Home Makala SERA MBOVU ZIMEPOROMOSHA VIWANGO VYA ELIMU MASHULENI

SERA MBOVU ZIMEPOROMOSHA VIWANGO VYA ELIMU MASHULENI

2309
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Siku zote tunaambiwa kwamba taifa lisilo na elimu haliwezi kupiga hatua za maana kimaendeleo, achilia mbali maendeleo binafsi mtu mmoja mmoja. Daima hukumbushwa kwamba neema mbele yetu itatokana na elimu tu.

Tena elimu iliyo bora, wanaongezea. Lakini kwa Watanzania walio wengi huu ni wimbo kutoka serikalini unaonekana si kitu ambacho mtu anaweza kukitia maanani.

Kama Alvin Toffler, Mmarekani mtunzi wa riwaya alipata kunena “wajinga wa karne hii ya 21 hawatakuwa wale wasiojua kusoma na kuandika, bali ni wale ambao hawawezi kujifunza kutoka kwa wengine” basi Tanzania inaingia vizuri katika mfano wa nukuu hiyo, hususan viongozi wake iwapo tu wataendelea kulihubiria suala hilo bila ya vitendo.

Hakuna anyepinga kwamba elimu ina gharama kubwa, kifedha, lakini mbadala wake — yaani ‘ujinga’ pia una gharama kubwa kwa taifa na hasa kwa serikali yake ambayo ndiyo yenye kubeba jukumu la kuona wananchi wake wanapata elimu.

Hapa Tanzania elimu ni miongoni mwa vitu viwili ambavyo vimekuwa vinaibua mijadala mizito – kwa wanasiasa, wasomi na wananchi kwa ujumla – na hasa katika kuporomoka kwa viwango vyake. kingine ni kilimo, lakini afya nayo imeingia katika kundi hili.

Juhudi za “kuirudisha elimu katika njia yake” zina umuhimu sana kwani malengo na viwango vyake vilipotea mnamo katikati ya miaka ya 70. Ni muhimu kutambua kwamba elimu ilikuwa bora wakati ikitolewa bure – bure kwa maana yake halisi.

Ilikuwa bora kwa sababu serikali haikuwa inaizungumzia elimu kwa ndimi mbili – kwani iliposema elimu ni chombo cha maendeleo, ilikuwa inajua inasema nini na kumaananisha nini.

Hali kadhalika si kweli kwamba kila kilicho bora maishani hupatikana kwa gharama. Watanzania wengi, wakiwemo wale waliowahi kushika nyadhifa kubwa katika serikali na taasisi zake, zikiwemo zile za binafsi wanapaswa kukiri kwamba walipata nyadhifa hizo kutokana na elimu ya bure waliyoipata – kuanzia sekondari kwenda juu.

Sasa hivi mtu anaweza kuandika kurasa elfu kadha kuhusu kuporomoka kwa viwango vya elimu na kwa nini ilitokea hivyo na bila serikali kuonekana kuguswa.

Si rahisi kwa Watanzania walioanza kuingia darasani katika miaka ya karibuni, tuseme kuanzia miongo miwili hivi iliyopita – kuujua ukweli kwamba viwango vya elimu hapa nchini vimeporomoka sana.

Watanzania walioanza kwenda shule zamani –kuanzia miaka ya 80 kwenda nyuma ndiyo wanaelewa viwango vya elimu vimeporomoka. Uelewa wa mwanafunzi aliyehitimu Darasa la Saba sasa hivi ni tofauti na yule aliyemaliza darasa hilo hilo miaka ya 60 au 70. Kadhalika uelewa wa wahitimu wa sekondari (Kidato cha 4 na 6) wa miaka ya 60 na 70 ni tofauti sana na wale wa sasa.

Hakuna haja ya kuyakataa ‘matunda’ haya hasi ya elimu yetu tunayoyavuna zaidi ya nusu karne tangu tuwaondoe wakoloni ambao kama kuna kitu kimoja ambacho walikuwa wanakiwekea mazingira mazuri ni elimu – haidhuru ile ya msingi na sekondari iliyokuwapo hapa nchini wakati wa utawala wao.

Kitu gani basi kimekwenda ndivyo sivyo? Kuna vitu vingi sana ingawa serikali ambayo ndiyo yenye jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wake wanaelimika mara nyingi haitaki kuukubali ukweli huu. Mara nyingine imekuwa hata haitaki kukosolewa.

Hali ya kusikitisha katika sekta ya elimu inajionyesha kila mara serikali inapoonekana kukerwa pale inapokosolewa katika usimamizi wa sekta hiyo – ingawa kukerwa huku kupo pia katika madudu yake mengi tu katika sekta nyingine.

Kwa mfano, serikali ya Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa iliwahi kuyafungia matangazo ya televisheni na radio yaliyokuwa yakifadhiliwa na taasisi binafsi ya HakiElimu.

Matangazo hayo yalikuwa yakiikosoa serikali jinsi ilivyokuwa ikisimamia sekta ya elimu – kwa maneno mengine kuonyesha hali ya kusikitisha katika shule zetu. Ilikuwa ni kweli tupu lakini serikali haikupenda kuambiwa ukweli.

Kufungiwa kwa HakiElimu kuliendelea kwa muda chini ya serikali ya Jakaya Kikwete ambayo ilitaka kwanza HakiElimu iombe radhi, kitu ambacho kilikataliwa mara moja. Waombe radhi kwa kitu gani?

Kwa kusema viwango vya elimu vimeporomoka kutokana na hali duni katika shule hizo? Kwamba baadhi ya shule binafsi zinapewa leseni bila ya kwanza kukidhi viwango? Kwamba shule kadha za serikali hazina maabara hivyo kuuona wito mzima wa serikali kwa wanafunzi kujikita zaidi katika masomo ya sayansi kuwa kichekesho?

Kwa upande wake serikali hupenda kujikosoa yenyewe, na si kukosolewa na watu wengine. Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita wakati Margaret Sitta alipokuwa Waziri wa Elimu alisimama Bungeni kutoa tathmini ya wizara kuhusu utitiri wa shule binafsi zilizokuwa zinaanzishwa nchini.

Alisema serikali ilikuwa ina wasiwasi iwapo shule hizo zilikuwa zinakidhi viwango na kwamba itachukuwa hatua za kuhakikisha zinakidhi viwango vilivyowekwa na serikali. Aliongezea kusema lengo si tu kutoa elimu, bali kutoa elimu ya viwango.

Kauli kama hizi ndizo siku zote zimekuwa zikitolewa na watu mbali mbali wakiwemo wasomi, wanasiasa na wanaharakati na ndicho kitu ambacho HakiElimu imekuwa ikikisema. Sasa huyo waziri alikuwa anatangaza kitu tayari kinajulikana.

Na mapema 2013 mtafaruku mkubwa ulizuka Bungeni pale Mbunge wa upinzani, James Mbatia alipotoa hoja ya kutaka serikali impatie mitaala ya elimu inayotumika.

Kwani tukiachilia mbali uhaba wa fedha, kwa kiasi kikubwa elimu duni mashuleni inatokana na mitaala mibovu, kitu ambacho serikali imekuwa vigumu kukiri.

Laiti Waziri wa Elimu wakati ule, Dk Shukuru Kawambwa angekuwa mwerevu angeweza kumuwahi Mbunge Mbatia kwa yeye (waziri) kuizungumzia mitaala hiyo ya elimu kwamba ni mibovu. Kwani si mambo mengi tu serikali huwa inasema yamekaa ovyo ovyo na hayaendi sawa? Lakini haipendi kukosolewa huko kutoka kwingine hasa upinzani.

Aidha mara kadha kumetokea wito kwamba serikali ingepitisha sheria Bungeni ya kuweka marufuku kwa watoto wa Wabunge na Mawaziri kusoma shule za binafsi – yaani kuwalazimisha wasome shule za serikali.

Viongozi hawa wanaona kuwa shule hizi haziwahusu, hawawapeleki watoto wao kwenye shule hizo. Watoto wao ama husoma shule za binafsi za gharama kubwa au zile za nje ya nchi. Hivyo hawaguswi kabisa na uzorotaji wa elimu hapa nchini.

Lengo la sheria kama hiyo ni kwamba viongozi hao wayapate ‘machungu’ ya watoto wao kusoma shule za serikali ili walazimike kuziboresha, na kwa ujumla kuiboresha elimu nchini. Sheria kama hii iko Uingereza, nchi ambayo uchumi wake ni mara milioni moja wa ule wa Tanzania.

Aidha, kuna suala la elimu bure – sera ambayo serikali ya CCM imekuwa ikiitumia mara kadha kisiasa zaidi kuliko uwezekano (practicability) yake.

Mapema mwaka jana (2015) na kwa mara ya pili tangu kujipatia uhuru miaka 54 nyuma yake aliyekuwa rais wa nchi hii Jakaya Kikwete alitangaza kwamba elimu kwa shule za sekondari itakuwa bure na kuweka bayana kwamba elimu hiyo ya bure itaanza mwaka unaofuata (2016), baada ya awamu ya utawala wake.

Mara ya kwanza kutangazwa kwa elimu ya sekondari kuwa bure ilikuwa mwishoni mwa 1963, yaani miaka miwili tangu uhuru, pale Rais Julius Nyerere alipotoa agizo kwamba elimu ya sekondari itakuwa bure – kwa maana kwamba serikali itagharamaia masuala yote ya kielimu katika shule hizo.

Na iliendelea kuwa bure, pamoja na ile elimu ya chuo kikuu kwa takriban miaka 30 iliyofuata – hadi mwanzioni mwa miaka ya 90 pale rais wa awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi aliporudisha karo, ingawa lugha laini ilitumika kutangaza sera hiyo – yaani ‘sera ya kuchangia gharama za elimu.’

Hii ‘elimu bure’ iliyotangazwa na Kikwete ilikuwa ni siasa tu kwani isingeweza kuwa bure kweli na kiuhalisia kama vile ilivyokuwa ‘elimu bure’ ya Mwalimu Nyerere. Enzi zile vifaa vyote vya elimu vilikuwa vinatolewa na serikali – vitabu vya kiada, madaftari, kalamu, vifaa vya maabara na hata vifutio, ukiachilia mbali chakula (kwa shule za bweni) na madawati.