Home Latest News SERIKALI INA WAJIBU KUWAELEZEA WANANCHI JUU YA GESI ASILIA

SERIKALI INA WAJIBU KUWAELEZEA WANANCHI JUU YA GESI ASILIA

3907
0
SHARE
NA HILAL K. SUED  |

Liliibuka kwa kishindo na baadaye kupotea kimya kimya. Ndivyo mtu anaweza kulielezea lile suala la kutangazwa kugundulika matrilioni ya futi mraba ya gesi asilia chini ya bahari katika maeneo ya Pwani ya kusini mwa nchi yetu.

Takriban miaka sita imepita tangu tukio hilo lililowapelekea wakazi wa mji wa Mtwara na maeneo ya jirani kufanya maandamano makubwa kupinga kauli ya serikali ya rais Jakaya Kikwete kuisafirisha nishati hiyo itakayovunwa kupelekwa Dare es Salaam na sehemu nyingine za nchi.

Mengi yalisemwa na kuandikwa wakati huo kuhusiana na suala hilo lililowagusa sana wakazi wa huko. Lakini hasira zao hasa hazikutokana na kile kilichoonekana cha serikali kuwa tayari kusafirisha maliasili hiyo kutoka mkoani mwao, bali pia lilitokana na tabia ya milolongo ya awamu za tawala zilizopitz kuwasahau kimaendeleo watu wa mikoa hiyo ya kusini na kwa ujumla kuwachukulia Watanzania wote kuwa ni watu wa kuafiki kila kitu, kila mipango ya serikali.

Miaka sita baada ya tukio lile ambalo lilikuwa la kutangazwa tu uwepo kwa wingi kwa maliasili hiyo mambo yametulia huku hakuna hata futi mraba moja ya gesi asilia iliyochimbwa na kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa lengo la kunufaika na fedha za kigeni.

Baadhi ya makampuni yaliyoshinda zabuni ya kupata ‘vitalu’ yameshindwa kufanya hivyo ingawa inadaiwa mitambo wa kuitoa gesi asilia hiyo kutoka kina kirefu (urefu zaidi ya sehemu nyingine duniani kunakopatika maliasili hiyo baharini) bado haipo kutokana na mapungufu ya teknolojia, au ndiyo iko mbioni kutengenezwa.

Lakini pia kuna suala la bei ya nishati hiyo pamoja na ile ya mafuta yasiyosafishwa katika soko la dunia kuwa chini – tena kwa kipindi kirefu tu hadi sasa – hali huenda ndiyo inayowafanya wawekezaji watarajiwa kusita kuanza shughuli ya uchimbaji.

Lakini haya ya ukimya yanayotokea hayaendani na hali iliyokuwapo miaka sita iliyopita kule Mtwara. Hamasa iliyokuwapo ilikuwa kubwa sana kwani kuna watu walipoteza maisha yao na wengine mali zao kutokana na ghasia zilizoibuka. Aidha kulikuwapo lugha za jeuri zilisikika kutoka kwa baadhi ya viongozi kama vile ile ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo akiwaponda wananchi wa huko.

Aliwatuhumu kwa kutojua chochote, kwa kucheza ngoma wasioijua, kutumiwa na wanasiasa wanaotafuta umaarufu, kutokuwa na shukurani kwamba siku zote wamekuwa wakiendelezwa na rasilimali kutoka sehemu zingine kama vile mkonge, kahawa na pamba, na kwamba gesi yenyewe inayogombaniwa wala haipatikani katika eneo lao, bali chini kabisa ya Bahari ya Hindi na mbali kabisa kutoka pwani yao.

Watu hawakukawia kumjibu: Hivi kweli alisahau kwamba Wana-Kusini pia walikuwa wanazalisha korosho iliyokuwa inaendeleza wanachi wa mikoa mingine pia?

Aidha aliwakejeli baadhi ya wafanyabiashara wazalendo ambao nao walikuwa wanaomba kupewa vitalu, akiwaambia hawawezi hiyo shughuli kwani wao wajikite katika kujenga viwanda vya juisi tu ambavyo ndiyo wanaweza.

Sasa kutokana na haya yote yaliyotokea angalau serikaliingekuwa inawaambia wananchi kitu gani kinachoendelea kwani walikuwa na matumaini makubwa katika maendeleo yao. Si vizuri kuwaacha hivi hivi bila kauli yoyote.

Ghasia za wakati za miaka sita iliyopita zilionyesha kitu kimoja: kwamba pamoja na mengine nchi hii inabadilika kwa kasi ya ajabu, kasi inayoonyesha serikali kuachwa nyuma katika mengi, hasa katika ufahamu wa wananchi. Ama ni kutokana na matatizo (sipendi sana kutumia neno ‘changamoto’ – msamiati ambao nauona umejaa usanii), au kutokana na uamsho (awareness) kutoka kwa wanaharakati, asasi za kiraia na vyama vya upinzani. 

Na hali hii yote ilitokana na serikali yenyewe kuendelea kuwa na dhana kwamba Watanzania wa ‘miaka ya 47’ ndiyo hawa hawa wa leo — kifikra. Kwa kutumia msamiati wa mitaani ni kwamba serikali imekuwa ‘haiko beneti’ na wananchi wake.

Kwa mfano, nadiriki kusema kwamba aliyekuwa rais wakati ule Jakaya Kikwete alifanya kosa kubwa sana pale alipozindua ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam katika tukio lilofanyika Kinyerezi, nje kidogo ya Dar es Salaam mapema mwezi Novemba mwaka jana. Hilo lilikuwa kosa moja kubwa ambalo bila shaka wana-Mtwara na wakazi wengine wa mikoa ya kusini waliliona na ambalo liliashiria kwamba mambo ni kama siku zote – maendeleo ni Dar es Salaam kwanza.

Kwa nini tukio hilo lisifanyike Mtwara, au eneo lolote huko huko kusini? Yumkini Wana-Mtwara waliona wamepuuzwa, pamoja na kwamba nishati hiyo iko chini ya ardhi yao. Hata kama serikali ilikuwa na mipango yake ya mtazamo wa kitaifa, angalau Kikwete angekwenda huko kuzindua ujenzi wa bomba, na kuwahutubia wakazi wa huko kwa kuwaambia serikali yao (chini ya ‘uongozi bora wa CCM’) itahakikisha kwanza kabisa inawanufaisha wao kwanza, hata kama ni maneno ya blah blah, yasiyo na udhati wowote ndani yake, lakini kauli ya namna hiyo ingewaliwaza Wana na wasingefanya zile ghasia.

Lakini kwa upande mwingine ni jambo jema kwa hatua ya serikali yetu ya kufanya subra kubwa katika suala zima hili ikilinganishwa na nchi kama Msumbiji na Chad, nchi ambazo hazikuwa na subra na matokeo yake yalijikuta yakibeba mizigo mikubwa ya madeni.

Msumbiji iligubikwa na kashfa kubwa mwishoni mwa mwaka 2015 baada ya kubainika kwamba mashirika mawili ya umma yalikopa kwa siri jumla ya Dola za Kimarekani 2 bilioni kutoka mabenki ya Ulaya kati ya 2012 na 2014. Ilidaiwa fedha hizo zilipangwa kugharamia kile kilichoitwa mradi wa kulinda mazingira katika maeneo ya pwani ya nchi hiyo.

Ilidaiwa kwamba serikali ingerejesha mikopo hiyo kutokana na mapato ya mauzo ya gesi asilia – ambayo ilitokana na taarifa zilizotangazwa – kwamba ilikuwa imegunduliwa kwa wingi katika bahari inayopakana na nchi hiyo. Hadi sasa hata galoni moja la gesi asilia hiyo haijauzwa nje.

Na huko Chad mwaka 2014 kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya nchji hiyo ilikopa Dola za Kimarekani 1.4 bilioni kutoka Glencore, kampuni ya kibiashara ya Uswisi.

Mkopo huo ulitakiwa kulipwa kutokana na mauzo ya hapo baadaye ya mafuta yasiyosafishwa yanalyozalishwa nchini humo – wakati huo bei ya nishati hiyo katika soko la dunia ilikuwa zaidi ya Dola 100 kwa pipa. Lakini miaka miwili baadaye, wakati bei hiyo ikiporomoka, ulipaji wa deni hilo ulikuwa unatafuna asilimia 85 ya mapato ya nchi hiyo yanayotokana na mafuta yasiyosafishwa.