Home Makala NJAA YATIKISA MTWARA, SASA MAHINDI HAYASHIKIKI 

NJAA YATIKISA MTWARA, SASA MAHINDI HAYASHIKIKI 

2591
0
SHARE
Mkulima akiweka mahindi kwenye mifuko

NA FLORENCE SANAWA, MTWARA


MKOA wa Mtwara ni moja kati ya mikoa inayojishughulisha na kilimo lakini zao kubwa linalofanywa mkoani hapa ni zao la Korosho.

Mazao mengine hulimwa kwa uchache na hivyo kuufanya mkoa huu kuwa na sifa ya kuagiza mazao hasa ya vyakula nje ya mkoa. Hali hii hufanya bei za mazao ambayo hayalimwi mkoani humu kuwa juu.

Kwa mfano sasa mahindi yamepanda bei hali ambayo imeongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa kipato cha chini ambao ndio wengi wanaotegemea huduma hiyo.

Kutokana na wakulima wengi mkoani Mtwara kukimbilia kilimo cha Mbaazi, mahindi yameendelea kuadimika na suluhisho linabakia kuyaagiza kutoka mikoa ya jirani au kuuza unga uliosagwa tayari.

Rajabu Hamis mfanyabishara soko kuu Mtwara anasema kuwa, unga umepanda bei ambapo kilo 25, sasa zinauzwa shilingi 40,000 badala ya shilingi 27, 000 bei ya zamani.

Anasema kuwa, bei hiyo imepelekea wafanyabishara kuanza kuuza unga kwa shilingi 1700 badalla ya shilling 1200 bei ya zamani, hivyo kufanya unga kuadimika katika masoko mbalimbali mkoani hapa.

Kwa upande wake Hamis Ayubu Mfanyabiashara Soko Kuu, yeye anasema kuwa, mahindi yamekuwa adimu kupatikana sokoni hali ambayo imeongeza bei ya unga.

Anasema kuwa, mahindi yamekuwa yakipatikana katika mikoa mingine mbali na Mtwara kwa kuwa asilimia kubwa ya wakazi wa Mtwara wamekuwa hawalimi mahindi kwa ajili ya chakula na hali ambayo inalazimu wafanyabiashara kuagiza bidhaa hiyo kutoka mikoa ya mbali.

“Unajua huku kwetu kila kitu tunaagiza tu, ndio maana vitu vikipanda bei mikoa mingine kwetu inaongezeka zaidi. Hii inatokana na kutokuwa na kilimo cha biashara ambacho kingeweza kutusaidia sisi tunaangalia usafirishaji zaidi,” anasema Ayubu.

Naye Meneja wa Umoja wa Ushirika Wafanyabiashara soko kuu Mtwara Mkoani hapa Said Namata anasema kuwa, wakulima hao kwa mwaka jana waliuza mbaazi shilingi 3000 hadi 4000 kwa kilo moja, hali iliyowafanya wengi wasilime mahindi.

Aidha, anasema hata mikoa inayolima mahindi nayo imepandisha bei. Mahindi mkoani Ruvuma yanauzwa shilingi 730 hadi 750 kwa kilo moja, huku akisema kwamba asilimia 70 ya mkoa wa Mtwara inategemea mahindi kutoka mkoani humo.

“Pamoja na changamoto hiyo ya kupanda bei, bado Manispaa nao wanachangia bei ya mahindi kupanda kutokana na kodi kubwa zilizopo hivyo ili kufidia kodi yao mfano gari la tani 30, wanataka laki moja hivi kwa stahili tutashindwa kupandisha bei ya unga?” anahoji.

“Sababu nyingine kubwa inayochangia kupanda kwa unga ni kutokana na Manispaa  kuwalipisha magari yaliyobeba mzigo wa mahindi shilingi laki moja kwa gari tani 30 kwa madai kwamba wanaharibu barabara” alisema Namata

Baada ya kuona utabili wa hali ya hewa mwishoni mwa mwaka jana Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Sebastian Waryuba, aliwatahadharisha madiwani wilayani humo kuchukua hatua na kutoa elimu kwa wananchi wao ili kuepukana na janga la njaa.

“Unajua hii wilaya ndio wilaya inayozalisha korosho kwa wingi. Wakazi wake kwa sehemu kubwa wamejikita kwenye zao hilo, ndio maana nilipoona taarifa ya hali ya hewa ilinishtua na hivyo nikaagiza madiwani wakatoe elimu kwa wakulima, ili waweze kulima mazao ya muda mfupi kwa kuwa kitendo cha wakulima kutegemea zao la korosho pekee inaweza kusababisha uhaba wa chakula wilayani humo baada ya kuyapa kisogo mazao mengine,” anasema Waryuba na kuongeza:

“Ifikie wakati wakulima wasione aibu kupanda mihogo. Tumeshuhudia mashamba mengi ya korosho yakiwa na nafasi kubwa kati ya mkorosho na mkorosho. Tutumie nafasi ile kwa kupanda mazao tofauti sehemu ambayo kivuli hakitaweza kuathiri mazao hayo.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Juma Sathma anaeleza kuwa walipokea taarifa ya kuwepo kwa viashiria vya njaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, hali ambayo ilizua mjadala katika kikao cha baraza la madiwani na wakafikia uamuzi wa kuiomba serikali kuwapatia chakula kwa bei nafuu, ili kuwanusuru na balaa la njaa linalowanyemelea wananchi wa eneo hilo.

Sathma anasema kuwa tatizo la njaa limejitokeza katika kata nyingina kwamba kamati maalum imetumwa ili kuhakikisha kuwa inapata taarifa kamili. “Sisi tunaupungufu kidogo kwa baadhi ya kaya hali ambayo inaonyesha kuwa na viashiria vya njaa,” anasema na kuongeza:

“Unajua haya malalamiko nimeona yamekuwa mengi zilikuwa tetesi lakini naona madiwani wanapotoa taarifa inaonekana kuwa tatizo ni kubwa …Sisi tunaiomba serikali utupatie chakula cha dharula tukipata tani 100-200 cha bei nafuu kitaweza kuwasaidia wananchi wetu” anasema Satmah.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Upande wa Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mtwara Amani Lusake anafafanua kuwa  hivi sasa mkoa  una watu ml 1.3 na unahitaji kuwa na tani  460,644.

Anasema kuwa msimu wa mwaka jana mkoa uliweza kuzalisha mazao mara mbili ambapo zaidi ya tani 469,486 huku zao la muhogo lilikuwa ni asilimia 70 kutokana na wakulima mkoani hapa kutolima mahindi mengi ya biashara.

“Mtwara hatuvuni sana mahindi bado bado ni tatizo mara nyingi inapofikia mwezi wa nane hadi 2 na 3 tunakuwa na uhaba mkubwa wa nafaka hususani mahindi. Mara nyingi huwa tuna utaratibu wa kuomba wizara ya kilimo kupitia ‘NFRA’ kutuletea mahindi ya kupunguza makali ya bei ambayo huwa tunayasambaza kwenye halmashauri zetu na kuwapa wakulima.

“Ni kweli hivi sasa kuna uhaba mkubwa wa mahindi hasa ukizingatia ukame uliopo hivi sasa mahindi  yamekuwa machache sana kwenye masoko yetu hivi sasa kilo moja ya unga inauzwa 1300 -1500 tofauti na wakati ambao mahindi yanakuwa mengi unga wa sembe  huuzwa kwa shilingi 1000 wakati unga wa dona huuzwa 800” alisema Lusake.