Home Makala BOMBA LA MAFUTA TANGA: FURSA MPYA YA KUHUISHA UCHUMI WA MKOA (3)

BOMBA LA MAFUTA TANGA: FURSA MPYA YA KUHUISHA UCHUMI WA MKOA (3)

1804
0
SHARE

 

NA SUSAN UHINGA

MKOA wa Tanga ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania. Uko Kaskazini Mashariki mwa nchi, ukipakana na Kenya upande wa Kaskazini, Bahari Hindi upande wa mashariki, na mikoa ya Morogoro, Manyara na Kilimanjaro.

Mpaka wake kwa upande wa kusini unafuata mto Mligaji kuutenganisha na Mkoa wa Pwani, makao makuu ya mkoa huo yapo mjini Tanga.

Tanga ni kati ya mikoa midogo ya Tanzania yenye msongamano mkubwa wa wakazi ndani ya eneo lake.

Msongamano wa watu hasa wanaojishughulisha na shughuli halali za kujiongezea kipato, unatajwa kuwa  mkubwa zaidi katika Wilaya ya Lushoto.

Lushoto imekumbwa na hali hiyo kutokana na eneo lake kubwa kutawaliwa na ardhi yenye rutuba nzuri.

Kwa ujumla Tanga ina ukubwa wa eneo la km² 27,348 ambalo linaunganisha sehemu za pwani pamoja na milima ya ndani kama Usambara.

Katika eneo lote hilo la ukubwa, ni km² 17,000 tu ndio zinafaa kwa shughuli za kilimo.

Tanga ina jumla ya wilaya nane ambazo ni Handeni, Kilindi, Korogwe, Lushoto, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga Mjini.

Kwa jumla hali ya hewa ni joto lenye unyevu. Mathalani Wilaya ya Handeni, kwa kiasi kikubwa imetawaliwa na joto kavu zaidi, wakati Wilaya ya Lushoto na maeneo mengine yaliyozungukwa na  Milima ya Usambara hakuna joto sana.

Kati ya Desemba  hadi Machi, halijoto mkoani humu hufikia sentigredi 30-32 mchana na 26-29 usiku.

Wakati wa Mei hadi Oktoba halijoto inapoa na kufikia sentigredi 23-28 mchana na 20-24 usiku, huku unyevu ukiwa  juu kati ya asilimia 65 na asilimia 100.

Maeneo mengi ya mkoa hupokea angalau milimita 750 za mvua kwa mwaka au zaidi, kwa upande wa Pwani hali huwa tofauti kidogo.

Huko hali ya mvua huongezeka na kufikia  takriban milimita 1,100 hadi 1,400 ikipungua sehemu za ndani, isipokuwa milima ya Usambara ambako mvua inaweza kuzidi milimita 2000 kwa mwaka.

WAKAZI

Mwaka 2012 wakazi waliohesabiwa katika sensa walikuwa 2,045,205.

Makabila makubwa mkoani Tanga ni Wasambaa, Wazigua, Wabondei na Wadigo. Aidha, yapo makabila kadhaa yaliyoweka maskani yake Tanga kutokana na kupakana na mkoa huo.

Makabila hayo ni Wapare, Wataita, Wambugu, Wasegeju na Wanago, lakini pia ipo jamii ya wenye asili ya Oman, jamii hii ina historia ndefu ambayo si rahisi kuijadili kwenye makala hii inayohusu umuhimu wa Bomba la Mafuta ghafi.

Wasambaa ndio kabila kubwa lililoko katika milima ya Usambara, Muheza, Korogwe na Lushoto. Kwa jumla kabila hilo ndilo asilimia 40 ya wakazi wote wa mkoa.

Wazigua ni kabila kubwa huko Handeni na sehemu za Korogwe na Pangani. Wabondei wako hasa Muheza na sehemu za Pangani. Wadigo ndio wengi Tanga Mjini na sehemu za Muheza.

ELIMU

Ingawa Tanga ndio inatajwa kuwa kitovu cha elimu tangu karne hizo, lakini ukweli ni kwamba katika mkoa huu elimu inahitaji kuboreshwa zaidi, hasa maeneo ya vijijini, maana watu wengi wa mkoa huu bado wametawaliwa na imani za kimila, hali hiyo huwafanya kushindwa kuendelea na shughuli za kimaendeleo katika Taifa la Tanzania.

Pamoja na baraka kadha wa kadha ilizobarikiwa mkoa huo, bado wakazi wake wengi ni masikini, mathalani Wilaya ya Handeni; kuna machimbo ya madini, lakini  elimu ipo nyuma sana.

UCHUMI

Kabla ya kukaribishwa kwa sera ya ubinafsishaji miongo miwili iliyopita, uchumi wa Tanga ulikuwa imara, ajira zilikuwa za kutosha, viwanda viliifanya Tanga ing’are, bahati mbaya hali sasa ni tofauti.

Tanga ya leo imechoka, haina nuru tena, imekosa matumaini ya kurejea kuwa moja ya mikoa inayochangia pakubwa bajeti ya Taifa.

Kwa sasa wakazi wengi wa mkoa huu hutegemea kilimo cha kubahatisha kinachosubiri zaidi mvua za msimu, ufugaji na uvuvi.

Mazao ya chakula hasa ni mahindi, muhogo, ndizi, maharagwe na mpunga, mazao ya biashara ni katani, pamba, kahawa, chai, nazi, tumbaku na korosho.

Mifugo inayopatikana Tanga ni ng’ombe, mbuzi, kondoo pamoja na kuku.

Katani ilikuwa zao la biashara hasa kwa ajili ya Tanga tangu kuingizwa kutoka Mexico zama za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Zao hili hulimwa kote mkoani isipokuwa Lushoto, eneo kubwa linalolima katani ni  Muheza na Korogwe kwenye mashamba makubwa. Mashamba hayo yalikuwa ya walowezi, yakataifishwa baada ya uhuru. Tangu kuanguka kwa sekta ya umma yamebinafsishwa tena siku hizi, zao la katani linategemea sana soko la dunia, umuhimu wake ulirudi nyuma tangu miaka ya 1960.

Hali imekuwa hivyo kwa miaka mingi sasa, huenda mkombozi wa uchumi wa Tanga sasa amepatikana.

Ujio wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga –Tanzania unaweza kusaidia kuhuisha uchumi uliokufa na kuelekea kuoza.

VIWANDA

Tanga ilikuwa na viwanda vingi kiasi katika miaka ya 1960 na 1970, lakini sasa karibu vyote vimekwama kutokana na siasa ya Ujamaa na uchumi wake ulioiga mfumo wa nchi za kisoshalisti.

Viwanda vichache vilivyobaki havizalishi mali kulingana na uwezo wao. Kilichobaki hasa ni kiwanda cha saruji Tanga.

Utalii umeanza kupanuka kidogo, hasa katika eneo la Pangani, Mapango ya Amboni na kituo cha Makumbusho ya Urithi Tanga.

Ili kuendelea kuwapa wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla ufahamu wa fursa ya ujio wa bomba la mafuta ghafi, tutaendelea kuleta mfululizo wa makala zenye kuainisha na kufafanua masuala mbalimbali yanayohusiana na mradi huo mkubwa barani Afrika.

0767414185