Home Makala Haiba ya kiongozi haijengwi kwa amri

Haiba ya kiongozi haijengwi kwa amri

2787
0
SHARE

Na Markus Mpangala

ULIMWENGU wetu kwa sasa umejaa habari nyingi mno kupitia uvumbuzi wa teknolojia. Ulimwengu huu umesababisha mambo mengi kuripotiwa. Teknolojia iemchangia kwa kiasi kikubwa kumulikwa kwa mambo mengi mno kuliko wakati wowote.

Labda, kwa Tanzania tulichelewa kumulika mambo hayo, lakini viongozi wa sasa wanatakiwa kuelewa kuwa tuendako watamulikwa zaidi hata muda wanaokwenda Maliwatoni. Hii ni moja ya matunda ya teknolojia.

Katika ulimwengu huu wa teknolojia tumekuwa tukimulika karibu kila jambo. Tunamwangalia kiongozi namna anavyozungumza. Tunatazama hulka zake wka kila tukio au jambo linalohusu mamlaka yake. Tunatazama kila hatua ya maamuzi yake katika taasisi.

Mathalani, taasisi ya urais kwa sasa inamulikwa kuliko kipindi chochote. Vilevile jamii yetu inamulika mambo mengi yanayowazunguka. Jamii inazungumza kutoka mtaani kupitia teknolojia mpya (ikiwemo mitandao ya kijamii).

Yanajadiliwa mambo mazito na yenye kubeba mantiki ya mustakabali wa taifa letu. Yanamulikwa yale muhimu na yasiyo na umuhimu. Dhumuni kubwa ni kuhakikisha tunaondokanana ‘takataka’ zinazorudisha nyuma maendeleo yetu.

Miongoni mwa mambo muhimu katika maisha ya mwanasiasa au kiongozi wa taasisi yeyote ile ni Haiba. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TUKI toleo la tatu inasema, ‘Haiba’ ni hali aliyonayo mtu inayowafanya wengine wavutike naye; uvutio wa heshima.

Kwa mantiki hiyo kiongozi anapokuwa na haiba yake wka jamii inaleta faida na kuchochea mambo mengi mno yenye tija. Mathalani, watanzania tumekuwa tukiimba jina la Mwalimu Nyerere kila kukicha.

Kadiri miaka inavyokwenda hata kizazi cha sasa kinataka kumjua zaidi Nyerere. Tunajua dosari zake ambazo zinaerekebishika. Tunajua haiba yake kama kiongoni ni mwenye msimamo, heshima, anaelekeza, anasisitiza, anawajibika, anakataza, mwadilifu na kadhalika.

Ni sababu hiyo hata alipostaafu urais bado tulijikuta tunamhitaji kwa masuala mbalimbali ya kiuongozo. Haiba yake imejengwa katika misingi ya eshima.

Sifa ya kiongozi siyo kuwafokea hovyo wasaidizi, lakini inaruhusiwa kusahihisha na kuwagombeza kwa heshima vilevile. Haiba ya kiongozi haijengwi kwa kuchukua hatua kali pekee dhidi ya wakosaji bali pale kiongozi anapokuwa mstahimilivu juu ya suala ambalo linatakiwa kuadhibi vikali.

Haiba huvutia watu kwenye jamii. Humwona kiongozi wao kama kimbilio. Haiba inawafanya watu waone sifa bora kutawalwia naye. Hakuna haiba ya mbovu kama kiongozi kudhani kuwa kulala selo au kuyazoea magereza ndiyo sifa.

Haiba mbovu ni pamoja na kushindwa kuhuisha fikra za kiongozi na matakwa ya kisheria au jamii husika. Jamii humsikiliza kiongozi kwa heshima, vivyo hivyo inatakiwa kiongozi ajifunze kuheshimu watu pia.

Madaraka si kigezo cha kukejeli watu au kuwa juu ya sheria.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya utawala na siasa, Elanie Kamarck, aliyeandika kitabu cha “Why President Fail And How They Can Succeed Again,” (2016) anasema, “Rais yeyote anayefanikiwa kwenye uongozi wake ni yule ambaye atamudu kuitumia Taasisi ya Urais na nafasi yake katika mambo makuu matatu; Utekenezaji wa sera madhubuti, Mawasiliano na watawaliwa na wasaidizi wake (mawaziri,makatibu, na watendaji wengine) na utekelezaji, tathimini ya mipango (kufanikiwa na kutofanikiwa),”.

Anaeleza kuwa Urais siyo hotuba nzuri kwa wananchi. Urais ni lazima uwe na mipaka ya kufanya uamuzi, hiyo ni pamoja na maofisa na washauri wa kitaalamu wa Taasisi ya Urais na Rais mwenyewe.
Katika muktadha huo, neon ‘Rais yeyote” tulitumie kwa kiongozi yeyote Yule kuanzia ngazi ya Kaya, Mtaa, Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya, Jimbo, Mkoa, Kanda na kadhalika. Kwamba njia nzuri ya kiongozi huyo kuwasiliana na jamii yake ni kuhakikisha anawajenga heshima na wao wajenge heshima.

Pili, kiongozi anatakiwa kuwa na uamuzi unaoeleweka. Kiongozi anatakiwa kuwa na hulka ya uvumilivu kila inapobidi na kuelekeza kwa msimamo thabiti unaoeleweka kwa jamii.
Kiongozi yeyote anapojibu tuhuma kwa kumkatisha mto tuhuma papo kwa papo, basi huyo ana matatizo makubwa mno akilini (wenye hulka hizo wameja ubahau).

Hulka za kihuni zinapogeuzwa kuwa haiba ya kiongozi ni dalili za kuficha udhaifu wa kushindwa kumudu majukumu kwa wanajamii. Kulala au kugeuza jela kuwa sehemu yao ya kawaida si sifa inayojenga jamii wala haiba ya kiongozi zaidi ua uhuni uhuni tu.
Aidha, hatunyoshi nchi kwa kuwalaghai watu kwamba dawa zipo Hiospitalini wakati uhaba umetukaba koo tunashindwa kupumua kuanzia mawio mpaka machweo.

Hatunyoshi nchi kwa kutowaheshimu watu. Kuitaka heshima ya wananchi bila kiongozi kuwaheshimu wao ni ukaidi usiovumilika. Ni lazima kiongozi anapotimzia wajibu wake akubali kuwa hayo ndiyo aliyotumwa na si hisani.

Mwandishi wa kitabu cha “The Character Factors: How We Judge America’s Presidents (2003),” James P. Pfiffner, anasisitiza haiba ya Rais wa nchi au mwanasiasa na kiongozi yeyote inatakiwa kuundwa na kulindwa kwa kiwango cha juu iwe faragha au hadharani.

Mtaalamu mwingine Samuel Kernell aliyeandikwa kitabu cha “Going Public: New Strategies of Presidential Leadership” (1997), anaungana na wenzake kwa kusema haiba ya Rais inaweza kuathiri utendaji kazi wake na wasaidizi wake, hivyo kudhoofisha ufanisi wa shughuli za nchi.

Ni lazima kuzingatia namna Rais, mwanasiasa, kiongozi yeyote wa kijamii anavyozungumza na wananchi wake. Namna anavyovaa uhusika. Namna anavyotamka maneno na kuwasilisha wka wananchi.

Namna anavyosisitiza jambo bila kuvunja heshima ya wengine. Namna anavyosomamia msimamo wenye tija kwa taifa. Namna anavyosikiliza kero na matatizo na kutoa majibu hujenga haiba ya Rais au kiongozi awaye yeyote kuwa mbovu au nzuri.

Haiba ya Rais mchapakazi pekee haijaweka msingi kuwa haiba ya moja kwa moja, huku ikiachwa ile ya ubinadamu kama, fikra zake, utulivu, mvuto wa heshima, ustahimilivu na kadhalika.

Tunapowatazama viongozi wetu tufikiri sana wanavyozungumza au kuwasiliana nasi. Wakati mwingine wanatia aibu mno, kwakuwa hawajengi vema haiba zao. Hizi si zama za ‘nimewachana’, bali ni za kushindana kuwapatia wananchi maendeleo pamoja na kutoa uhuru wa kujifanyia shughuli za msingi na ziada.