Home Makala HAKIELIMU: Vyuo vikuu vimekuwa shamba la bibi

HAKIELIMU: Vyuo vikuu vimekuwa shamba la bibi

2415
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

KATIKA siku za karibuni kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusu suala la elimu ya vyuo vikuu inayotolewa nchini. Hali hiyo imesababishwa na uamuzi wa Serikali kutoa sifa na vigezo vipya vya kudahiliwa na kupewa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao umekuwa ukipigiwa kelele kila kona na baadhi ya wasomi.

Hivi karibuni wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kutoa mwongozo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini ambapo pamoja na mambo mengine iliagiza vigezo hivyo kuzingatia vipaumbele vya kitaifa vinayoendana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Hata hivyo, baadhi ya miongozo hiyo imewagusa baadhi ya wadau wa sekta ya elimu akiwamo Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Taasisi ya HakiElimu, Godfrey Bonaventure, ambaye RAI limezungumza naye na kupata kufursa ya kudadavua mambo mbalimbali.

 RAI: Juni mwaka huu Serikali ilitoa vigezo vipya vya udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu na kufuta programu zilizokuwa zinawezesha baadhi ya wanafunzi wasiokuwa na sifa za kujiunga na elimu ya juu kuweza kupata shahada. Unafikiri uamuzi huo wa serikali una tija katika kuboresha sekta ya elimu nchini?

BONIVENTURE: Serikali inataka kuhakikisha kwamba vyuo vikuu vyote vinasimama kwenye misingi thabiti, ile changamoto ya miaka mingi kuwa vyuo vimekuwa vinalazimisha kuwa na vijicourse vingi hasa hivi vyuo binafsi kwa ajili ya kupata wanafunzi wengi.

Vyuo hivi vimekuwa vinasahau lengo lao na umadhubuti wa awali, kuhakikisha kwamba wanasimamia utoaji wa elimu bora na ukiangalia kumekuwa na changamoto ya wahadhiri na mambo mengine.

Ndio maana serikali imekuwa inazuia hizo foundation course zote ili kwanza zipite kule juu na kuhakikisha vyuo vinaboresha kwanza utoaji wa shahada na shahada ya uzamivu ndipo wafikirie kutoa astashahada na stashahada. Ila sasa kumekuwa na vurugu.

Sijatafiti kwa kina kuangalia lengo la serikali kuweka vigezo hivyo ila nadhani inataka kuhakikisha kuwa hakuna ubabaishaji ili kuhakikisha kwamba kama chuo kinataka kutoa elimu ya juu basi kitoa elimu ya juu ndio maana zamani kukawa na chuo kinatoa stashahada na astashahada na vingine vikatoa hizo shahada na shahada ya uzamivu.

Sasa kumefika mahali kila chuo kikuu kinataka kutoa stashahada.

Sio mbaya kwa chuo kutoa kozi zote, lakini unafikia mahali unatoa hivyo vitu kutokana na uwezo wa chuo, ila sasa imekuwa kama shamba la bibi kila chuo kinakimbilia kutoa kozi zote bila kuwa na usimamizi dhabiti. Tumekuwa tukivitengenezea mahitaji mengi bila kuwa na uwezo.

Kwa sasa hivi tumeanzia mbali kwenye udahili, kuhakikisha wanaokwenda vyuo vikuu wanakuwa na vigezo stahiki, hivyo lengo la serikali ni kuhakikisha vyuo vinatoa elimu bora na si shamba la bibi.

Na tulilegalega muda mrefu sana na hii ilikuwa kazi ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ambayo ilijikita kwenye udahili tu na kusahau viwango vya vyuo, sasa haingii akilini kusikia watu walikuwa wanatumia vyeti vya ndugu zao kusoma vyuo vikuu, tulikuwa wapi kudhibiti mambo ya aina hii.

Ingawa watu waliosoma na kumaliza wanabainika kutumia vyeti vya kidato cha nne na sita ambavyo si vyake. Sasa serikali inatakiwa kudhibiti vyote hivi, ubora wa chuo, anayesoma na wahadhiri wenyewe.

RAI: Pia kumekuwapo na vigezo vya utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, Nini kimechangia bodi ya mikopo kushindwa kutekeleza zoezi hilo ipasavyo?

BONIVENTURE: Suala la msingi ni kusimama kwenye miongozo ya bodi ya mikopo, kuwa imeanzishwa kwa ajili ya nini, na vigezo vinavyotakiwa kutumiwa ni vipi… kwa sababu kila kitu kinakwenda kwa sheria, lengo bodi ni kuwasaidia watanzania, si kuwakomoa, hata watanzania tumekuwa tukiwekeza kwa kiwango cha juu ili kila mmoja apate elimu ya juu. Masuala ya nani apate au nani asipate kulingana na vigezo ndio jambo la msingi.  Kumekuwa na changamoto sana katika urudishaji wa mikopo hiyo kwamba waliokuwa wanapata mikopo si wale waliokuwa wanastahili.

Hivyo sasa kinachotakiwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele vya nchi, kuna maeneo yenye changamoto kubwa sana kama udaktari na yale ambayo wananchi wana uhitaji lazima wasaidiwe kupata elimu ya juu kwa sababu ni ghali hivyo watoto wa matajiri watasoma na wa maskini hawatoweza kusoma.

Lazima kuwe na mfumo wa kuwabaini hawa wanafunzi wenye uwezo na wasiokuwa na uwezo wa kusoma. Katika kutekeleza suala hili lazima kuwe na dhana ya uwajibika, kwa sababu elimu ya chuo kikuu si ghali kama elimu ya msingi, kuna chekechea ambayo ada ni zaidi ya milioni tatu wakati kuna vyuo vingine vina ada kuanzia Sh 800,000. Kama mtoto amesoma chekechekea na shule binafsi za sekondari za aina hii lazima mzazi awajibike kumwendeleza.

Bodi ingetakiwa kuanza na rekodi hizo ila bado wanakumbana na ubabaishaji ambao umekuwa mkubwa sana hivyo lazima tuwe na uzalendo ambao ni vipaumbele vikubwa vya nchi kwa sababu haiwezekani mtu aweze kusoma kuanzia msingi hadi sekondari shule binafsi ashindwe kusomeshwa chuo kikuu, ila kuna wengine wazazi wao wamefariki kipindi hajamaliza hilo nalo ni la kuzingatia.

RAI: Kumekuwapo na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na udahili katika sekta ya elimu nchini kila kiongozi mpya anapoingia madarakani, unafikiri mabadiliko haya yatatufikisha katika kuifikia elimu bora nchini?

BONIVENTURE: Suala la mabadiliko mabadiliko linatuvuruga. Kwa sababu tunashindwa kwenye misingi kwa kuwa hatuna miongozo… ndio maana HakiElimu tunasema lazima tuwe na falsafa ya nchi ili kiongozi yeyote anayekuja ajue tunaelekea wap?

Pia tuwe na malengo ya kitaifa kama ni teknolojia tujue ili tufikie hapo tunafanya nini. Kama watoto wawe na teknolojia, uchumi na mambo mengine, baada ya hapo lazima tuwe na mfumo, mipango mikakati ya muda wa kati na muda mrefu, hapo itatuambia shule zote tuziendeshe na walimu tutawaandaje na wanafunzi watatathminiwa vipi na hata maendeleo yao.

Tukiwa na hayo tutakuwa na misingi imara kwa sababu kukitokea kiongozi anataka kuondoa biashara tunamkatalia kuwa mipango yetu ni suala hili ama lilea. Sasa tunaishi kwa matamko hatuna falsafa wala mipango yetu, hatuna mipango kutoka juu.

RAI: Rais John Magufuli anatarajiwa kutimiza mwaka mmoja madarakani wiki ijayo, Unazungumziaje utekelezaji wa mojawapo ya ahadi yake ya utoaji elimu ya msingi na sekondari bure na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu?

BONIVENTURE: Ahadi hiyo sitoizungumzia sasa kwa sababu tumefanya utafiti kuhusu suala hilo, tumezungumza na wadau hivyo ndio tupo katika hatua ya kwanza ya uandaaji wa ripoti ya utafiti huo, hivyo tusubiri wiki ijayo tutaizindua hiyo ripoti.

RAI: Unafikiri tumepiga hatua katika suala zima la kutahini wanafunzi na kuboresha sekta ya elimu nchini?

BONIVENTURE: Kuna kitabu cha serikali cha takwimu pia kuna tafiti za benki ya dunia na za haki elimu ambazo kwa pamoja zinazungumzia namna ya kurejesha hadhi ya walimu,  pia walimu wetu namna wamefuzu vigezo na wanahamasa kufundisha.

Tanzania imefanikiwa katika udahili kwa kiasi kikubwa kwani ndani ya miaka 10 iliyopita kuanzia shule za msingi hadi elimu ya juu tumevuka kwa zaidi ya asilimia 200. Tulikuwa na shule za msingi 12,000 sasa zipo 16,000, shule za sekondari  900 sekondari sasa zimefikia 4600, vyuo vilikuwa 10 sasa vipo 46, wanafunzi vyuo vikuu sasa zaidi ya wanaodahiliwa ni zaidi ya 200,000, wanafunzi wa shule za msingi sasa ni zaidi ya milioni 10. Hatua hizi zilifanikisha kupewa zawadi benki ya dunaini katika kipengele cha  mpango wa elimu kwa wote, eneo hilo tulifanikiwa, ila shida ikaja kwenye utenganifu katika suala la ubora.

Miaka saba tumekuwa na kipindi kibaya sana katika ubora wa elimu, zaidi ya wanafunzi asilimia 50 wanafeli katika shule za msingi na sekondari, na sasa ufaulu ni asilimia 68 licha ya kwamba tunatekeleza matokeo makubwa sasa.

Lakini miaka mitano kurudi nyuma ilikuwa asilimia 50 hadi 60, ndipo kukafanyika mabadiliko matano hadi sita ya mifumo ya kutahini wanafunzi, Tume ya Pinda ikashauri turudi mifumo ya kutahini wanafunzi, kutoka kwenye mfumo ambao haubadiliki  tukaenda ambao unabadilika.. wakaondoa division sifuri.

Tafiti nyingine kama ya Uwezo ambayo ilitoka hivi karibuni ilionesha kuwa kati ya watoto 10 watano tu wanaweza kusoma habari ya darasa la pili wakiwa la tatu, wakati watoto wawili kati ya 10 wana uwezo kusoma habari ya kiingereza wakiwa darasa la tano. Pia ilionesha watoto wanne kati ya 10 wa wa darasa la tatu ndio wenye uwezo wa kukokotoa hesabu, wanafunzi kumaliza darasa la saba hawajui KKK hii ndio hali halisi, Ni dhahiri kuwa tunahitaji kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu.