Home Makala Wahariri wamekisahau kilimo, kulikoni?

Wahariri wamekisahau kilimo, kulikoni?

2416
0
SHARE

Mwaka mmoja wa utawala wa Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli umetimia wiki iliyopita Novemba 5, 2016. Hapana shaka hata kidogo kwamba umekuwa ni mwaka wa kufuatilia kwa karibu kila hatua ya uongozi mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni kipindi ambacho wale waliokuwa hawajajiridhisha kuhusu usahihi wa uamuzi wao wa kumpigia kura mgombea huyo wa urais kupitia CCM walikuwa wakifuatilia kwa karibu kila hatua ya maamuzi yake na kuona kama uamuzi wao wa kumpigia kura ya ndiyo kama ulikuwa sahihi.

Miongoni mwa waliompigia kura za ndiyo kiongozi huyo bila shaka ni wakulima, wavuvi na wafiugaji ambao ndio walio wengi miongoni mwa wapiga kura. Hilo la wingi wa watu hao miongoni mwa wapigaji kura halina ubishi wala halihitaji uthibitisho wa Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC). Ni ukweli usiopingika kwamba wapiga kura walio wengi nchini ni wakulima, wavuvi na wafugaji.

Mwaka mmoja baada ya Rais John Pombe Magufuli kula kiapo cha kuiongoza Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano swali ambalo pengine lilikuwa ni la msingi na muhimu kwa kiongozi huyo katika kuadhimisha mwaka mmoja wa uongozi wake lingekuwa nini alichokifanya, alichopanga kukifanya na anachodhamiria kukumbukwa nacho katika sekta hiyo muhimu sana katika uchumi wa Tanzaniua.

Mwaka mmoja wa utawala wa Rais Magufuli kwa mwananchi wa kawaida na huyo anayeitwa mwananchi wa kawaida kwa hakika ndiye hasa mwananchi wa Taifa hili uliyakiwa kuwa wa kufanya tathmini kuhusu kilichofanyika katika mwaka mmoja, kinachofanyika na kile kitakachofanyika hapo baadae.

Ni tathmini ambayo haimithiliki kutokufanyika kwa sababu kila taarifa kuhusu uchumi inasema kwamba Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi. Sasa iweje nchi iwe ya wakulima na wafanyakazi halafu tathmini ya utendaji wa serikali usizungumzie kuhusu wakulima na wafanyakazi kwa ujumla wao na mchango wao katika uchumi wa taifa?

Katika mkutano wake wa kwanza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari pamoja na wahariri waandamizi wa kujitegemea uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam siku ya Ijumaa Novemba 4, 2016 yaliulizwa maswali mengi na bila shaka majibu yalikuwa yanalingana na maswali yaliyoulizwa.

Tathmini binafsi iliyofanywa na Rais Magufuli ilijikita katika kutoa maelezo ya mwelekeo mzima wa utawala wake na bila shaka aliweza kutoa maelezo kwa kadiri ya jinsi mazingira yalivyomruhusu.

Pamoja na wahariri kuuliza maswali mengi lakini kuna jambo moja ambalo lilijitokeza wazi kabisa na ambalo lilituacha baadhi yetu tukijiuliza maswali mengi.

Katika tathmini iliyotolewa pamoja na Rais Magufuli kusema kwamba wakulima wa korosho huko kusini mwa Tanzania wanafaidika na jitihada za serikali kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa bei muafaka kwa mazao yao na kutolea mfano wa zao la korosho ambalo limefikia hadi shilingi elfu 4 kwa kilo, hakuna swali lolote lile lililojitokeza kuhusu suala la kilimo na mustakabali wa wakulima katika nchi yetu. Hiyo si bahati mbaya, la hasha.

Ni ushahidi wa wazi kabisa kwamba wahariri wetu hawakitambui kilimo kama mchangiaji mkubwa katika pato la taifa na pia kuwa ni mwajiri wa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wote.

Haiyumkiniki hata kidogo kwamba sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji ambayo ni muhimili mkubwa sana katika uchumi wetu haikusikika ipasavyo katika mkutano huo na mkuu wa nchi isipokuwa kwa tuhuma na lawama za mifugo kuingilia au kuvamia maeneo ya hifadhi.

Tatizo liko wapi? Kwa nini wahariri wetu hawakuuliza maswali ya kumsaidia mkuu wa nchi kutoa maelezo ya mwenendo na mwelekeo wa serikali yake katika sekta hiyo muhimu sana katika uchumi na maisha ya Watanzania.

Ni wazi kabisa kwamba wahariri wetu ni wa mjini zaidi na kinachowagusa ni siasa na kwa kiasi fulani viwanda.

Ikumbukwe kwamba kuzungumzia viwanda katika nchi kama Tanzania ni lazima uzungumzie kilimo, uvuvi na ufugaji. Si rahisi kuwa na viwanda vyenye tija kwa maisha ya watu wengi hapa nchini kwetu kama kilimo, uvuvi na ufugaji havitakuwa sekta lengwa katika zoezi zima la kuendeleza viwanda hapa nchini.

Kiwanda ambacho kitajengwa kwa ajili ya kutoa ajira tu kwa watu bila ya kujali ni kwa kiwango na kiasi gani kiwanda hicho kitachangia katika kuboresha maisha ya wakulima, wavuvi na wafugaji kitakuwa si mahali pake kwani haina maana yoyote kujenga viwanga ili mradi kama haviongezi thamani katika sekta hiyo muhimu sana.

Bila hata kurejea katika nyaraka za chama tawala CCM, Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi. Kwa mantiki hiyo mageuzi yoyote yale ya uchumi ni lazima yazingatie kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu na kwa mantiki hiyo idadi kubwa ya Watanzania ni waajiriowa katika sekta hiyo.

Pengine wahariri wetu hawatambui nafasi ya kilimo, uvuvi na ufugaji katika maisha yetu, Pengine magari na barabara pana za Dar es Salaam zimewaondoa kabisa kutoka katika uhalisia wa maisha yetu hapa nchini. Huenda ndiyo sababu hakuna aliyeuliza swali kuhusu mustakabali wa wakulima, wavuvi na wafugaji ili kupata maoni na maelezo ya mkuu wa nchi kuhusu mambo hayo muhimu sana.

Ilikuwa ni wakati muafaka wa kumuomba Rais Magufuli atueleze dira yake kuhusu kilimo, uvuvi na ufugaji. Kwamba kilimo cha Tanzania kitaendelea hadi lini kutegemea mvua na ni lini tutakuwa na miundo mbinu mizuri ya kumwagilia maji ikimaanisha kuwa na miradi mikubwa ya umwagiliaji kama njia mojawapo ya kuwafanya wakulima wawe na uwezo wa kuzalisha zaidi ya mara mbili au hata tatu kwa mwaka.

Ulikuwa ni wakati muafaka kabisa wa kumuomba Rais Magufuli atoe msimamo wake kuhusu kilimo na kumshauri aielekeze wizara ya kilimo na umwagiliaji kuhakikisha kwamba unafanyika mkakati maalum wa kitaifa wa kueneza teknolojia ya kisasa ya umwagiliaji mashamba kwa kutumia mitambo ya kudondosha maji badala ya mtindo wa hivi sasa ambao maji yanamwagwa kwa kutumia mifereji na hiyo kupotea kwa wingi bila ya faida yoyote.

Kwa hakika ulikuwa ni wakati wa kumshauri Rais Magufuli aziagize wizara zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na biashara na viwanda, kilimo na umwagiliaji na mambo ya nje kuhakikisha kwamba uwekezaji katika viwanda unafanyika kwa kuzingatia mahitaji ya kilimo, uvuvi na ufugaji.

Mantiki ya kawaida inadai kwamba taifa ambalo walio wengi ni wakulima, wavuvi na wafugaji basi na viwanda vyake vingi ni lazima kwa makusudi kabisa visaidie kuboresha sekta hiyo muhimu.

Kwa nini waandishi wetu hawa waandamizi hawakumshauri Rais ili shirika la viwanda vidogo hapa nchini lisaidiwe ili kuanzisha viwanda vidogo kwa ajili ya kuisaidia sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji?

Hadi leo mkulima wa Tanzania hana mashine ndogo, ya kati au kubwa kwa ajili ya kukamua mafuta kutokana na mazao anayozalisha.

Katika nchi ambayo inazungumzia kuinua uchumi wa wananchi hadi kuwa wa kati ni lazima kila jitihada zifanyike kuongeza vipato vya wananchi wa kawaida. Vipato haviwezi kuongezeka kama mazao wanayozalisha hawataweza kuyachakata walau katika awamu ya mwanzoni ili kuuza kwa bei bora zaidi.

Rais Magufuli hana budi kutupia jicho maisha ya wakulima, wavuvi na wafugaji na kuhakikisha kwamba maneno matamu na matupu ya kisiasa yanatupiliwa mbali na nafasi yake kuchukuliwa na vitendo vya makusudi kabisa vinavyolenga katika kuongeza uzalishaji na hivyo kuongeza kipato katika sekta hiyo.

Ni wazi kwamba kama Rais Magufuli ataelekeza mawaziri na watendaji wake kuhakikisha kwamba viwanda tunavyovijenga vinaongeza tija katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji.

Mvuvi wa Tanzania anatumia nyenzo duni sana na hili wahariri wetu wanaweza kujiridhisha kwa kutembelea maeneo yote ambayo ni ya uvuvi. Uduni wa vifaa vya uvuvi unatokana kwa kiasi kikubwa na ukweli kwamba tunaagiza kila zana kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa sana.

Kama idadi ya watu waliopo kwenye uvuvi ni kubwa na inatosheleza kuwa na kiwanda cha kuzalisha zana na nyenzo za uvuvi kwa nini tusielekeze nguvu huko? Hilo si ni suala ambalo wavuvi wangelisikia Rais wao akilizungumzia wangelifarijika na kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora kushinda leo? Kwa nini hajaulizwa? naamini angeulizwa angetoa majibu.

Hatuwezi kuzungumzia Tanzania ya uchumi wa kati kwa kuangalia tu upana wa barabara, barabara za juu na majengo marefu ya kutisha. Watanzania walio wengi ama ni wakulima, wavuvi na wafugaji au ni watu ambao maisha yao kwa njia moja au nyingine yanategemea sekta hiyo.

Kwa mantiki hiyo basi haiyumkiniki hata kidogo kuzungumzia maendeleo kama bado tunalima kwa kumtumainia Mungu alete mvua, au tunanyweshea mashamba kwa kutumia mbinu za kale badala ya kuwa na vifaa na mitambo ya kisasa ambayo inawezekana kabisa kuitengeneza hapa nchini.

Nashadidia hili la umwagiliaji kwa sababu tuna viwanda vya kuzalisha vifaa mbalimbali vya plastiki vya maji lakini mabomba kwa ajili ya umwagiliaji maji mashambani hatuzalishi. Ninamaanisha mabomba ya umwagiliaji kwa njia za kisasa yaani umwagiliaji mdondosho.

Hivi ni vifaa ambavyo vinaweza kuzalishwa nchini lakini la ajabu ni kwamba viwanda vyetu vinazalisha matanki ya kuhifadhi maji ambayo hayamsaidii sana mkulima huko kijijini.

Pengine wahariri wangeweza kumshauri Rais Magufuli kuitaka wizara inayoshughulikia umwagiliaji kuona uwezekano wa kuvitaka viwanda vya mabomba hapa nchini kuanza kuzalisha vifaa vya umwagiliaji kwa ajili ya wakulima wetu kama ambavyo shirika la viwanda vidogo lingeweza kushauriwa kuwahamasisha wabunifu kuzalisha mashine mbalimbali kwa ajili ya kukamua ng’ombe na kuchakata maziwa na bidhaa zinazohusiana nazo.

Pamoja na pongezi zangu kwa wahariri kwa kushiriki mkutano na Rais Magufuli lakini nawashauri watambue kwamba Watanzania ni pamoja na wakulima, wavuvi na wafugaji. Na ikumbukwe kwamba bila ya wakulima, wavuvi na wafugaji haitawezekana kuizungumzia Tanzania yenye hadhi ya uchumi wa kati.