Home Habari ZUMA ‘ARUDI’ SERIKALINI KIVINGINE

ZUMA ‘ARUDI’ SERIKALINI KIVINGINE

710
0
SHARE

BALINANGWE MWAMBUNGU NA MITANDAO

JINA la aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma limerejea kivingine ndani ya Serikali ya Rais Cyril Ramaphosa.

Hivi karibuni Zuma alilazimika kujiuzulu nafasi ya urais baada ya Kamati Kuu ya chama chake cha ANC, kumtaka ajiuzulu kutokana na kukabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Hata hivyo, jina la Zuma limerejea tena Serikalini, safari hii likiwa chini ya mtalaka wake Nkosazana Dlamini.

Nkosazana Zuma ambaye ni mwanasiasa mwanamke machachari nchini Afrika Kusini, ameteuliwa kuwa Waziri Ofisi ya Rais.

Mwanamama huyo ambaye pia liwahi kuwa Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) atakuwa na jukumu la kushughulikia masuala ya utekelezaji nafasi iliyokuwa chini  ya Jeff Radebe.

Nkosazana ambaye alipata kuungwa mkono na mumewe wa zamani katika harakati zake za kisiasa aliwahi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Rais wa ANC na kushindwa na Ramaphosa.

Kitaaluma mwanamama huyo ni daktari wa tiba, aliwahi kuongoza Wizara ya Afya, Mambo ya nchi za Nje na Mambo ya Ndani, kabla ya kujiunga kuhudumu kama Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU.

Mbali ya Zuma, wateule wengine wa Rais Ramaphosa ni David Mabuza, ambaye anakuwa Makamu wa Rais. Mabuza ambaye ni mwalimu, alikuwa Waziri Mkuu wa Mpulanga Mashariki tangu mwaka 2009.

Mabuza ambaye anajulikana kama DD, alifanya kazi kubwa ya kuwashawishi wajumbe wa mkutano mkuu wa ANC ili wamchague Ramaphosa kuwa rais wa chama hicho mwezi Desemba mwaka jana.

Kuteuliwa kwake kushika nafasi hiyo kunamfanya DD kujiweka karibu na Urais kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

Nhlanhla Nene, ambaye alifukuzwa kazi na Rais Zuma mwaka 2014 na kusababisha mvutano mkubwa uliosababisha kushuka kwa idadi ya uwekezaji wa kigeni,  amerejeshwa katika nafasi ya Waziri wa Fedha.

Nene ambaye alikuwa Naibu Waziri wa fedha chini ya Pravin Gordhan mwaka 2014, anaheshimiwa na wawekezaji.

Aliacha kazi 2015 na nafasi yake ikachukuliwa na Des van Rooyen, mbunge ambaye hakuwa anafahamika sana, uteuzi wake ulisababisha kushuka kwa thamani ya Rand na amana za serikali.

Nene aliacha ubunge ili kushika nafasi ya Meneja wa Mfuko wa Bodi ya Allan Gray na kuwa mshauri wa Thebe Investment.

Kwa muda mfupi alishika nafasi ya Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Witwatersrand.

Anachukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Malusi Gigaba, ambaye amerejeshwa kwenye nafasi yake ya awali kama Waziri wa Mambo ya Ndani.

Nafasi ya Waziri wa mambo ya Nje imekwenda kwa mwanamke Lindiwe Sisulu, ambaye kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Nyumba.

Sisulu anachukua nafasi ya Maite Nkoana-Mashabane, ambaye amepewa Wizara ya Maendeleo na Ardhi, mwanamama huyo alikuwaa mgombea mwenza wa Ramaphosa katika kinyang’anyiro cha urais wa ANC mwaka jana, lakini akashindwa na David Mabuza.

Lindiwe ni binti ya Walter Sisulu, shujaa aliyefungwa pamoja na Nelson Mandela na utawala wa makaburu, alisomea uwalimu na kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Ulinzi, Wanajeshi Wastaafu, Usalama, Utumishi wa Umma na Utawala.

Wizara ya Mashirika ya Umma imekwenda kwa , Pravin Gordhan, ambaye atasimamia mashirika makubwa sita, likiwamo Shirika la Umeme la Eskom Holdings SOC Ltd, Shirika la Bandari na  Uchukuzi wa Reli—Transnet SOC Ltd.

Baadhi ya mashirika atakayoyasimaia Gordhan, yalikuwa yanahusishwa na kashfa ya familia ya Gupta ambayo inashirikiana kibiashara na watoto wa  kiume wa Zuma.

Gordhan, ambaye alisomea ufamasia, alikuwa Mkuu wa Mamlaka ya Kodi, kabla ya kushika wadhifa wa Waziri wa Fedha mwaka 2009 – 2014.

Alirudishwa katika Wizara hiyo 2015, baadae Rais Zuma alimwengua na kumteua Nhlanhla Nene  kushika nafasi hiyo hali iliyosababisha  sintofahamu katika soko la fedha, baadae hakuelewana na bosi wake,  akafukuzwa kazi na nafasi yake kuzibwa na Gigaba.

Hata hivyo Gordhan aliendelea na nafasi yake ya ubunge na alikuwa hasimu mkubwa wa Rais Zuma, sasa anachukua nafasi hiyo iliyokuwa chini ya Lynne Brown.

Gwede Mantashe ambaye kabla ya Desemba mwaka jana alikuwa Katibu Mkuu wa ANC anashika nafasi ya Waziri wa Madini. Mantashe alikuwa mfanyakazi katika migodi, alijiunga na Chama cha wafanyakazi Migodini na kushika nafasi ya Katibu Mkuu wake.

Ni mwanachama wa Chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini, ambacho ni mshirika wa ANC na alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho hadi  2012.

Ni rafiki wa karibu wa Ramaphosa na anachukua nafasi ya  Mosebenzi Zwane, Mwanasheria Jeff Radebe, ambaye amekuwa kwenye baraza la mawaziri kwa muda mrefu kuliko wote, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati.

Amezitumikia wizara tano tangu kuanguka kwa utawala wa Makaburu mwaka 1994. Wizara alizoziongoza ni Ujenzi, Mashirika ya Umma, Uchukuzi, Sheria na Waziri Ofisi ya Rais. Alikuwa mmoja wa wanachama wa ANC waliogombea nafasi ya juu ya chama hicho mwaka jana, lakini jina lake halikurudi. Anachukua nafasi ya David Mahlobo ambaye hakuteuliwa.

Askari Polisi Bheki Cele ambaye alifukuzwa kama Mkuu wa Polisi mwaka 2012 kwa ubadhirifu, alituhumiwa kukubali kukodi ofisi za kazi kwa bei ya zaidi ya mara tatu ya bei ya kawaida, anarudi wizarani hapo kama Waziri wa Polisi. Alikuwa mmoja wa watu waliofanyakazi kubwa kuhakikisha Ramaphosa ananyakua nafasi ya juu ya uongozi wa ANC, anachukua nafasi ya Fikile Mbalula, amabaye amehamishiwa makao Makuu ya ANC.