Home Maoni TUNAPINGA UDHALILISHAJI WA NAMNA HII

TUNAPINGA UDHALILISHAJI WA NAMNA HII

695
0
SHARE

Walipokula kiapo cha uadilifu baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli, tulitegemea kwamba watakuwa mfano wa kuigwa. Hawa ni wateule karibu wote kuanzia wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya na mikoa — kwa wastani ni vijana.

Lakini mambo yanavyoonekana sasa ni kwamba baadhi yao wamekuwa wateule wasiojua mipaka ya kazi zao — wababe, wasumbufu, wakandamizaji na wadhalilishaji wa wananchi.

Tumeshuhudia vituko vyao kadha — wengine badala ya kufanya kazi ya uongozi (utawala), wamejikita zaidi kwenye mambo ya kisiasa, ili waonekane kwamba wanakisaidia chama tawala kuvunja ngome za vyama vingine.

Wengine kazi yao ni kutoa amri kwa Polisi, kuwakamata viongozi wa vyama vingine na kuwaweka ndani kwa visingizio dhaifu!

Lakini matukio mawili ya hivi karibuni ya wakuu wa wilaya wawili — Glassius Byakamwa wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, na Mkuu wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Simon Odunga, hakika yametia fora.

Byakamwa alimsweka lupango Mwalimu Erasto Mhagama wa Shule ya Sekondari Lerai, baada ya kukataa amri ya kupiga ‘push up’ — eti kwa sababu alishindwa kujibu maswali yaliyoulizwa na DC Byakamwa.

DC anafanya ziara kwenye shule, halafu ananza kuwauliza walimu mambo yasiyohusiana na taaluma yao kama vile wataje jinal lae (la DC). Kwa ujumla siyo lazima walimu wote wajue kirefu cha IGP, CDF, au CUF na CAF. Haiwaongezei shibe, maslahi au maarifa na umahiri wa kufundisha.

Kituko cha DC wa Chemba, cha kumcharaza fimbo na kumpiga na kumjeruhi Chindika Pingwa (57) wa kijiji cha Kambi ya Nyasa, eti kwa sababu mtoto wake alivunja kioo cha gari la DC (STL 669) wakati akicheza na wenzake, kinatutia kichefuchefu.

DC Odunga hakutumia busara, wala kuheshimu watu wa umri mkubwa. Aidha mzee huyo hakuhusika na tukio au kuwatuma watoto kucheza sehemu lilikokuwa limeegshwa gari hilo.

Katika matukio yote mawili, waliodhalilishwa na kuumizwa, tunawashauri watafute mawakili na wawashitaki binafsi wakuu wa wilaya hao na kuwadai fidia. Hakuna sheria inayompa madaraka DC yeyote kuchukua sheria mkononi na kuonea watu wasio na hatia.

Lakini zaidi ya hayo, mamlaka teuzi iwavue kofia ya u-DC, ili wakasimame mahakamani kwa majina yao na ikithibitishwa walitenda makosa hayo, sheria ichukuwe mkondo wake kutokana na madai ya mlalamikaji.

Wateule wa Rais Mgufuli, katika baadhi ya maeneo, wanadhani kuwazuia viongozi wa vyama pinzani, kuwadhalilisha, kuwafungulia kesi kila uchao, wanamjenga rais na chama chake.

Kinyume chake kinaweza kuwa kweli — kama tulivyowahi kusema huko nyuma — wanajenga chuki miongoni mwa wananchi na pamoja na mazuri ambayo Serikali hii inayafanya, watu wanaweza wakakipa kisogo chama na kumweka pabaya Rais Magufuli.

Tunamshauri Rais Magufuli kuzipitia upya ripoti za watendaji — hasa wale waliopewa rungu la kumweka mtu ndani kwa saa 48. Aidha, Rais awakemee polisi ambao badala ya kushughulika na wahalifu katika maeneo yao —wanawawinda viongozi wa upinzani ili waonekane wanatekeleza vizuri majukumu yao.

Huu ni udhaifu mkubwa katika Jeshi la Polisi ambao kazi yao kuu ni kulinda usalama wa raia na mali zao.