Home Michezo Kimataifa CAF KUIVUA KENYA WENYEJI CHAN 2018?

CAF KUIVUA KENYA WENYEJI CHAN 2018?

1126
0
SHARE

HASSAN  DAUDI  NA  MITANDAO

FAINALI za Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani maarufu kama ‘Chan’  zinatarajiwa kufanyika kati ya Januari 11 na Februari  mwakani nchini Kenya.

Hata hivyo, kasi ya uandaaji wa viwanja vitakavyotumika imeonekana kuwashitua wadau wa soka kiasi cha kuanza kutilia shaka utayari wa nchi hiyo kuweza kuandaa fainali hizo zenye mchango mkubwa katika kuinua ligi za ndani  barani  Afrika pamoja na viwango vya wachezaji wengi wazawa .

Inaelezwa kwamba ni Viwanja vya Meru Kinoru na Kasarani pekee ndivyo  vinavyoonekana kuwa sawa katika orodha ya vile vitakavyotumika.  Uwanja wa Kasarani ni ule ulioandaliwa kwa ajili ya Michuano ya Riadha ya Vijana wenye umri  chini  ya  miaka 18, iliyoanza Julai 12 na kumalizika Julai 16, mwaka huu.

Kasarani ndiyo uwanja pekee uliofikia viwango vya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), ukiwa na mfumo wa uchukuaji wa matukio ‘live’, vyumba vinne vya kubadilishia, vyumba vya waamuzi, na chumba maalumu cha kukabiliana na utumizi wa dawa za kuongeza nguvu michezoni.

Kwa upande mwingine, viwanja vingine vitatu vilivyopo kwenye ratiba ya kutumika katika michuano hiyo ya Chan mwaka 2018 vimeonekana kuwa na changamoto kubwa. Viwanja vya Kipchoge Keino na Machakos havijaweza kuwa kwenye ubora unaoweza kukubalika na Caf.

Julai mwaka huu,  Rais wa Caf, Ahmad Ahmad, alisema Kenya wameomba kupewa hadi mwezi ujao kuhakikisha viwanja hivyo vinakuwa sawa, kwani shughuli nyingi zilisimama kupisha Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8.

Ombi lao hilo limekubaliwa na Caf, na wamepewa hadi  kufikia Septemba 7 viwe tayari kwani  maofisa wa Shirikisho hilo watakwenda kufanya ukaguzi.

Hata hivyo, akizungumzia uwezekano wa Kenya kupoteza nafasi ya kuandaa Chan 2018, endapo watashindwa kukamilisha miundombinu, Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini humo, Sam Nyamweya, alitahadharisha jambo hilo akisema litakuwa baya mno na kuleta athari kubwa kama nchi.

“Itakuwa mbaya ikiwa Kenya itapokwa uenyeji wa fainali hizo za Chan,  Sipati picha  jinsi tutakavyokuwa tumepoteza rasilimali nyingi zilizotumika kuipata nafasi hiyo,” alisema Nyamweya.

Taarifa zilizopatikana nchini humo zimedai kwamba kuipata haki ya kuandaa michuano hiyo mwaka 2013,  Kenya ilitumia kitita cha  fedha takribani Sh milioni 50.

“Hii si habari njema kwa Kenya kabisa. Nafikiri  wahusika wanayafanyia kazi  na jitihada hizo zitazaa matunda ili kuhakikisha tu kama nchi Kenya itaandaa michuano kama ilivyopangwa,” alisema kiongozi huyo wa zamani wa KFF.

Katika hatua nyingine, tayari mataifa mawili ya Morocco na Ethiopia yameshajitokeza kusikilizia upepo edapo Kenya itapokonywa wenyeji basi yaweze kuwania nafasi hiyo ya kuandaa fainali hizo.

Lakini kama itakuwa hivyo, haitakuwa mara ya kwanza kwa Kenya kupoteza nafasi kama hiyo  ya kuandaa michuano ya Caf.

Itakumbukwa kuwa nchi hiyo ilitakiwa kuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa Afrika (Afcon) mwaka 1996, lakini ilijikuta ikinyang’anywa nafasi hiyo na nafasi yake kupewa……….

Baadaye ni Kenya ambayo ndiyo iliyoandiika barua kwenda Caf, wakadai  hawako tayari kuandaa michuano hiyo na hatimaye bahati ikaiangukia Afrika Kusini.  Haikuishia hapo  bali Caf waliipa adhabu Kenya wakiifungia kushiriki fainali mbili  za  Afcon.

Huku Kenya wakishushiwa rungu hilo, wenyeji Afrika Kusini walichukua ubingwa kwa kuichapa Misri katika mtanange wa fainali na kubeba taji hilo.

Wachambuzi wa soka wametilia mashaka kuwa huenda balaa hilo likaikuta tena Kenya, endapo tu itashindwa kukamilisha mapema maandalizi ya Chan  2018.

Ivory Coast nao wako makini kufuatilia kama Kenya watanyoosha mikono ili  waweze kujitosa kuwania uwenyeji wa michuano hiyo inayoandaliwa na shirikishyo hilo la soka la Afrika.

Ujumbe wa Caf utakaokuwa na wakaguzi utaingia Kenya Septemba 7 ,waka huu na kufanya kazi hiyo kwa siku chache kabla ya kuwasilisha ripoti  na kujulikana mbivu na mbichi  juu ya suala hilo..

Hata hivyo, mmoja wa vigogo wa Kamati ya Maandalizi, Herbart Mwachiro, amewatoa hofu mashabiki wa soka nchini Kenya akisema michuano hiyo itafanyika nchini humo kama ilivyopangwa.

“Haki ya kuandaa Chan  itabaki  kuwa ni ya Kenya mpaka pale Caf watakavyoamua vinginevyo.  Kumekuwa na hofu kuwa hatutaandaa lakini  binafsi ninaamini tutakuwa tayari tumekamilisha matengenezop yote hadi kufikia muda uliopangwa ,” alisema Mwachiro.

Alisema kumekuwa na miradi mikubwa ya ukarabati tangu Uchaguzi Mkuu ulipomalizika, ukiwamo wa kuufunga Uwanja wa Taifa wa Nyayo kwa ajili ya matengenezo.

Katibu wa Wizara ya Michezo, Utamaduni na Sanaa nchini humo, Dk. Hassan Wario,  naye alisisitiza kwamba uhondo wa Chan 2018 utakuwa Kenya na si kwingineko.

Mataifa 14 yanatarajiwa kushiriki fainali hizo ambazo hutupiwa macho na mawakala mbalimbali pande zote za dunia. Baadhi ya nchi ambazo trayari zimefuzu ni pamoja na Morocco, Cameroon, Nigeria na  Ivory Coast huku zingine zikiwa bado zinapigana kuwania nafasi hiyo.