utaongeza uzalishaji wa umeme nchini kufikia asilimia 144.8 hivyo kuondoa upungufu wa nishati uliopo kwa sasa na pindi utakapokamilika utawanufaisha watanzania wengi wanaoishi bila umeme ikiwa ni pamoja na kukidhi mahitaji yake ya kuendesha viwanda.

Meja Jenerali Milanzi alilazimika kutoa maelezo hayo kwa kamati hiyo ili kuweka bayana dhamira ya dhati Serikali ya Tanzania ya kuendelea na ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya maendeleo endelevu huku akitoa rai kwao kuwa Serikali bado ipo tayari kwa mazungumzo ya namna bora ya kutekeleza mradi huo kwa faida ya jamii, uchumi na mustakbali bora wa mazingira ya hifadhi ya Selous na taifa kwa ujumla.

“Kwa kutumia teknolojia bora zilizopo, mipango imara na usimamizi thabiti, mradi huu utakua na faida kubwa kwa taifa ikiwa na pamoja na kuboresha maisha ya watu maskini na jamii kwa ujumla bila kuathiri mazingira yanayotoa faida hizo”, alisema Milanzi.

Hapo awali, kabla ya mkutano huo, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu huyo ulifanya mazungumzo na Maafisa Waandamizi wa Kituo cha Urithi wa Dunia na Bodi za Ushauri ya kituo hicho na kuwasilisha kwa maandishi msimamo wa Tanzania kuhusu ujenzi wa mradi huo.

Tanzania ilipinga vikali rasimu ya azimio No. 41 COM 7 A.17 aya ya 7 ambalo liliitaka kusitisha kabisa (to permanently abandon) ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Hydro Power Project).

Baada ya tamko la Tanzania kupinga azimio hilo kipengele hicho kilifanyiwa marekebisho ipasavyo na neno “to permanently abandon” (kusitisha kabisa) liliondolewa katika azimio hilo kupisha majadiliano zaidi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama zilizosaini mkataba wa urithi wa Dunia wa mwaka 1972 huku ikiwa na maeneo saba yaliyorodheshwa katika urithi huo ikiwepo Pori la Akiba la Selous, Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mji Mkongwe (Zanzibar), Hifadhi ya Ngorongoro na Michoro ya kondoa na Kilwa Kisiwani. Aidha, ni mwanachama wa Kamati ya Urithi wa Dunia kwa kipindi cha miaka minne hadi mwaka 2019.

Tokea ijiunge na kamati hiyo mwaka 2015, Tanzania imekua na msimamo wa kuwa na maendeleo endelevu katika ajenda za mikutano yake pamoja na miongozo yake ili kuruhusu kuendeleza maeneo ya urithi wa dunia kuweza kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi bila kuwepo kwa athari kubwa katika mazingira.

Mkutano huo wa 41 wa wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia ulihudhuriwa na nchi wanachama 193.

KAULI YA RAIS

Juni 21, mwaka jana Rais Magufuli akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani, mbele ya wananchi waliohgudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Bwawani mjini Kibaha, alisema Serikali yake imejipanga kuhakikisha inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Rais aliitaja miradi hiyo kuwa ni  ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo imeanza kujengwa, ujenzi wa barabara ya njia sita kati ya Dar es Salaam na Chalinze yenye urefu wa Kilometa 128, ujenzi wa bandari kavu ya Ruvu itakayopokea mizigo ya kutoka bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao mipango ya utekelezaji kwa kushirikiana na Ethiopia imeanza.

Alibainisha kuwa pamoja na kutekeleza miradi hiyo Serikali ya awamu ya Tano itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaolihujumu Taifa ikiwemo kujihusisha na vitendo vya wizi na rushwa na haitakatishwa tamaa na watu wanaolalamika na kubeza juhudi hizo.

“Stiegler’s Gorge mradi ambao ulifanyiwa utafiti tangu enzi ya Mwalimu l. Julius Nyerere, tukautelekeza, nataka tujenge bwawa litakalozalisha umeme utakaotosheleza katika nchi yetu, nchi ya viwanda, ili Watanzania wasilalamikie tena suala la umeme, nataka tuachane na umeme wa matapeli wanaokuja hapa wanawekeza kwa lengo la kutuibia.

“Mimi nachukia wezi, na kwa kweli wezi watakoma tu, awe mwizi wa Tanzania, awe mwizi wa Ulaya, awe anatoka magharibi, mashariki, kaskazini au kusini, mwizi ni mwizi tu,” alisisitiza Rais Magufuli.