Home Makala MITANDAO YA KIJAMII INAVYOATHIRI USOMAJI WA MAGAZETI

MITANDAO YA KIJAMII INAVYOATHIRI USOMAJI WA MAGAZETI

1416
0
SHARE
Wenye simu za viganjani habari za matukio huwafikia popote wanapokuwa.

NA HILAL K SUED


KUTOKANA na kasi kubwa ya usafiri wa mawasiliano na upashanaji habari, dunia sasa hivi inazidi kuwa ndogo sana. Matokeo yake ni kubadilika namna tunavyowasiliana, shukrani kwa uwepo wa mitandao ya jamii inayowezeshwa na teknolojia ya intaneti.

Kwani kabla ya hapo watu duniani walikuwa wanakwazwa sana katika kuingiliana (interact) baina yao na hasa kwa watu katika jamii ambao binafsi wanawafahamu mmoja mmoja.

Lakini pamoja na watu wengi kunufaika na maendeleo ya kiteknolojia hii ya mawasiliano, kuna baadhi ya maeneo yaliyokuwapo huko nyuma yameathirika kwa kiasi kikubwa.

Hakuna anayebisha kwamba mitandao ya jamii na intaneti kwa ujumla vimeathiri sana uhai mzima wa sekta ya uchapishaji magazeti. Athari hii imekuwa ikijionyesha katika nchi za Marekani na Ulaya na polepole imeanza kuzagaa nchi nyingine zinazoendelea za Ulimwengu wa Tatu, hasa pale teknolojia hii imekuwa ikiingia na kukua pole pole katika nchi hizo ikiwemo Tanzania.

Ni vigumu kwa nchi yoyote kukwepa athari hii, hata zile nchi za kikomunisti ambazo mamlaka zake zimekuwa zikiweka uthibiti mkubwa katika kupashana habari, bado mipaka ya anga ambamo mawimbi (waves) ya mawasiliano inakuwa na matundu ya kupenya kwa wananchi.

Kabla ya kuzungumzia Tanzania, tuangalie kwa ufupi athari ya mitandao ya jamii dhidi ya tasnia ya uchapishaji magazeti huko Marekani na Ulaya.

Inaelezwa hadi sasa huko Marekani mapato kutokana na mauzo ya magazeti yamekuwa yakiporomoka kwa asilimia 17 kila mwaka kuanzia muongo mmoja uliopita na kufanya magazeti mengi kuwa katika hali mbaya kifedha.

Katika mwaka 2016, pekee makampuni matatu makubwa yanayomiliki magazeti (New York Daily News, San Diego Tribune na Washington Examiner) nchini humo yaliamua kuuza mitambo na mali nyingine zaidi ya 100 ili tu kuokoa vitengo vyao vya utangazaji wa kielektroniki) redio na televisheni.

Na huko Uingereza katika kipindi cha mwaka mmoja hadi kufikia Aprili 2016, mauzo ya kila siku kwa ujumla wake yalipoteza nakala nusu milioni. Mauzo ya nakala za magazeti yanayouzwa Uingereza yaliporomoka kwa wastani wa nakala milioni 7.6 kwa siku kati ya Machi 2015 na Machi 2016.

Magazeti matatu makubwa nchini humo; The Sun, Daily Sport na Daily Record yote yalitangaza kuporomoka kwa mauzo ya zaidi ya asilimia 10 katika kipindi hicho. Gazeti la Mirror lilipata nafuu kidogo, lilianguka kwa asilimia 6.74.

Gazeti la Guardian ndilo liliporomoka vibaya sana miongoni mwa magazeti makubwa ya kila siku hadi kufikia mauzo ya nakala 174,000 nchi nzima, anguko la asilimia 10.23.

Gazeti lililofanya vyema ni The Times ambalo liliporomoka kwa asilimia 0.9 kimauzo.

Kama nilivyotaja huko juu kule Marekani makampuni ya magazeti yenye vitengo vya utangazaji wa kielektroniki yalipata pa kushikia baada ya kuona mauzo ya magazeti yao yakiporomoka kwa kasi. Hali hiyo haiko sana Uingereza ambako makampuni mengi ya uchapishaji magazeti hayana vitengo vya utangazaji wa kielektroniki.

Hapa Tanzania ni dhahiri hali ni mbaya sana ingawa hakuna takwimu za kiutafiti zinazoelezea viwango vya athari ya mitandao ya jamii kwa vyombo vya habari, hususani magazeti. Na kibaya zaidi tangu mwanzo hali hii imechangiwa kwa kutokuwepo kwa usomaji mkubwa wa magazeti miongoni mwa jamii.

Na ni vyema ikatajwa hapa kwamba si mitandao ya jamii pekee imekuwa ikiathiri mauzo ya magazeti yanayochapishwa, bali pia vile vyombo vya habari vya kielektroniki (electronic media) kama vile redio na televisheni navyo pia vimechangia kwa kiasi kikubwa.

Siku hizi takribani vituo vyote vya redio na televisheni wana vipindi vya kuwasomea wasikilizaji/watazamaji wao habari za magazeti yaliyochapishwa siku hiyo, angalau vichwa vya habari.

Lakini kuna baadhi ya magazeti husoma pia habari (news stories) mwanzo mwisho na hata makala pia. Sasa nani atataka tena kuingia gharama na kununua gazeti lilisomwa namna hiyo?

Kupungua kwa wasomaji wa magazeti (na hata vitabu na machapisho mengine) katika jamii kunachangiwa na hali ya kutokuwepo kwa Tabaka la Kati (Middle Class) lililoendelezwa yaani tabaka katika jamii la watu waliosoma wastani (tuseme hadi kidato cha sita) na wenye kipato cha kadiri cha kuwawezesha kukidhi maisha bila matatizo.

Watu katika tabaka hili huwa na uwezo wa kuchunguza na kutafakari masuala ya kisiasa na ya kijamii na hivyo kuwa na ushawishi wa angalau kununua magazeti.

Lakini kuna ukweli pia magazeti ya udaku na yale ya michezo bado yanayo usomaji mkubwa katika jamii, lakini nayo pia hasa yale ya michezo yamekumbwa na athari ya kupoteza wasomaji kutokana na mawasiliano ya intaneti yanayopatikana kwenye simu za viganjani.

Kwa kutofautisha, Tabaka la Juu (Upper Class) linajumuisha wasomi waliobobea, viongozi wa juu wa Serikali na wa vyama vya siasa, matajiri wakubwa na wengine wa kundi hilo na idadi ya hawa katika nchi yetu ni ndogo mno.

Halafu kuna tabaka la chini, wale ambao shughuli yao kubwa ni kujitafutia kipato cha kukidhi milo yao ya kila siku. Hawa siku zote huwa hawana uwezo wa kununua magazeti kabisa.

Lakini wale waliopo wa Tabaka la Kati na ndiyo wenye uwezo wa kununua magazeti wameanza kuhama na kuvutiwa zaidi na simu za viganjani vyenye huduma ya intaneti, Facebook, Instagram na sasa hivi Whatsapp.

Whatsapp ndiyo imefunika hayo mengine kwa sababu watumiaji wana uwezo wa kufanya mawasiliano miongoni mwao na kujibizana papo kwa papo duniani kote. Na kwa kuwa kuna ushindani mkubwa baina ya makampuni ya simu za mkononi basi gharama za vifurushi vimekuwa vikienda chini ingawa Serikali nayo imekuwa inatia mkono wake wa kodi.

Magazeti takribani yote yanaweza kusomwa angalau vichwa vyake vya habari na mmiliki wa simu ya kiganjani, hususani kwa wale wenye simu za kisasa za Smartphone, popote pale alipo. Simu hizi nazo pia bei zake zimekuwa zikiteremka siku hadi siku.

Mbali na mitandao hiyo tajwa, pia kuna blogu mbalimbali katika intaneti ambazo pia huhabarisha na nyingine huweka uwanja (au sebule) ya majadiliano kuhusu suala lolote linaloibuka katika jamii hasa yale masuala yenye kuibua utata. Blogu maarufu inayoongoza kwa kutoa huduma ya aina hii ni ile ya Jamii Forums.

Kwa upande mwingine kumekuwa na hoja kwamba mitandao ya jamii kwa ujumla wake hususani blogu hazichukui nafasi ya tasnia ya habari (journalism) bali tu inaongezea tu safu nyingine ya upashaji habari mbali na zilizokuwepo.

Lakini hoja hii inajikita zaidi kwenye namna wanahabari wanavyofanyakazi hasa katika kukusanya habari zinazoandikwa kwenye magazeti yao. Mitandao inawawezesha wanahabari kukusanya habari na vitu vingine vingi kama vile makala kutoka vyanzo vya watu au taasisi mbalimbali na kuweka katika magazeti yao.

Aidha, mitandao ya jamii inawawezesha wanahabari kupata kwa haraka mashuhuda wa matukio mbalimbali yanayotokea kwani mara nyingi watu huwa na hulka au ari kutuma kupitia mitandao ya Facebook na siku hizi Whatsapp, Twitter kwa marafiki zao kitu gani wamekiona au kukisikia.

 Hii huwasaidia sana wanahabari kuwatafuta mashuhuda ambao ndio walikuwa wa kwanza kushuhudia tukio husika.