Home Habari kuu PROFESA LIPUMBA AMGEUKIA JPM

PROFESA LIPUMBA AMGEUKIA JPM

1824
0
SHARE

Sasa atamani kufanys kazi na Maalim Sief

NA GABRIE MUSHI

WAKATI Rais John Magufuli akitarajiwa kutumiza muda wa mwaka mmoja madarakani tangu aapishwe kushika wadhifa huo Novemba 5 mwaka jana, mmoja wa wanazuoni maarufu na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameukosoa uongozi wake na kusema kuwa utekelezaji wa ahadi ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda ni jambo ambalo haliwezekani.

Profesa Lipumba alikwenda mbali zaidi na kuchambua baadhi ya mambo ambayo yameonekana kukwamisha utekelezaji wa ahadi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine pia alibainisha wazi kuwa lengo hilo la Rais Magufuli ni kubwa mno.

Akizungumza na RAI juzi, Profesa Lipumba alisema kuifanya Tanzania kuwa nchi inayotegemea uchumia wa viwanda ni jambo ambalo linahitaji muda wa utekelezaji kwani kuna mambo muhimu ambayo yapaswa kuzingatiwa ili kufikia mafanikio hayo.

Profesa Lipumba alitole mfano huduma za uzalishaji na usambazaji wa huduma za umeme wa viwandani kuwa bado ni kikwazo nchini ikiwamo ni pamoja na mazingira ya uwekezaji na ya kufanya biashara vilevile.

“Kwa sababu masuala ya maendeleo ya viwanda ni yanategemea zaidi sekta binafsi kuliko uwekezaji wa serikali, serikali inajenga miundombinu na kuweka mazingira, tunatakiwa kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi, pamoja na sera zinazotabirika, kwa mfano taratibu za uwekezaji ziko vipi, vivutio vinavyotolewa vinaonekana, ulinzi wa viwanda unaeleweka, hilo ni muhimu katika sekta ya viwanda, miundombinu ya barabara na umeme, na mawasiliano haya ni mambo ambayo bado hayajaimarika hapa kwetu,” alisema.

Aidha, alisisitiza ”Kutokana na changamoto hizo ni wazi kuwa lengo alilojiwekea ni lengo kubwa mno haliwezekani kwamba sekta ya viwanda ifikie kuzalisha ajira kwa zaidi ya asilimia 40,  hilo hata katika nchi ambazo zimekua na viwanda hazijafikia, mfano Korea ya kusini au China hazijafikia, zinaanza katika kiwango cha chini sana asilimia tano, ikiwamo viwanda vidogovidogo,” alisema.

Sijapata ushirikiano na Maalim Seif

Pamoja na mambo mengine, Profesa Lipumba hakusita kuzungumzia ushirikiano kati yake na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye hapo awali aliongoza kikao cha kutomtambua Mwenyekiti huo na kuzua mtafaruku uliozimwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini bila mafanikio.

“Katika ushirikiano, bado naendelea kufanya jitihada kwa sababu sipati ushirikiano kutoka kwa katibu mkuu wangu, lakini kwa upande wa viongozi wengine wa chama napata ushirikiano mzuri mfano wilaya za kusini wanachama wana hali nzuri hamasa imeongezeka ya ujenzi wa chama, Dar es Salaam, Bagamayo viongozi wana ari nzuri, katika kipindi hiki tunahitaji kujenga chama, hasa baada ya kumalizika uchaguzi mkuu kwa sababu shughuli za ujenzi wa chama ziliakua bado hazijaanza.

“Jambo la msingi niwaambie wana CUF kuwa mtandao wetu Zanzibar upo vizuri, kazi kubwa ni Tanzania bara, lengo ni ujenzi wa chama tunatakiwa kujenga zaidi huku, hivyo nitoe wito kwa ndugu zangu wa Zanzibar kuwa muungano imara ambao nutatokana na chama chetu kuwa imara pande zote.

Aidha, alisema ujio wa Edward Lowassa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa namna moja au nyingine pia umechangia kukivuruga chama hicho hasa baada ya Chadema kufanikiwa kutumia vizuri nafasi ya umoja huo unaoundwa na vyama vinne vya siasa.

“Tulikosa umoja uliokuwa mzuri na wenzetu Chadema wakautumia, kwa sababu kwa upande wa Chadema kwa kuzingatia msimamo ambao walikuwa nao kwa muda mrefu walijipambanua katika suala la kupinga ufisadi sasa Lowasa aliguswa katika orodha ya mafisa na Dk. Slaa, ni wazi kabisa taswira ya Chadema ambayo Dk. Slaa aliipambanua imevurugika, ndio maana CCM na Rais Magufuli wakajijenga,” alisema.