Home Makala Kung’oa viti, kuua watafiti, kupigwa mwanafunzi ni msingi mmoja

Kung’oa viti, kuua watafiti, kupigwa mwanafunzi ni msingi mmoja

2497
0
SHARE
Nape nnauye akikagua uharibifu wa viti uwanja wa taifa

NA M. M. MWANAKIJIJI

Kuna matukio matatu yametokea wiki kadhaa zilizopita ambayo unaweza kudhani hayahusiani kabisa, lakini ukiyaangalia kwa karibu, unaweza kuona yote yananing’inia kwenye kamba moja. Matukio haya yamegusa hisia za wananchi kwa namna mbali mbali, lakini msingi wake ni matukio ambayo hayakupaswa kutokea kabisa.

Tukio la kwanza lilitokea Uwanja wa Taifa wakati wa mechi ya watani wa jadi. Baadhi ya mashabiki wa Simba wakionesha hasira baada ya kukubaliwa goli ambalo wengi wanaamini lilipaswa kukataliwa kwa sababu mchezaji aliunawa mpira.

Mashabiki waliamua kung’oa viti katika uwanja huo mpya wa kisasa. Inasadikiwa kuwa walisababisha hasara ambayo inakadiriwa kuwa si chini ya shilingi milioni 200.

Tukio la pili lilitokea mkoani Dodoma ambapo watafiti wa Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian kilichopo Arusha, waliuawa na wananchi na kisha kuchomwa moto wakiaminiwa kuwa ni “wanyonya damu”.

Taarifa zote za awali zinaonesha kuwa watafiti hao waliuawa baada ya kina mama kudhani kuwa wamevamiwa eneo hilo na watu wenye nia mbaya nao. Cha kusitikisha zaidi ni kuwa watu waliofika pale, badala ya kuwasikiliza, waliamua kuwashambulia wakiamini kabisa kuwa watu hao ni wanyonya damu.

Kuuawa kwa watumishi hao kumeacha majonzi makubwa kwa familia na kwa Taifa, kwa sababu wameuawa bila sababu ya msingi na katika mazingira ambayo katika karne hii wangeweza kabisa kuwekwa chini ya ulinzi na kutafuta uhakika zaidi kuhusu wao ni nani hasa.

Kwamba, wananchi hawakuwa na uvumilivu wa kutaka kujua zaidi au kwenda kwenye vyombo vya dola na kuamua kujichukua hatua wenyewe, ni jambo la kumkasirisha mtu yeyote anayeheshimu jamii inayoamini katika utawala wa sheria.

Tukio la tatu ni la kupigwa kwa mwanafunzi huko Mbeya na walimu waliokuwa mafunzoni, kwa kitu ambacho hakikupaswa kufikia kilikofikia. Kitendo cha wanaume watu wazima, tena wenye dhamana ya kutoa elimu, kumshambulia kijana mdogo kwa sababu yoyote ile, ni kitendo kinachopaswa kulaaniwa na kila mtu.

Cha kusikitisha zaidi ni kuwa tukio lile limetokea mbele ya hadhara na hakuna mtu aliyeweza kuwazuia walimu wale na wao wenyewe walikosa akili ya kujua kitendo wanachofanya siyo tu ni cha kihalifu (criminal), lakini zaidi ni kitendo ambacho kimeudhalilisha utu wao wenyewe.

Matukio haya matatu kama nilivyosema, yamening’inia kwenye kamba ile ile. Kamba hii ina mambo kadhaa. Matukio yote matatu msingi wake ni ujinga (ignorance). Kuna msemo kuwa “kama unadhani elimu ni ghali sana, basi jaribu ujinga”.

Nchi nyingi duniani ambazo zimerudi nyuma kimaendeleo na ziko nyuma sana, ni jamii ambazo pia masuala ya elimu yako nyuma. Ujinga una gharama kubwa sana kwa watu. Ndio maana wenzetu walioendelea walifanya hivyo kwanza kabisa kwa kutambua umuhimu wa kujua na kufahamu mambo, badala ya kuishi kwa imani na kudhania tu.

Tanzania tunaongoza kwa imani za kishirikina kiasi kwamba kuna baadhi ya vitu tunaamini, na tuko tayari kuamini hata kama tunajua haviwezekani au ni vya kijinga. Matokeo yake ni rahisi kuburuzwa au kujikuta unafuata mkumbo fulani. Ujinga una gharama kubwa sana.

Goli hata kama halikuwa halali, siyo jambo ambalo linaweza kumfanya mtu mwenye akili kuamua kuvunja kiti kwa sababu ya hasira! Ni mjinga tu mwenye kufanya hivyo. Mtu mwenye akili– na tumewaona wengine kwenye nchi nyingine ambapo timu wanazozipenda zimefungwa magoli kama lile la Yanga, lakini hawakuvunja viti au kitu kingine chochote – kwa kuwa wanajua kuwa hapaswi kufanya hivyo. Zaidi wataishia kumrushia maneno refa na kusubiri mchezo uendelee.

Hili ni kweli hata kwenye suala la kuuawa kwa watafiti. Msingi wa mauaji yale ni ujinga ule ule. Hivi leo bado wapo watu wanaamini kabisa kuna “wanyonya damu”? Na wanyonya damu ni kina nani? Zamani hata sisi wengine tuliamini ukiona gari lenye msalaba mwekundu ujue ni la “wanyonya damu”.

Kumbe magari yale yalikuwa ni ya chama cha Msalaba Mwekundu. Lakini ujinga ni upi? Kumbe chama cha Msalaba Mwekundu kuna wakati kweli wanafanya shughuli za kuchangisha damu kwa ajili ya kusaidia hospitali ili kuokoa maisha ya watu.

Unaweza kweli kuwaita “wanyonya damu” lakini ukiishia hapo utakuwa ni mjinga mwingine; unyonyaji damu unafanywa wazi na kwa taratibu na katika ulimwengu huu, sote tunapaswa kujua kuwa kuchangia damu siyo jambo la kichawi.

Watu waliowashambulia watafiti kwa sababu wamesikia ni “wanyonya damu” ni wazi hawakuwa na maarifa haya. kwani wangekuwa nayo wangepaswa kujiuliza maswali kadha wa kadha. Lakini siwezi kushangaa wapo watu wengine wasomi kabisa wakiambiwa “yule ni mnyonya damu” wanaanza kumkimbia! Na wanaweza wakawa miongoni mwa watakaomshambulia! Ujinga una gharama sana!

Jambo jingine ni kuwa matukio yote matatu yametokea mbele ya hadhara na yakihusisha saikolojia ya kundi (mob psychology), yaani kufuata mkumbo. Mtu mmoja alianza kung’oa kiti wengine wakafuata, mtu alianza kushambulia watafiti na wengine wakafuatia. Mwalimu mmoja alianza kumchapa mwanafunzi na wengine wakafuatia! Katika haya yote tunaweza kujiuliza walikuwa wapi mashujaa wa kusema “hapana”?

Kama polisi wasingeingilia kati, Uwanja wa Taifa ungekuwaje? Kushindwa kuwazuia wanakijiji matokeo ni vifo, na kama labda video isingekuwepo ya mwanafunzi kuonekana akipigwa na angalau sauti ya nani sijui ikiwasihi kutokumuumiza, matokeo yangekuwaje? Hivi yule mwanafunzi angeuawa walimu wale karibu sita wangeweza kweli kusimama na kusema kisa kilikuwa nini? Kwamba, hawakujifunza huko chuoni maana ya “mob psychology”?

Utaona basi kuwa matukio haya matatu, yanatufundisha mambo mengi na muhimu. Machache ya kuweza kuyatafakari ni kuwa ni vizuri sana watu kujitahidi kujua zaidi juu ya jambo kuliko kudandia mbele ya safari. Ni vizuri kujifunza kupima matokeo ya matendo, kabla ya kutenda na kujua ni kitu gani hakipaswi kuwa. Ni vibaya sana kuishi kwa kudhaniam, hasa kama kuna nafasi ya kuweza kujua zaidi.

Matukio yote matatu yangeweza kuepukika kabisa kama watu wangetumia dakika chache kujijuza zaidi juu ya jambo fulani na kupima uzito wake.

Lakini pia matukio haya yanatufundisha umuhimu wa kujifunza kujizuia (self-control), hasa unapokuwa katika kundi. Mara nyingi nimekuwa nikitolea mfano wa jinsi gani miaka mingi nyuma nilifika mahali nimeshuka kwenye daladala na watu wengine tukakuta, kijana ameitwa “kibaka” na watu wakaanza kumpiga.

Watu tulioshuka nao kwenye daladala, bila kujua kijana anadaiwa kuiba nini na kama kweli ni kibaka, au vipi nao wakaanza kurusha ngumi na teke huku wakiendelea na safari zao! Wachache kati yetu tuliweza kumchukua yule kijana ili kumuokoa na kuhakikisha amefikishwa Polisi Msimbazi pale. Kama tusingeamua kuingilia kati katika hali ile ngumu sijui ingekuwaje.

Ni hatari sana kukaa kimya mbele ya uovu. Na wakati mwingine inawezekana mtu asisikike, lakini watu wengi wakisimama pamoja kupinga jambo fulani wanaweza kuwa na nguvu.

Majasiri walikuwa wapi wakati watu wanavunja viti? Majasiri walikuwa wapi wakati watafiti wanauawa? Majasiri walikuwa wapi wakati mwanafunzi anapigwa na watu wanaangalia? Nani angekuwa na ujasiri wa kwenda kumkinga yule mtoto badala ya kusema “mwalimu mtamuumiza”?

Ndugu zangu, matukio haya yatulazimishe kujichunguza sisi wenyewe na tujiulize; Je, kama sisi tungekuwa katika moja ya matukio hayo, tungekuwa upande gani? Tungefanya nini? Je, tungeweza kuzuia yasitokee? Au sisi tungekuwa ndio wale?

www.zamampya.com