Home Habari MWENYE NJAA HANA STAHA

MWENYE NJAA HANA STAHA

1367
0
SHARE

NA VICTOR MAKINDA

NJAA mbaya. Adui yako mwombee njaa,akiwa na njaa huwa mpole, msikivu, mtii na mnyenyekevu.

Adui akiwa na njaa huenda akaomba msamaha bila kujali.

Njaa hupunguza     na kuondoka kabisa utashi, uwezo wa kufikiri na kuhoji unapotea.Mwenye njaa fikra zake huelekeza kufikiri namna anavyoweza kupata shibe tu, anaweza kufanya hata lililo batili ili apate shibe.

Ukitaka kupima uwezo wa ustahimilivu wa mwanadamu jaribu kwenye njaa. Kisa cha Esau na Jacob katika Biblia kinaeleza madhila ya njaa na namna gani mwenye njaa anaweza kuuza utu wake ili apate shibe.

Biblia inasimulia kuwa Esau alikuwa mwindaji, naye Yakob alikuwa akishiriki shughuli za jikoni na mama yake. Siku moja Esau alikwenda mawindoni, lakini hakupata kitoweo.

Alirudi nyumbani na njaa kali, alimkuta Yakob akiwa amepika dengu. Esau alimuomba Yakob ampatie bakuli la dengu ili atulize njaa yake.

Yakob alimwambia kaka yake Esau ikiwa anataka bakuli la dengu basi akubali kuwa mdogo kwake. Yaani Esau akubali kuwa Yakob ndie mzaliwa wa kwanza wa Isaka baba yao  na Esau awe ni mzaliwa wa pili.

Biblia inasema kwa kuwa Esau alikuwa na njaa sana, alikubali sharti hilo la kuwa mdogo kwa Yakob. Yakob alimpatia Esau bakuli la dengu naye Esau akamaliza njaa yake. Kisa hiki ni kirefu sana,lakini maelezo hayo mafupi yanatoa picha halisi ni namna gani mwenye njaa anaweza kukubali ushauri, sharti, au ushawishi wowote akilenga kupata shibe bila kujali ushauri au sharti hilo laweza kuwa na madhara makubwa kiasi gani kwake au kwa jamii inayomzunguka. Esau aliuza haki yake ya uzaliwa wa kwanza kwa sababu ya njaa.

Kuna kisa kingine, kinasimulia kuhusu Yesu na wanafunzi wake.    Yesu alikuwa akipita na wanafunzi wake pembezoni mwa mashamba ya ngano. Ilikuwa ni siku ya Sabato. Biblia inasema kuwa wanafunzi wa Yesu walikuwa wana njaa. Wakaanza kukwanyua masuke ya ngano toka shambani walimokuwa wakipita na kuyala. Mwenye shamba akamuuliza Yesu, mbona wanafunzi wako wanafanya mambo yasiyofaa siku ya Sabato?

Vipo visa vingi mno vinavyosimulia kuhusu njaa na namna watu walivyofanya ndivyo sivyo baada ya kukumbwa na njaa.

Ukweli ulivyo siku ya leo sina lengo la kunukuu vitabu vitakatifu kwa mintaarafu ya kuhubiri dini.  Lengo la kunukuu maelezo hayo kutoka kwenye Biblia ni kutaka kujenga hoja juu ya adha, madhila, umuhimu na athari za jamii kuwa na njaa.

Njaa imegwanyika katika makundi mengi. Kuna wenye ya kweli kwa maana ya njaa, njaa ya tumboni. Lakini pia kuna wenye njaa iliyohama kutoka tumboni na kuhamia kichwani baada ya matumbo yao kushiba. Hawa wameshiba lakini bado wana njaa ama twaweza sema tama.

Wenye njaa zilizohama kutoka tumboni na kwenda kichwani ni wale ambaowana uwezo wa kumudu kula, kuvaa na mahali pazuri pa kuishi. Hawa pia wana vyeo na nyazfa katika jamii zao lakini katu hawaachi kuwa wanyonyaji na kuwanyonya wengine hususani walio na njaa. Waliotawaliwa na tabia ya kujilimbikizia mali hata kama hawana kazi nazo na sio mahitaji muhimu. Ndio, Nani anaweza kusema kuwa na magari kumi ni mahitaji muhimu. Wapo wengi wana magari zaidi ya hayo tena ni ya kifahari. Tamaa.

Tunayo mifano mingi. Ufisadi, Rushwa na wizi wa mali za umma ni miongoni mwa hayo. Wapo watu tuliowapa madaraka, tuliowapa vyeo, tuliwapa dhamana ya kutuongoza lakini wanatunyonya. Hawa tunawapa nyumba, mishahara minono, wanatibiwa kwa kodi zetu lakini hawatimizi wajibu wao kwetu. Wangali wanatufisidi katika mali ambao zingeleta shibe kwetu.

Hawa hawajawa suluhu ya matatizo yetu. Hawafikirii na kubuni mbinu muafaka ya kuzimaliza njaa zetu. Wao mafikirio yao makubwa ni juu ya kujazia shibe zao. Kimsingi hawana njaa, wameshibabali wametawaliwa na njaa ya tamaa ya kudhurumu wahitaji.

Chukulia mfano, kiongozi wa umma, anayepata nyumba bure, gari bure, dereva bure, watumishi wa ndani bure, chakula na vinywaji bure na pia analipwa mshahara mnono, ana sababu gani za kuwa fisadi na kutotimiza wajibu wake?

NJAA HUHAMA

Viongozi wengi wa Kiafrika matumbo yao yameshibishwa na chakula kizuri na minofu. Wakiishashiba matumbo na kusaza njaa zao huhamia kichwani. Ukweli ulivyo njaa inayohama kutoka tumboni na kuhamia kichwani ni njaa hatari zaidi kuliko ile ya tumboni.

Migogoro mingi na migongano inayoleta machufuko mahali pengi barani Afrika na maeneo mengine ulimwenguni inatokana na njaa kuhama kutoka tumboni na kuja kichwani.

Njaa iliyo tumboni huisha mara tu mtu huyo anapopata chakula. Njaa iliyo kichwani hutawaliwa na tamaa na uchu wa kupindukia. Ndio sababu tunashuhudia mahali pengi duniani kwa sasa migogoro imekuwa haiishi kwa sababu tu ya njaa ya baadhi ya tuliowapa madaraka.Wanaendekeza njaa ilhali wameshiba huku wakiwasahau wenye njaa ya kweli.

Hawa licha ya kuwa wana uhakika wa maisha yao na vizazi vyao lakini hawaachi kutamani kuchukua kila kitu na kukifanya kuwa chao. Mfano rahisi ni kwa marais wafutao, Joseph Kabila wa DRC, Robert Mugabe wa Zimbabwe na Yoweri Museveni wa Uganda wapo wengine wengi.

Mugabe ameitawala Zimbabwe kwa miongo mingi mpaka hivi juzi alivyofurushwa kwa mbinu za kimedani. Vinginevyo angeendelea kuikalia nchi hiyo hadi mauti. Licha ya utajiri mkubwa aliokua nao bado Mugabe hakuwa ametosheka. Njaa ya madaraka ilikuwa inamtuma kuendelea kutawala nchi hiyo kama familia yake huku maisha ya wananchi yakiwa magumu huku huduma zote za kiutu zikizorota.

Tumeona nchini Uganda, Yoheri Museveni kaibadilisha katiba. Katiba ya nchi hiyo sasa inamruhuru kugombea na kutawa kwa kipindi kirefu zaidi. Museveni anatajwa kuwa rais tajiri Afrika, utajiri alionao haujamaliza njaa yake. Njaa yake imempelekea kuwa na tamaa na uchu wa madaraka wa kutawala muda wote wa uhai wake.

Vivyo ilivyo kwa Joseph Kabila wa DRC, amekuwa rais wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa tangu mwaka 2001.Utajiri ambao haujawanufaisha wananchi. Wananchi wa nchi hiyo wanakabiliwa na ugumu katika kila nyanja kuanzia miundombinu, hospitali, shule na hata uhakika wa chakulia. Kila ukaribiapo uchaguzi huusogeza mbele ili aendelee kutawala. Amekula ameshiba. Tumbo limejaa ila njaa imehamia kichwani. Anatamani aendelee kula pasipo kujali kundi kubwa la wahitaji wenye njaa matumboni mwao.

OLE WENU

Ole wenu enyi viongozi wa Afrika. Ole kwa vyama tawala Afrika ambavyo Serikali zenu hazitosheki. Ambao uongozi wenu umetawaliwa na njaa iliyohama kutoka tumboni na kuhamia kichwani. Ole wenu mnaotamani kutawala milele huku mkiwa hamjali maslahi na mahitaji ya tabaka la watawaliwa.   Ole wenu ambao mnadhani wenye njaa ya kweli wataendelea kuwa  wastahimilivu milele. Ukweli ulivyo ni kwamba mwenye njaa hupungua utashi. Kadiri mnavyoendekeza njaa/tamaa zenu huku mkiliacha kundi kubwa lenye njaa ya kweli likitabika na kuzidi kufukarika ndivyo siku zenu zinavyohesabika.

Nimetangulia kusema awali, mwenye njaa kwanza kinachopungua akilini mwake ni utashi. Hawa wenye njaa ya kweli, ambao kila uchao wanazidi kuwa mafukara, huku wakikosa tumaini la kesho, ipo siku wanaweza kufanya jambo litakalowashangaza.

Natoa wito kwa serikali    za  Kiafrika na mahali pengine duniani,     ni hatari sana kuzidi kumfukarisha fukara. Ni vema Serikali na viongozi wa Kiafrika, kuacha kuendekeza tamaa zao binafsi na kuanza kuwekeza nguvu nyingi kuwashibisha wananchi wenye njaa.  Hii itaepusha vishawishi vibaya kwa wananchi hao kwa kuwa wana njaa.

Kesho ya watawala inategemea staha  ya watawaliwa. Mtawaliwa akiwa na njaa na akashindwa kustahimili njaa yake, mtawala hana chake. Njaa mbaya. Mwenye njaa hana staha.