Home Habari kuu KARUME AWAKOSOA VIONGOZI, BALOZI MWAPACHU AMUUNGA MKONO

KARUME AWAKOSOA VIONGOZI, BALOZI MWAPACHU AMUUNGA MKONO

4773
0
SHARE
NA MWANDISHI WETU   |  

RAIS mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume amekosoa hatua ya viongozi wengi wa Afrika kukosa uadilifu na uwajibikaji, hatua inayoweza kutowesha amani katika nchi zao. RAI linaripoti.
Kiongozi huyo wa zamani wa Zanzibar ambaye alifanikisha kurejesha amani ya kisiasa visiwani humo kwa kuridhia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, aliwataka viongozi wa Afrika kutambua kuwa siasa ni harakati muhimu na halali za binadamu kwa sababu zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Alisema  katika kuendesha siasa safi inapobidi si vibaya ikatolewa nafasi na uwiano  sawa kwa masilahi ya makundi mbalimbali ndani ya jamii.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa uadilifu na uwajibikaji kutoka kwa viongozi wa serikali, vyama vya siasa, Wabunge, Mahakama, wananchi, tasnia ya habari, asasi za kiraia na hata taasisi za dini.”
Karume aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa Taasisi ya Amani Duniani-Global Peace Foundation (GBF), uliofanyika kwenye ukumbi wa Skainos, mjini Belfast nchini Ireland, Machi 8 mwaka huu.
Katika mkutano huo mada kuu ilikuwa ni “Umuhimu wa uongozi adilifu na wa ubunifu kwa ajili ya amani Barani Afrika.”
Katika hutoba yake hiyo, Rais mstaafu Karume  alihimiza utamaduni wa kuaminiana na kuheshimu siasa na taasisi za utawala na kusema kwamba vitu hivi ni muhimu kwa kudumisha amani ndani ya jamii, hususani katika nchi zenye demokrasia changa.
Alisema katika suala la uaminifu  ni lazima viongozi  wasimame kidete kushughulikia majukumu yao ya kiutawala na maadili hasa katika medani za siasa zenye changamoto nyingi ndani ya jamii zilizogawanyika.
Aliyataja maadili yanayopaswa kusimamiwa na viongozi kwa nguvu zao zote kuwa ni  uadilifu, uaminifu na utoaji wa haki.
“Viongozi wanapaswa kuwa waadilifu,lazima wawe wanyenyekevu na wasisite kuonyesha ari yao ya kuifanyia makubwa jamii inayowazunguka, wajitahidi kutokuwa na upendeleo, wawe tayari kuwajibika, kukiri makosa na kuheshimu haki za kila raia.”
Akimnukuu Rais wa zamani wa Mexico, Benito Juarez, Rais mstaafu Karume alisema:  “kuheshimu haki za wengine ndiyo amani yenyewe.”
 “Viongozi wa kisiasa lazima wawe mfano kwa wafuasi wao ambao wanapaswa kuwaona viongozi wao kama ni waadilifu, wakuaminika na wenye ujasiri.
“Barani Afrika tuna bahati ya kuwa na viongozi wengi walioonyesha viwango vya juu vya uadilifu na ubunifu katika uongozi wao kama vile waasisi wa mataifa yetu Samora Machel wa Msumbiji, Kenneth Kaunda wa Zambia, Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini hapa nimewataja wachache tu.
“Na kama ni lazima basi pia nijitaje mimi mwenyewe na marehemu baba yangu Abeid Aman Karume ambaye katika kipindi kifupi tu aliweza kuleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi Zanzibar.”
Alisema suala la uongozi wa uadilifu halitokani na uzoefu wake wa urais wa Zanzibar, bali ni suala ambalo linaendelea kumiliki fikra zake, mazungumzo na wenzake na matumaini yake katika hali ya baadaye ya nchi yake kwa ujumla.
 “Si peke yangu ninayethamini uongozi wa adilifu na kufahamu umuhimu wake katika kuijenga amani. Uwepo wenu kwa wingi leo katika mkutano huu unaonyesha umakini wenu mlio nao katika suala hili.
“Tumekutana hapa kupeana na kujadili mawazo muhimu ya uongozi adilifu katika kujenga na kudumisha amani miongoni mwetu, suala la uongozi adilifu limejikita katika jamii zote duniani tangu enzi za Julius Cesar na bado linaendelea kumiliki vichwa vya habari katika vyombo vya habari na kuwa katika mijadala mbalimbali miongoni mwa wasomi na watu wengine.”
Gaius Julius Caesar alikuwa kiongozi wa kisiasa na wa kijeshi wa Roma ya Kale. Anakumbukwa hasa kwa mambo mbalimbali yanayoonekana kuathiri dunia hadi leo
Aidha, Karume alisema Afrika ni Bara lililo katika mageuzi makubwa, lina utajiri mkubwa wa rasilimali za asili na nguvukazi kubwa, lakini bado linajikongoja katika kuuondoa umasikini, njaa na ongezeko la tofauti kati ya walionacho na wasio nacho.
Akizungumzia suala la kukosekana kwa usalama katika nchi nyingi za bara hilo, alisema kunatokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, ugaidi na vurugu nyingine.
Alisema muda sahihi wa kuondoa changamoto hizi zilizopo chini ya mwavuli wa utawandawazi barani Afrika ni sasa, lakini ili tufanikiwe kwenye hilo kunahitajika kuwepo viongozi waadilifu na wenye utayari wa kuwajibika.
WASHIRIKI WENGINE
Katika mkutano huo uliokuwa na dhamira ya kuimarisha masuala ya amani, Rais mstaafu Karume aliungana na watoa mada wengine 14 kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini na wa kisiasa.
Miongoni mwao ni rais wa taasisi ya GBF James P. Flynn, makamu wake Dk. Tony Devine na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Peter Sheridan.
Wengine ni mchungaji Dk. Lesley Carroll,  Mchungaji Gary Donegan, Mbunge wa zamani wa jimbo la Belfast Mashariki, mwanaharakati wa haki za lugha Linda Ervine, Mchungaji John Joseph Hayab na mwanaharakati David Holloway.
Wasemaji wengine katika mkutano huo walikuwa ni Mwanasheria wa kimataifa Conor Houston,  Shekhe Halliru Abdullahi Maraya kutoka Nigeria, mwanasiasa wa zamani wa Ireland Tina  McKenzie, mpigania haki za binadamu Andree Murphy na Mkurugenzi wa GPF nchini Nigeria, John Oko.
BALOZI MWAPACHU
Akizungumzia hotuba ya Karume kupitia mtandao wake ya Twitter, mwanasiasa mkongwe Balozi Juma Mwapachu ameiunga mkono na kuipongeza hotuba hiyo kwa kusema inaelezea hali halisi ya kisiasa na kiuchumi ilivyo Barani Afrika kwa sasa.
Mwapachu ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini pamoja na kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa alisema hotuba hii ingefaa kusambazwa nchini kwani ina umuhimu mkubwa hususani kwa vijana ambao wanahitaji kufahamu vyema kasi ya mabadiliko katika kipindi hiki.