Home Makala MWAKYEMBE: TUSIPOJIPANGA SASA KUTUMIA FURSA, WAGENI WATAZITUMIA

MWAKYEMBE: TUSIPOJIPANGA SASA KUTUMIA FURSA, WAGENI WATAZITUMIA

1046
0
SHARE

NA AMINA OMARI, TANGA

MKOA wa Tanga ni mojawapo ya mikoa iliyokuwa imesheheni viwanda na fursa mbalimbali za kiuwekezaji katia miaka ya 1990. Kutokana na dhana ya ubinafsishaji iliyoanzishwa katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, mkoa huo uliporomoka na kubakia na viwanda mfu.

Hata hivyo, Mungu hamtupi mja wake na kwani sasa mkoa huo umeanza kufufuka upya hasa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kuingia madarakani.

Licha ya kuchagizwa na kaulimbiu ya Tanzania ya Viwanda, ujio wa mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka nchini Uganda hadi eneo la Chongoleani jijini humo ni chanzo kingine kilichoonesha namna Mkoa wa Tanga utaanza kufufuka na kuwa nguzo kuu ya uchumi wa Taifa.

Mradi huo wa bomba la mafuta umeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuvutia wawekezaji mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi kuwekeza katika maeneo yaliyoko mkoani humo.

Hali hiyo imeulazimu uongozi wa mkoa kuandaa mkutano wa Jukwaa la biashara ambalo linalenga katika kutangaza fursa za kiuchumi, kiuwekezaji pamoja na biashara zilizoko katika mkoa huo.

Akizungumzia umuhimu wa kutumia fursa zilizopo katika mkoa huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amewataka wakazi na  wafanyabiashara wa mkoa huo kuanza mapema kuzitumia fursa zilizopo katika mkoa huo kabla ya wageni hawajazitumia na kuwaacha wenyeji kuwa watazamaji.

Anasema Watanzania wana fursa nyingi katika maeneo yao ambayo kama wataweza kuzitumia vizuri wanaweza kujikwamua kiuchumi.

“Niwaambie  hakuna muda wa kupoteza kwa wakazi wa Tanga kutokana na rasilimali, fursa zilizowazunguka ikiwemo uvuvi, kilimo pamoja na bomba la mafuta ambalo limeshazinduliwa pamoja fursa za utalii,” anasema.

Anasema Watanzania wana tabia  ya kukurupuka wakati ambapo mradi umekwishaanza, hivyo  tunakuwa tunashindwa namna bora ya kujipanga toka awali na kubakia kuwa wasindikizaji tu.

“Tusipojipanga leo na kuzitumia vizuri hizi fursa nyingi zilizopo, basi tujue fursa hizi zitatumiwa na wageni ili hali Watanzania tuna uwezo.

“Sitashangaa wataalamu wa ujenzi wa bomba wote wakawa wanaishi mjini Mombasa nchini Kenya na wakawa wanakuja hapa Tanga kufanya kazi pekee na jioni wanaondoka kurudi kulala nchi jirani,” anasema Dk. Mwakyembe.

Anasema wataweza kutumia uwanja wetu wa ndege kwa ajili ya kuleta ndege zao za kukodi na kuacha za kwetu zikiwa zipo tuu na hata vivutio vyetu vya utalii hawataweza kwenda bali watakwenda vilivyoko nchi ya jirani.

“Huku vivutio vya kwetu wakiviacha kutokana na kushindwa kujitangaza au kutokana na kutokuwepo kwa maandalizi mazuri ya kuwezesha kufika huko,” anasema Waziri huyo.

Aidha, Mwakyembe anawasisitiza Watanzania kuwekeza katika biashara ya huduma na viwanda vya uzalishaji bidhaa ndogondogo na za kati  ambazo zitakuwa zikihudumia katika ujenzi wa miradi mbalimbali hususani wakati wa ujenzi wa  bomba la mafuta kutoka Hoima-Uganda hadi Chongoleani-Tanga.

“Juzi kuna mtu alinifuata kutoka nchi jirani sitamtaja, alitaka kujua taarifa za mradi huo hasa katika upande wa huduma ili aweze kushawishi baadhi ya makampuni ili wafanyakazi wao wawe wanaishi katika hoteli yake ambayo ipo Mombasa.

“Hivyo mnaona namna wenzetu walivyokuwa na haraka ya kuchangamkia fursa hata pale wanapozikosa wako tayari hata kuvuka nchi kwa ajili ya kufanya uwekezaji na kuimarisha uchumi wao,” anasema.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, anasema ni muda mwafaka kwa wawekezaji kukimbilia kuwekeza mkoani hapa kutokana na Serikali kutenga maeneo mengi ya uwekezaji katika halmashauri zote sambamba na kupatikana kwa malighafi.

Anasema kwa sasa wapo kwenye jitihada za kuboresha bandari, kupanua uwanja wa ndege na ujenzi wa barabara za ndani ya mkoa ili kuimarisha miundombinu hiyo iweze kupitika kwa muda wote.

“Tuna imani kama tukiimarisha miundombinu kama barabara na bandari, tutaweza kuvutia wawekezaji kuweza kuja kufanya uwekezaji katika maeneo yetu kwa urahisi.

“Tayari tuna maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda kama vya matunda, bidhaa zitokanazo na kilimo pamoja na madini katika maeneo ya wilayani na mijini,” anasema RC Shigela.

Anasema tayari wameshaanza ushawishi kwa wafanyabiashara hususani  wenye mahoteli kuangalia namna ya kuboresha utoaji wa huduma ili ziweze kuendana na hadhi ya nyota tano.

Hata hivyo, anataja baadhi ya uwekezaji unaotarajiwa kufanywa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda kipya cha saruji, ujenzi wa hoteli, kilimo, upanuzi wa uwanja wa ndege na uimarishaji wa miundombinu ya reli na bandari.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Sabasaba Moshingi, anasema katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kufufua viwanda nchini, Benki hiyo ipo tayari kuwasaidia mikopo yenye masharti nafuu wafanyabiashara ili kuweza kufikia mafanikio yao.

Anasema benki hiyo inatoa huduma za mikopo kwa wafanyabiashara wa kada zote ili waweze kukuza mitaji yao na kutanua wigo wa biashara zao.

“TPB ni benki ya kizalendo iliyojikita katika kumsaidia Mtanzania wa kawaida ili aweze kuinua shughuli zake za kiuchumi na hatimaye kukuza uchumi wa nchi yetu kwa ujumla,” anasema Moshingi.

Vilevile amesema  katika kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda, ni vema vijana wakajengewa uwezo wa kiuchumi, hivyo benki hiyo ipo tayari kuhakikisha wanawasaidia vijana kuweza kukamata fursa zilizopo za  kiuchumi.