Home Makala WAPINZANI WANAPASWA KUPATA TIBA YA KUVUMILIA, KUTATUA MIGOGORO

WAPINZANI WANAPASWA KUPATA TIBA YA KUVUMILIA, KUTATUA MIGOGORO

1507
0
SHARE

NA LAMU KILIMBA


UPINZANI Tanzania ni muhimu lakini kuhusu kushinda nafasi ya urais kwenye uchaguzi halali ni ndoto isiyowezekana, pengine ndoto ya upinzani kwenda magogoni iliyeyuka rasmi Oktoba 25, mwaka 2015.

  1. Wapinzani hawana viongozi wenye kutosha nafasi ya urais (presidential leaders) wenye uwezo wa kupambana na CCM yenye shehena la viongozi na wanachama, wakati upinzani wanategemea mzee Lowassa, Lipumba, Sumaye wenye ukakasi mwingi. CCM kuna viongozi wenye uwezo wa kupokea kofia ya Rais John Magufuli kama Mwigulu Nchemba, January Makamba, Hussein Mwinyi, Kassimu Majaliwa (PM) , Samia Suluhu, Rose Migiro, yaani ni orodha ndefu CCM kuna zaidi ya wanachama 400 wenye uwezo na sifa ya kuvaa kofia ya JPM mwaka 2025. Kuondoka kwa Dk. Slaa na kuyumba kwa mzee Lowassa ni kuyeyuka kwa ndoto ya upinzani na Ikulu.
  2. Wapinzani hawana uwezo wa kuvumiliana kwenye misukosuko ya kisiasa na kujinasua kama ilivyo CCM, wakati CCM wakivuka vihunzi na kusonga mbele migogoro na misukosuko ya upinzani imekuwa sehemu ya kuyumba mpaka kwenye uchaguzi mfano misukosuko ya Zitto Kabwe dhidi ya Chadema ndiyo ilikuwa anguko lake Kigoma na ukanda wake, mgogoro wa Lyatonga Mrema na NCCR-Mageuzi ilikuwa hitimisho la chama hicho ukanda wa Kilimanjaro, Arusha, Manyara na kwingine, mtifuano wa Dk. Slaa na Chadema ilikuwa kidonda kisichopona mpaka sasa hakuna mbadala wake Chadema. Mgogoro wa Prof. Lipumba na CUF imekuwa anguko la CUF uchaguzi mdogo wa hivi karibuni wakati haya yakiwa upinzani CCM hakuna misukosuko yenye kuyumbisha chama kiasi cha kushindwa uchaguzi. Mfano Lyatonga Mrema alileta mnyukano akashindwa chama kikashinda, mzee Lowassa alileta mpasuko CCM ikashinda yeye akashindwa na viongozi wengi kama Steven Wassira, Makongoro Nyerere, Sumaye wamewahi kujaribu kuitikisa CCM mwisho walishindwa wao chama kikashinda. Wapinzani wanapaswa kupata tiba ya kuvumilia na kutatua migogoro ili kwenda ikulu, hili bado ni ndoto.
  3. Wapinzani wanategemea makosa na madhaifu ya CCM kufanya siasa zao kitu kinachoweza kuwapa likizo ya kufanya siasa mfano leo siasa zao ni Paul Makonda na Nape Nnauye, awali ilikuwa bunge ‘live’ na naibu spika, CCM na adhabu za wasaliti, sasa ni Rais na uteuzi badala ya kujikita kwenye ajenda muhimu kuhusu utekelezaji wa bajeti, ajenda muhimu za masilahi wananchi, Watanzania wanategemea kuona mawazo mapya kwa wapinzani kuhusu elimu, huduma za afya, miundombinu, masilahi ya watumishi, sera na mikakati kwenye utalii, kilimo, uvuvi na mengine si kulalamika bila kutoa njia mbadala. Upinzani lazima uje na mawazo mbadala juu ya namna ya kuendesha nchi tofauti na CCM ili Watanzania wapate kushawishika vinginevyo watakuwa wapiga kelele na matukio yanayopotezwa na matukio mapya. Kwenda Magogoni kwa msaada wa madhaifu ya CCM yenye sura ya matukio ya wakati yasiyodumu itabaki ndoto.
  4. Wapinzani wanapigana vita wao kwa wao kuliko kumpa hata CCM, si ajabu ACT Wazalendo kuwa na vita dhidi ya Chadema kuliko hata CCM, CUF kumchapa NCCR-Mageuzi si ajabu, Chadema kumtandika CUF ni kawaida sana Tanzania hata wanapoamua kuungana bado majeraha ya vita ya wao kwa wao hubaki kwenye mioyo ya wanachama na wafuasi wao mfano mzuri uchaguzi wa 2005, Chadema na CUF walipigana bila kujua ni faida kwa CCM, 2010 ndiyo vita ilikolea CUF na NCCR-Mageuzi walipigwa na Chadema mpaka kiasi cha kushutumiana kutumika na CCM kwenye mikutano pengine walishambuliana kuliko hata kuomba kura, 2015 ikawa vita ya ACT Wazalendo dhidi ya Ukawa kwa mazingira haya CCM inapata fursa ya kushinda kirahisi. Ili angalau wapinzani waisogelee Ikulu lazima waungane ni ngumu sana ACT, CUF, NCCR-Mageuzi, ADC, Chauma, TLP, UDP, Chadema, nk kuwa kitu kimoja hata viongozi wa juu wakiamua bado wafuasi wao watagoma hadharani au kwenye nafsi.
  5. Wapinzani hawana watu vijijini, upinzani wamejikita mijini wakati CCM wapo vizuri vijijini na wapo wastani mijini mwisho wa siku kwenye uchaguzi CCM inakusanya kura za kutosha kutoka vijijini inajumlisha na mgawanyo wa kura za mijini mchezo unaisha. Upinzani wanapaswa kulipa deni la kupata wafuasi vijijini kama CCM ndipo waanze vita ya kuelekea Magogoni.
  6. Wapinzani wanacheza ngoma za CCM bila kujitambua, mara nyingi wapinzani Watanzania hujikuta katikati ya midundo ya CCM pasipo kujua mfano kupoteza muda mwingi kujadili marekebisho ya katiba ya CCM 2017, kutumia nguvu kubwa kujadili mchakato wa kupata mgombea wa CCM 2015, kutumia nguvu nyingi kujadili uteuzi wa Rais bora hata mijadala yao ingekuwa katika uelekeo wa kujenga na kuimarisha upinzani lakini wanakuwa watoa mawazo na hisia utadhani wao ni wanachama wa CCM waliojeruhiwa na maamuzi ya CCM. Tabia ya upinzani kupoteza muda mwingi kucheza ngoma za CCM itawachelewesha sana kwenda ikulu hata kuyeyuka ndoto jumla.
  7. Kuwepo viongozi wa upinzani waovu kuliko hata wa CCM, ili Watanzania wachague upinzani wanahitaji kuona tofauti hasa kwenye uadilifu, nidhamu na weledi kutoka kwa viongozi wa upinzani katika mazingira ya viongozi wa upinzani wenye tuhuma za rushwa, ngono, ulevi, ugomvi, ukwepaji kodi, matumizi mabaya ya madaraka si rais kushinda urais. Wabunge, madiwani, wenyeviti, makatibu na viongozi wengine wa upinzani lazima waoneshe tofauti ili kuleta imani kwa Watanzania vinginevyo CCM itatawala karne kadhaa.
  8. Upinzani viongozi na waasisi (waanzilishi) wa chama ni bora kuliko chama, ndani ya vyama vya upinzani ni ngumu kupenyeza mawazo mapya maana kila kitu huhitimishwa na waasisi pamoja na viongozi wa chama mfano bila Mzee Edwin Mtei na Mbowe hakuna lolote linaweza kufanyika Chadema, bila Zitto Kabwe na Prof. Kitila hakuna lolote ACT Wazalendo, bila Mbatia NCCR-Mageuzi haipo, bila Cheyo UDP haipo, bila Rungwe Chauma haipo tazama CUF walijaribu kupenyeza mageuzi ya uongozi bila Prof. Lipumba. Upinzani wanapaswa kuvifanya vyama mali ya wanachama ili kushinda urais hili ni ndoto.
  9. Upinzani upatikanaji wa wagombea huacha mpasuko na majeraha makubwa kuliko CCM, pamoja na uchache wa wagombea wanaojitokeza upinzani kwenye ubunge wa jimbo, viti maalumu, EALA, udiwani, urais, nk bado michakato huacha maumivu makubwa kutokana na njia za mkato kupitisha wagombea mfano ubunge wa EALA wamewapitishwa Masha na Wenje Chadema huku nafasi zikiwa mbili badala ya kutoa fursa kwa vijana wanaojaribu bahati zao kuomba kura bungeni, 2015 wagombea walipendekezwa na viongozi waandamizi huku wanachama wakiachwa midomo wazi majimboni, kupitishwa Edward Lowassa mgombea urais ndio mfano unaoishi.
  10. Wapinzani wanategemea wafuasi kufanya kazi za chama huku CCM ikiwa na wanachama wenye uwezo wakufanya kazi za chama bila hata malipo, si ajabu upinzani kukosa hata mawakala wa kuhesabu kura zao, si ajabu upinzani wakakosa hata wanachama wa kupokea viongozi vijijini, wakati CCM mizizi yake ipo imara upinzani wameimarika matawi pasipo mizizi yenye afya. Wanachama wa CCM wapo sehemu zote penye kazi za CCM, lakini wapinzani hulazimika hata kusafirisha wanachama kwenda mikoani kuwa mawakala wa vyama kwenye uchaguzi achilia mbali hilo bado kura za wanachama ni uhakika kuliko za wafuasi, CCM kuna wanachama watiifu zaidi ya milioni nane sasa hivyo kuna kura za uhakika zaidi ya milioni tano tuseme milioni tatu wasaliti. Upinzani ongezeni wanachama msitegemee kwenda ikulu kwa msaada wa wafuasi wanaobadilika kila dakika.

Kushinda nafasi ya urais kwenye uchaguzi si jambo jepesi, lazima iwepo mipango ya muda mrefu, lazima ziwepo ajenda endelevu, lazima wawepo watu wengi wenye uwezo na ubunifu, lazima uwepo ushirikiano wenye upendo.

CCM ipo imara kuanzia chini mpaka juu wakati upinzani ni kama uyoga juu imara chini dhoofu kiasi cha kuangushwa na viashiria vya upepo kabla hata ya upepo wenyewe kuvuma.

CCM ni taasisi imara anguko lake si leo wala kesho bado kitaendelea kutawala.

lamuelizayo@gmail.com
+255766033331