Home Makala CCM INGIZENI SERA YA ‘KUTOFUKUA MAKABURI’ KATIKA ILANI YA UCHAGUZI  

CCM INGIZENI SERA YA ‘KUTOFUKUA MAKABURI’ KATIKA ILANI YA UCHAGUZI  

1905
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Unaweza kutumia msamiati wowote unaopenda kuielezea sera hii isiyofaa – kama vile ‘kuoneana haya,’ ‘huyu ni mwenzetu,’ ‘kulindana,’ au msamiati wa sasa wa ‘kutofukua makaburi’, — athari zake kwa taifa ni zile zile.

Kubwa katika athari hizo ni kuuendeleza uthubutu miongoni mwa wachache katika jamii wenye, au watakaoshika hapo baadaye nyadhifa kubwa zenye maamuzi ya kitaifa, maamuzi ambayo mara kadha yamekuwa yakiligharimu sana taifa hili la watu masikini, badala yake kunufaisha masilahi yao binafsi na, au yale ya familia zao na maswahiba wao

Ni sera ambayo kwa kiasi kikubwa imehusika katika kulifikisha taifa lilipo baada ya zaidi ya nusu karne ya uhuru uliosakwa na kupatikana katika kipindi wananchi wakiwa na matumaini makubwa ya kujikwamua kutoka dimbwi la umasikini, ujinga na maradhi. Hadi leo inaonekana ni kama kwanza ndio tunaanza kuyashughulikia masuala haya.

Lakini sera hii zaidi imekua na kupevuka katika kipindi cha pili cha nusu karne niliyotaja – kiasi hata cha kuwafanya baadhi ya wachache hao kuwa na dharau na kiburi kwa kuwakejeli wananchi kwa maneno yasiyofaa – kama vile “hizo pesa zenyewe ni vijisenti tu”, “ni za kununulia mboga tu”, “ni hela ya ugoro tu”, “ni bora wananchi wale majani kuliko kuacha kununua ndege” – na kadhalika na kadhalika.

Kauli hizi zinaonyesha waliozitoa hawajali umasikini wa wananchi na hasa pale ambapo hazikaripiwi kutoka juu mara moja na hatua kuchukuliwa – kitu kinachoashiria kwamba huenda walipata Baraka zao.

Sote tunakumbuka wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana aliyekuwa mgombea wa chama tawala – CCM – John Magufuli jinsi alivyoibua matumaini makubwa miongoni mwa wananchi kwamba ndiye atakayeshughulikia kikamilifu masuala haya na kurudisha heshima katika nchi.

Ni lazima niseme ukweli kwamba alikuwa na nia njema kutenda aliyoahidi na awali alionyesha ari hiyo hadi kushangaza si Tanzania tu, pengine ulimwengu mzima. Ni kweli alianza kwa kawavunja vidole baadhi ya watendaji wakuu waliokuwa wakiipora nchi kushoto, kulia na katikati tena kwa miaka mingi ingawa bado hatujui mwisho wa kesi husika zilizotinga mahakamani – iwapo itakuwa ni ‘yale yale’ au la – yaani walipeleka watuhumiwa sio, hati za mashitaka kuwa na walakini kiba na kadhalika. Tulishayazoea hayo.

Lakini inawezekana hao wakawa ni mbuzi wa kafara tu hasa ikizingatiwa kwamba waliyafanya yale huku wakubwa zao wakiwatazama tu. Sera hii ya kulindana zaidi imejikita ngazi ya juu kabisa.

Kuhusu hilo sasa hivi polepole ukweli unadhihirika. Kama huko nyuma ilikuwa ni hisia tu miongoni mwa jamii kuwepo kwa kulindana kwa wakubwa ndani ya utawala wa CCM, sasa hivi si hisia tena, bali ndiyo hali halisi, kwani imetamkwa bayana na vingozi wakuu wawili wa nchi katika kipindi cha miaka kumi tu iliyopita.

Mwezi Juni mwaka huu katika hafla moja jijini Dar es Salaam iliyohusu masuala ya ulinzi na usalama, huku rais aliyemtangulia Jakaya Kikwete akiwa karibu yake, rais Magufuli alitamka bayana kwamba hatamgusa mtangulizi wake kuhusu tuhuma zozote za ufisadi alipokuwa madarakani na aendelee na maisha yake ya ustaafu kwa amani kabisa.

Ni vyema nikataja hapa kwamba ‘wanaosamehewa’ hapo ni pamoja na ndugu, jamaa, familia na maswahiba wa huyo mtangulizi wake.

Kama vile ‘hukumu’ ya hatia ya jinai alivyotoa kwa watendaji wakuu wengine (mfano kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam marehemu Wilson Kabwe) ‘hukumu’ ya kutokuwapo kwa jinai kwa Jakaya Kikwete ilishangaza wengi.

Lakini kauli ya Magufuli ilikuja miaka kumi kamili baada ya huyo mtangulizi wake (Kikwete) kutoa kauli kama hiyo hiyo, naye ikimhusu mtangulizi wake Benjamin Mkapa.

Mwezi Juni 2006 Jakaya Kikwete, akiwa rais, akijibu swali lilioulizwa na mwanahabari mmoja katika hotuba yake kwa taifa kupitia mkutano na wahariri wa vyombo vya habari aliouitisha Ikulu alisema si vyema kuwaandama marais waliotangulia kwa makosa waliofanya wakiwa madarakani kwa sababu kufanya hivyo huwafanya baadhi yao kubadilisha katiba za nchi zao na kujiongezea vipindi vya utawala kwa kuondoa ukomo.

Muulizaji swali alitaka maoni ya Rais Kikwete kuhusu ripoti zilizokuwa zikizagaa zikimtuhumu mtangulizi wake, Benjamin Mkapa alijihusisha katika biashara akiwa Ikulu na wasiwasi wake ni kwamba angeweza kutumia nafasi yake kwa kujinufaisha binafsi katika biashara hiyo.

Swali kubwa hapa ni je, kauli hizi za ‘kusameheana’ kwa wakubwa ndiyo mwisho au zitaendelea kwa marais wajao kutoka chama hicho? Jibu ni kwamba zitaendelea tu kwani ndicho kinachokifanya chama hicho kuendelea kuwa madarakani – na hivyo kukifanya kuwa ni chama kikongwe kuliko vyote ambacho bado kiko madarakani Barani Afrika.

Tunashukuru katika nchi yetu hakuna ung’ang’anizi wa madaraka katika ngazi za juu – na utamaduni uliopo ni kwamba marais huachia ngazi kila pale kipindi chake knamalizika kikatiba. Lakini hili la kulindana linaifanya hali hii nzima kutokuwa tofauti sana na ile ya marais wanaoganda madarakani.

Sidhani iwapo kukabidhiana vijiti kwa namna hii ni muafaka sana katika vita dhidi ya ufisadi – vita ambayo Magufuli aliashiria kuingia nayo kwa gia kubwa na ambayo ahadi yake ya majukwaani wakati wa kampeni iliaminiwa na wengi ambao ndiyo walimpa ushindi.

Kwa ujumla hali kama hii ipo pia katika nchi nyingine Barani Afrika ambazo chama kinachotawala ni kile kile ingawa marais huheshimu vipindi vya uongozi. Lakini tofauti ni kwamba viongozi hao hawalitamki sera hii kinagaubaga, tena kwa kujiamini kama ilivyo hapa.

Kwa ujumla ‘sera’ hii inaonyesha kutokuwepo kwa ari katika kupambana na kansa hii ya ufisadi katika safu za juu za uongozi, kansa inayolitafuna Bara la Afrika ambalo lina kila aina ya utajiri.

Kuna baadhi ya watu wamemfananisha Magufuli na Rais wa Rwanda – Paul Kagame – kwa namna yake ya utawala wa nidhamu ya juu kwa watendaji wake na kwa kutovumilia ufisadi katika ngazi zote za utawala. Huo ni mtazamo wa juu juu tu hasa kwa watu ambao hawaijui historia ya Rwanda na hasa jinsi Kagame alivyoingia madarakani.

Tofauti na Magufuli, Kagame hakuingia kidemokrasia, aliishika nchi kijeshi baada ya mauaji yale ya kimbari ya mwaka 1994. Kagame alianza na ‘ubao uliokuwa umefutwa’ (clean slate) hivyo hakuwa na matatizo ya watu wengine waliokuwa madarakani katika utawala uliopita ambao walikuwa wanataka upendeleo fulani, kulindwa kwa madhambi yao ya ufisadi nk – kama jinsi Magufuli yanavyomkuta sasa hivi katika chama chake – CCM.

Sawa, kuna baadhi ya wakuu katika utawala wa chama chake ambao Magufuli anaweza kuwapuuza tu na pengine hata kuwashughulikia vilivyo – kama ambavyo tayari tumeona – lakini kuna wengine hawezi kamwe – la sivyo anaweza akasababisha hali ya sintofahamu katika chama. Na ndiyo maana zinakuja hizi kauli za “kutokuwa tayari kuyafukua makaburi.”

Sasa kama ni hivyo, na ndiyo inaonekana sasa kuwa ni sera kwa marais wanapokabidhiana vijiti, ingelikuwa vyema iwapo hili nalo lingeingizwa kwenye ilani ya kampenui za CCM wakati wa uchaguzi.