Home Habari BAJETI 2017/18 WASOMI WAONYA

BAJETI 2017/18 WASOMI WAONYA

1994
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


BUNGE la Bajeti ya mwaka 2017/18 linaendelea na vikao vyake mjini Dodoma, kwa wizara mbalimbali kusoma mwelekeo wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha huku Bajeti Kuu, ikitarajiwa kusomwa Juni 15 mwaka huu.

Bajeti hiyo ambayo inakadiriwa kufikia kiasi cha sh. trilioni 31.6, tayari imeonekana kukosolewa na makundi ya kada mbalimbali kwa hoja kuwa upo uwezekano mkubwa wa kutokutekelezeka.

Hoja ya kutokutekelezeka inanawirishwa na kukwama kwa kiasi kikubwa cha bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17 unaofikia kikomo Julai 30 mwaka huu.

Baadhi ya wasomi wa uchumi wameliambia RAI kuwa ipo haja kwa Serikali kubadilika na kuandaa bajeti yenye namba ndogo inayotekelezeka kuliko inavyofanya sasa, ambapo ina namba kubwa lakini haitekelezeki kutokana na kutegemea fedha nyingi za wafadhili.

Mhadhiri mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humprey Moshi, alisema hakuna cha ajabu kwani hata miaka 15 iliyopita bajeti zote zilizokuwa zikiwasilishwa zilikuwa hazitekelezeki kwa sababu asilimia kubwa ya makusanyo hayafikii kiwango cha bajeti.

Alisema fedha zinazoenda kwenye wizara hazifiki hata asilimia 80.

“Bajeti ya kwanza ya Magufuli ilitupa matumaini baada ya kutenga fedha za maendeleo kwa asilimia 38 kutoka nane hadi 10, bahati mbaya katika utekelezaji hata ile bajeti ya maendeleo imetekelezeka kwa asilimia ndogo. Hivyo tatizo kubwa bajeti inayosomwa leo inakwenda kutekeleza ile ya mwaka jana.

“Tuwe na bajeti ambayo inatekeleza walau kwa asilimia 80, kwa sababu asilimia 100 haiwezekani, hivyo tuwe na bajeti ya kweli kwa kuangalia hali ya uchumi na makusanyo, pia tupunguze utegemezi kwa wafadhili, kwa sababu hii ya kutegemea nayo inaturudisha nyuma. Kenya wanategema asilimia 5 tu kutoka kwa wafadhili wakati sisi ni asilimia 35 hadi 50.

“Ili kupiga hatua Rais anatakiwa kuthubutu na kupitia ile mikataba mibovu ya madini na gesi na kuifanyia marekebisho kwa sababu tumeshapoteza madini mengi ila sasa inabidi kuwa na mikataba ambayo inakubalika, ile ambayo inaruhusu rasilimali za umma lazima iende bungeni ichangiwe, kwa mfano Liberia wameshaanza, haya mambo ya siri ndio rushwa na kujenga ubinafsi, baada ya kutekeleza haya yote ndio tutakuwa na bajeti ya kweli.”

PROF. SEMBOJA

Akifafanua kwa kina kuhusu hofu iliyopo juu ya kukwama kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18, Mhadhiri wa Chuo Cha Dar es Salaam, Profesa Hadji Semboja, alisema licha ya kwamba namba kwenye hesabu ni zilezile ila huwa zinaleta tafsiri mbalimbali kwa mwanataaluma.

“Bajeti ya mwaka jana na mwaka huu kuna mkazo wa maendeleo na kwa namna Rais alivyo amekuwa na mkazo kwenye uwekezaji wa miundombinu, mwenyewe anajua kusimamia, kufuatilia na kufanya tathmini. Katika bajeti, moja ya mambo muhimu ni hayo.

“Kosa ambalo lilitokea mwaka jana lilifanywa na waziri mwenyewe, naona iwapo angeelewa taaluma ya bajeti asingefanyaje vile. Kwanza bajeti ya kawaida ni tofauti na bajeti ya maendeleo, kwani ya kawaida ukisema siku wiki, mwaka inakua vilevile kwa sababu watu wanalipwa kwa mwezi, posho na kusafiri, ilivyopangwa ndivyo ilivyotekelezwa, tofauti na bajeti ya maendeleo. Kwa mfano ujenzi wa reli una awamu nne kubwa, kwanza usanifu na maandalizi mbalimbali, huwa hela haihitajiki nyingi sana, ya pili ndipo unapoanza kuhitaji fedha kama asilimia 30 hadi 40, awamu ya tatu ndio unanunua mashine kubwa kama treni, vichwa na ya nne ambayo ni ya mwisho ni matumizi madogo ya kumalizia mradi.

“Sasa fedha zilizotumika ni sawa na fedha zilizotengwa kwa mradi, lakini sio kwamba fedha zote zilizowekwa zilitakiwa kutumika mara moja, kuna tafsiri potofu, kuna tatizo la Watanzania kuishi kama ‘mr. zero balance’, kwamba chochote tulichopanga mwaka huu lazima kitumike chote. Hapana!

“Lazima tujifunze kuwa kuna bajeti ya maendeleo ambayo kuna fedha mbazo zitapangwa mwaka huu zitatumika mwaka kesho, zinatakiwa ziwe ‘saved’ kwa matumizi ya mwaka kesho, kwa hiyo si kosa la Watanzania kutafsiri, ni kosa la Waziri,  ameshindwa kujieleza. Kwamba kile kilichokuwa kinahitaji kwa matumizi ya maendeleo ni sahihi kuna ambacho kimepangwa si lazima kiwepo leo.

“Hata hivyo, hatujazoea kufanya vitu vya maendeleo, tulizoea kuwa kilichopangwa lazima kitumike chote. Hatuwezi kugawa treni leo wakati hujaweka reli.

“Ninachoona ni kwamba miradi hii tutatekeleza na hakuna haja ya kukosa fedha za kutekeleza. Hatuna sababu ya kukosa fedha za maendeleo kwenye ile miradi,”alisema Prof Semboja

  1. MPANGO

Kwa mujibu wa Dk. Mpango bajeti ya mwaka huu 2017/18,  fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka trillion 11.8 mwaka 2016/2017 mpaka kufikia shilingi trillion 11.9 kwa mwaka huu Mpya wa bajeti 2017/2018 ambapo ni sawa na wastani wa asilimia 38 ya bajeti yote tarajiwa.

Dk. Mpango alibainisha vikwazo vilivyochangia kukwama kwa bajeti inayoishia mwezi Juni kuwa ni mwamko mdogo wa kulipa kodi, matumizi hafifu ya mashine za risisti za kielektroniki (EFDs) na kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje.

Sababu nyingine ni majadiliano ya muda mrefu yaliyosababisha kuchelewa kupatikana fedha za washirika wa maendeleo.

Akiwasilisha bajeti pendekezwa Dk. Mpango alisema hadi kufikia Februari 2017, makusanyo yote ya Serikali yalikuwa Sh trilioni 15.37 sawa na asilimia 79 ya malengo, kati yake mikopo ya ndani Sh trilioni 3.5 sawa na asilimia 78 ya malengo, misaada na mikopo nafuu Sh trilioni 1.25 sawa na asilimia 40 ya malengo.

Dk. Mpango alisema mikopo ya kibiashara kutoka vyanzo za nje ilitarajiwa kuwa Sh trilioni 2.1, lakini hadi sasa hazijapatikana.

Kusuasua huko kumeelezwa kusababisha hofu kwa Serikali ambayo baadhi ya wachumi pia wameeleza kuwa hata bajeti ya mwaka huu 2017/18 haitakuwa na jipya kutokana na wasaidizi wa Rais ambao ni mawaziri na makatibu wakuu kushindwa kusimamia weledi wa taaluma zao.

MATUMIZI
Katika mwaka 2017/18, serikali imepanga kutumia jumla ya Sh. trilioni 32.946 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati yake, Sh. trilioni 19.782 zitatengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambapo Sh. trilioni 7.206 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi za umma na Sh. trilioni 9.723 ni kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa lililoiva.

Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh. trilioni 13.164, sawa na asilimia 40 ya bajeti yote, ambapo fedha za ndani ni Sh. trilioni 9.960, sawa na asilimia 76.

SURA YA BAJETI
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 inatarajiwa kuwa jumla ya Sh. trilioni 32 zitakazokusanywa na kutumika katika kipindi hicho.

Waziri huyo alieleza kuwa mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 20.872 sawa na asilimia 63 ya mahitaji yote. Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh. trilioni 18.097 sawa na asilimia 87 ya mapato ya ndani.

Mapato yasiyo ya kodi Sh. trilioni 2.022 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh. bilioni 753.3.

Serikali inategemea kukopa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 900 (Sh. Sh. trilioni 2.080 kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara na Sh. trilioni 4.434 zinazotarajiwa kupatikana kutokana na mikopo ya ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva. Sh trilioni 1.859, sawa na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Pia washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. trilioni 3.7. Kati yake, Sh. bilioni 496.3 ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti (GBS), Sh. trilioni 2.821 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh. bilioni 382.4 ni misaada na mikopo nafuu ya mifuko ya pamoja ya kisekta.

 

RAIS KENYATA ARUSHA DONGO

Katika mazungumzo yake hivi karibuni nchini Kenya, Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta, alizitupia dongo Bajeti ya Tanzania na Uganda kwa kudai kuwa zinategemea fedha za wafadhili katika kushughulikia masuala ya afya na elimu, huku bajeti ya nchi yake ikijitegemea.

Pamoja na mambo mengine Rais Kenyatta alisema amefanya mengi na anataka kuona wataalamu wanafanya kazi zao.

Nataka wataalamu wafanye kazi zao na kwa kufanya hivyo Kenya ndio nchi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambayo bajeti yake ya matumizi ya kawaida kwa asilimia 100 inatokana na makusanyo ya ndani na si midaada ya wafadhili.

“Tunawalipa waalimu wetu, tunawalipa watoa huduma za afya, tunawalipa watumishi wetu, tofauti na Tanzania na Uganda ambazo karibu asilimia 40 ya bajeti zao hugharamiwa na wafadhili.

“Sisi hapa hakuna shilingi ya Mzungu inayowalipa walimu katika Kenya hii. Ni kitu ambacho tunajivunia kwa sababu tuna watu sahihi tumewaweka kufanya kazi sahihi.” Alisema Rais Kenyatta.