Home Makala WAZIRI MKUU TATIZO NI BANDARI, BARABARA ZETU MBOVU

WAZIRI MKUU TATIZO NI BANDARI, BARABARA ZETU MBOVU

734
0
SHARE
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika chumba cha nahodha wa moja kati ya meli mbili zilizonunuliwa na serikali ili zihudumie wananchi katika ziwa Nyasa

JULAI 29 mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua mradi wa meli za mizigo na abiria katika Bandari ya Itungi, iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya. Meli hizo  Mv Njombe na Mv. Ruvuma zina uwezo wa kubeba jumla ya tani 200 za mizigo na abiria 200 mabazo zitafanya shughuli zake ndani ya Ziwa Nyasa.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) bandari ilikuwa ni mojawapo ya vipaumbele vitano vya kimkakati vyenye lengo la kufungua fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuwanufaisha wengi.

Binafsi ninaunga mkono juhudi za kuongezwa meli mpya, kwa sababu ninao uzoefu katika ziwa Nyasa na nimelitumia katika shughuli zangu zote za maisha. Kwahiyo ninafahamu adha kubwa iliyozikabili meli zote mbili zilizokuwa zikitumika awali, yaani Mv Iringa na Mv. Songea.

Sitarudi nyuma kuelezea matukio ambayo niliyashuhudia nikiwa safarini, kwa sababu sikusudii kutafuta mchawi wa makosa ya kale ikiwa tunaweza kurekebisha matatizo.

Uzinduzi wa Waziri mkuu Kassim Majaliwa umenivutia na kusikitisha. Kinachosikitisha ni ucheleweshwa wa mradi wenyewe pamoja na changamoto nyingine inayoikabili Halimashauri ya Wilaya ya Nyasa pamoja na mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Mkoa wa Mbeya unazo bandari mbili tu, Itungi na Kiwira ambazo safari za meli hizo huanzia. Kwa mkoa wa Njombe unazo bandari za Manda na Lupingu zilizopo katika wilaya ya Ludewa. Mkoa wa Ruvuma ndiyo wenye sehemu kubwa ya bandari zitakazotumiwa na meli hizo. Kuna bandari za Ndumbi, Lundu, Nkili, Njambe, Liuli na Mbamba Bay.  Hapo ndipo tatizo linaanzisha.

Ni hivi! Mojawapo ya changamoto kubwa inayoikabili Halmashauri ya Nyasa ni ujenzi wa gati katika bandari zake zote. Mathalani, bandari ya Ndumbi imepewa umuhimu mkubwa kutokana na upatikanaji wa makaa ya mawe.

Mji wa Ndumbi unasadikika (haijathibitishwa kitaalamu) umezungukwa na makaa ya mawe mengine ambayo hayajachimbwa. Jambo la pili ni kutokamilika kwa ujenzi wa gati lilipo katika bandari hiyo.

Niliona kwa macho yangu namna ambavyo makaa ya mawe yalivyorundikwa bandarini hapo. Pili, Gati lenyewe halikuwa limekamilika, jambo ambalo nilifahamishwa kuwa linakwaza shughuli za usafirishaji wake.

Tatu, kutokuwepo kwa majengo yanayohifadhi mizigo (Godown) ni kikwazo kingine. Inafahamima bandari nyingi katika ziwa Nyasa hazina majengo ya kutosha ambayo yanahifadhi abiria. Zipo sehemu ya kuhifadhi mizigo pekee lakini usalama na mali za abiria bado haueleweki.

Tuchukue mfano, bandari ya Ndumbi ambayo bila hata kufanya utafiti wa kitaalamu inafahamika kuwa kiunganishi kikubwa cha ukuaji wa uchumi kati ya wilaya ya Nyasa, Mbinga na Songea. Tatizo kubwa lilipo ni ubovu wa barabara.

Kwahiyo changamoto mbili zipo katika bandari moja, Barabara ya Mbinga-Lituhi ni mbovu, huku makaa ya mawe yakiwa bidhaa muhimu inayohitajika kuinua uchumi wa wilaya ya Nyasa na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Nini kifanyike hapo! Kwanza kukamilishwa kwa ujenzi wa gati la bandari ya Ndumbi ni jambo muhimu zaidi. Tunafahamu historia ya eneo hilo, ni zuri, linavutia kiuwekezaji wa bandari licha ya kina kifupi kilichopo.

Pili, ujenzi wa barabara ya kutoka Ndumbi kwenda Lituhi kisha Songea ni jambo nyeti ambalo linaweza kuondoa vikwazo vya uwekezaji. Tunafahamu mawaziri kadhaa wamewahi kuzuru eneo hilo. waziri wa mazingira, Januari Makambda, Naibu waziri wa uchumi Edwin Ngonyani na aliyekuwa waziri wa nishati na madini, Profesa Muhongo. Ubovu wa barabara katika maeneo yote yanayotumiwa na wawekezaji wanaochimba makaa ya mawe umechangia kudhoofisha kasi ya maendeleo ya eneo hilo. inachukua saa takribani 7 kutoka Songea kwenda Lituhi hadi Ndumbi, mahali ambapo pangejengwa barabara nzuri angalau ya kiwango cha kokoto ingepunguza matatizo mengi ya miundo mbinu. Ardhi ya kutoka eneo la Kitai ambapo ni njia panda kati ya Songea, Mbinga na Nyasa ni tambarare ambayo inarahisisha utengenezwa wake.

Sababu!

Wilaya ya Nyasa inazo barabara kuu tatu tu. Barabara ya Songea kwenda Lituhi, Barabara ya Lituhi kwenda Mbamba Bay na barabara ya Mbamba Bay kwenda Songea. Njia hizi zikitengenezwa zitanufaisha zaidi serikali na wananchi wake kwa kiwango kikubwa. Aidha, inachochea ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Malawi pamoja na Tanzania na Msumbiji.

Kwa mingi biashara ya Malawi na Tanzania kupitia ziwa Nyasa inadhoofishwa na usafiri mbovu. Mwanzoni mwa miaka 2000 kulikuwa na meli kama MV Ilala kutoka Malawi pamoja na nyingine ambazo zilichochea biashara ya pande mbili. Bahati mbaya Malawi walitukimbia sababu ya miundombinu mibovu.

Sasa basi, kwa vyovyote kuletwa kwa meli mpya maana yake kunapanua shughuli za kiuchumi, lakini zinakutana na kikwazo kingine cha ulinzi wa raia na mali pamoja na ubovu wa barabara.

Baruapepe; mawazoni15@gmail.com