Home Makala SIASA ZA DHULUMA ZISIHARIBU SIFA YA TAIFA LETU

SIASA ZA DHULUMA ZISIHARIBU SIFA YA TAIFA LETU

1227
0
SHARE

Na FARAJA MASINDE

NCHI ya Tanzania imejijengea heshima kubwa kwa kuwa kitovu cha amani na utulivu miongoni mwa mataifa ya Afrika kwa kipindi kirefu sasa.

Kuwapo kwa amani katika Taifa la Tanzania ambalo lilipata uhuru wake mwaka 1961, kumekuwa kukichagizwa na mambo mengi, ikiwamo  kuwapo kwa viongozi makini ambao wamekuwa ni waumini wa siasa safi, zisizo na chembe yoyote ya chuki, pamoja na mambo mengine kama vile kutokukumbatia ukabila usio na tija.

Misingi hiyo imara ambayo iliwekwa tangu uongozi wa awamu ya kwanza chini ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere imeendelea kuwa nguzo imara ambayo ilishawishi hata Mataifa mengine kuja kujifunza, Tanzania namna ya kuwa na mshikamano kama taifa pasi na kuwapo kwa machafuko au siasa za visasi na chuki baina ya vyama vya siasa.

Hata hivyo, kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwapo na wingu zito ambalo limekuwa likijaribu kutanda kwenye amani ya Tanzania kupitia taswira ya siasa, mambo ambayo awali yalikuwa ni nadra sana kuonekana kutokana na uungwana ambao umekuwapo kwa kipindi kirefu baina ya vyama vya siasa na Serikali.

Kwa namna hali ilivyo ni wazi kuwa kumeanza kuwa na hali ya wasiwasi wa kiusalama kufuatia kuwapo kwa matukio ambayo mengine yanafikirisha na kuacha maswali mazito kwenye kichwa cha kila mtanzania mpenda amani, jambo la kushtua zaidi ni kuona kuwa hata watu ambao wanahusika na kusaidia upatikanaji wa haki za Watanzania nao wamejikuta kwenye hali ya sintofahamu kufuatia kukumbwa na kadhia ya ukosefu wa usalama kwenye ofisi zao, swali la kujiuliza ni je wao wenyewe watakuwa salama iwapo ofisi zao zinaweza kuraruliwa?.

Mapema wiki hii tumesikia taarifa za kulipuliwa kwa ofisi za kampuni ya mawakili ya IMMMA Advocates zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.

Mkurugenzi Mtendaji wa IMMMA Advocates, Sadoc Magai, aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika tukio hilo walielezwa na askari polisi kuwa walikuta madumu yanayodaiwa kuwa petroli ingawa hawakutaja idadi yake.

Kwa mujibu wa, Magai alisema alipigiwa simu na kufika eneo la tukio juzi saa 11 alfajiri. “Saa 11 asubuhi tulikuja, tukakuta polisi wapo tayari hapa, Majirani wanasema tukio lilitokea saa 7 usiku.

“Jengo limekuwa ‘damaged’ (limeharibiwa), hatujui sababu, hatujui nini kimetokea, huko ndani kuta zimevunjika, milango ambayo ‘partition’ yake (imegawanywa) ni vioo imebomoka,” alisema.

Kwa mujibu wa Magai, polisi pia waliwaarifu kuwa walinzi wao wawili wa Kampuni ya, Knight Support waliokuwa wanalinda ofisi hizo siku ya tukio, nao walikutwa wametupwa eneo la Kawe wakiwa hawajitambui, mithili ya watu walioleweshwa dawa.

Hii ni hali ya hatari kwa  maisha ya kawaida kwani ni jambo la kutisha kwa Watanzania kuona kuwa imefikia mahali watu wananguvu ya ‘kuwakunja’ hata wale wanaoaminiwa na kupewa kazi ya kulinda ofisi na mali zake.

Mbaya zaidi ni kukuta walinzi hao wakiwa wametupwa nje na ofisi zao zilipo huku waki hawajitambui, huu ni ujasiri wa ajabu

ambao umekuwa ukifanywa na Watanzania wenzetu ambapo kwa namna yoyote tuna wajibu wa kukemea vitendo hivi kwa nguvu zote tunaopenda amani.

Kwa mujibu wa Rais, wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amenukuliwa kwenye mkutano wake na wandishi wa habari akisema kuwa ofisi hiyo ya IMMMA, wanawakilisha Kampuni ya Madini ya Acacia Mining PLC ya Uingereza ambayo ina mgogoro mkubwa unaoendelea baina yake na Serikali.

Pia mawakili hao wanamwakilisha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad katika mashauri yanayohusu mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho, ambazo zote hizo ni hoja ya sababu ambazo zinaelezwa kama kichocheo cha tukio hilo japo hakuna aliyethibitisha.

“Mawakili wa IMMMA pia ni sehemu ya timu ya mawakili wanaomwakilisha Rais wa TLS katika kesi kadhaa za jinai.

“Wakili Fatma Karume wa IMMMA Advocates amefungua mashauri ya madai dhidi ya askari wa Jeshi la Polisi aliyemshambulia wakati akiwa anatekeleza wajibu wake kama wakili wa Rais wa TLS.

“Hata hivyo, sheria zinazohusika zimeweka wazi katika kutekeleza wajibu wao wa kitaaluma, wanasheria wasitambulishwe na mamlaka za nchi au na wananchi kutokana na masilahi ya wateja wao katika mashauri,” anasema Lissu.

Aliongeza kuwa, inawezekana baadhi ya kazi ambazo wamekuwa wakizifanya mawakili wa IMMMA Advocates siku za karibuni zinaweza kuwa sababu.

Bado kuna utata juu ya kifaa kilichotumika kulipua ofisi hizo za kampuni kubwa ya uwakili hapa nchini.

Hapa kuna maswali magumu ambayo kama Watanzania wapenda amani na taifa letu kwa ujumla lazima tujiulize ikiwamo ni watu gani ambao walitekeleza mlipuko huo.

Lakini pia nia yao ilikuwa ni nini hasa? Aina gani ya mlipuko ambao ulitumika kutekeleza kitendo hicho ambacho hakina sura wala harufu ya kitanzania?

Lakini pia, Je, maboksi yanayodaiwa kuchukuliwa yalikuwa na nini? Kwanini iwe IMMMA? Na kwa nini walipuaji hawakuchukua kitu cha thamani kama kompyuta, simu au fedha kama lengo lao lilikuwa ni kujipatia kipato?

Je, ni kitu gani walichopewa walinzi hadi kulewa na waliwachukua vipi hadi Kawe? Je, polisi waliwatambua vipi kama walinzi hao waliokotwa Kawe ni wa Kampuni ya IMMMA? Rejea kauli ya Magai kwamba aliambiwa na polisi kwamba walinzi hao wamepelekwa Muhimbili na kwamba yeye alikuwa hajawaona.

Haya ni mambo yatakayoturejesha nyumba kama taifa iwapo itabainika kweli kuwa mlipuko huo ulitokea kwa sababu tu ya kuwapo kwa Mawakili wanaotetea vyama vya upinzani au wale wanaoenenda kinyume na Serikali, iwapo itakuwa sahihi basi hii haitakuwa njia salama ya kukabiliana nawatu wanaoipinga Serikali.

Na badala yake itakuwa ni chanzo cha kuibua hali ya hatari ndani ya nchi yetu sisi wenyewe, kwani ni dhahiri kuwa tutakuwa tumeichoka amani yetu sisi wenyewe ambayo mataifa kadhaa yameikosa. Kila Mtanzania anawajibu wa kukemea kitendo hiki kwani iwapo tutaacha kwamba ni mambo ya wanasiasa tutakuwa tunajichimbia shimo sisi wenyewe.