Home Habari MFALME ALIZUIA MTO ILI WAPINZANI WAKOSE MAJI

MFALME ALIZUIA MTO ILI WAPINZANI WAKOSE MAJI

2298
0
SHARE

NA BALINAGWE MWAMBUNGU

“Sisiemu ni ile ileile, sisiemu ni Nambari One, mtaisoma namba, wape wape vidonge vyao” ni baadhi ya nyimbo za bendi ya Chama cha Mapinduzi, TOT zinazoimbwa wakati wa kampeni kwa mbwembwe nyingi na kejeli kwa vyama pinzani. Je, kweli sisiemu ni nambari wani? Kwa vigezo vipi?

Kimeenea nchi nzima hadi vijijini, inadaiwa kuwa na wanachama milioni 10, ni chama dola, kimeshinda kila chaguzi—tangu mfumo wa vyama vingi ukubaliwe kikatiba. Ni taasisi kubwa na ni chama kikongwe kuliko vyote hapa nchini. Kwa hiyo kina viongozi wenye uzoefu mkubwa katika utawala na mambo ya siasa. Hili halina ubishi.

Kwa hiyo, chama Nambari One kinaaminika na wananchi, hakiwezi kufanya figisu figisu kwenye uchaguzi wowote ule. Chama kipana ambacho ni Nambari One, hakiwezi kubebwa na vyombo vya Dola—hasa Jeshi la Polisi, kwa sababu kina mizizi mirefu.

Chama Nnambari One ni chama dume (sijui kama kuna chama jike), hakiogopi mgombea binafsi. Ni chama kinachofuata

Katiba yake na kanuni lilizojiwekea. Chama Nambari One, hakiwezi kuiba kura kama inavyodaiwa, wala hakiwaagizi vijana wake kuwafanyia fujo, kuwapiga, kuwaumiza na hata kuwaua wapinzani wake.

Haya ni madai ya wapinzani ambayo hutokana na kukosa kuaminiwa na wananchi katika kila uchaguzi mkuu—ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano, au chaguzi ndogo za marudio.

Chama Nambari One, kinamini katika misingi ya haki na hakiogopi kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Kinaitaka Serikali ifute sheria ya sasa inayompa madaraka Waziri wa Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa, kuwa msimamizi mkuu wa chaguzi zote—za Madiwani na  Wabunge.

Chama Nambari One hakiwezi kuogopa undwaji wa Katiba Mpya kama ilivyopendekezwa na wananchi hupitia Tume ya Jaji Joseph Warioba.

Chama Nambari One hakiogopi kura za siri katika vikao vyake vya ndani, wala hakimlazimishi Spika wa Bunge kutumia kura ya mayowe ya ‘ndiyooo’—ana uhuru wa kutumia kanuzi za Bunge—za siri au uwazi.

Chama Nambari One hakiwezi kuwanyamazisha wanachama wake kuhoji namna baadhi ya viongozi wake wanavyopatikana. Ni uwongo kwamba wajumbe wa kikao fulani cha juu, eti walipewa shilingi tano kila mmoja, ili kupitisha jina la mtu mmoja ambaye uongozi wa juu ulimtaka. Uwongo usio kifani. Wajumbe wanaweza kunyamazishwa kwa shilingi tano (5) kweli? Kama si uzushi nini?

Chama Nambari One hakiwezi kudhoofisha vyama vingine, ili kibaki peke yake bila ushindani. Mchezo uitwao siasa (au ni sihasa?), hauwezi kunoga bila upinzani. Ni kama nilivyosoma maelezo ya picha kwenye lori limeandiandikwa: “Mwanaume asiye na mchepuko ni sawa na Taifa bila chama cha upinzani.” Raha ya vyama vingi ni ushindani wa hoja.

Eti chama Nambari One kiko kizimbani kutokana na matokeo chanya ya uchaguzi mdogo wa majimbo ya Ukonga  na Monduli. Nani anasema hesabu haikuwa sahihi? Angali kura za 2015. Jimbo la Monduli, mkoani Arusha, walijiandikisha watu 1,002,023.

Katika uchaguzi wa marudio, Monduli waliojiandikisha ni 80,282 waliopiga kura ni watu 69,521 kwamujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi. Na Ukonga yenye watu wenye haki ya kupiga kura ni 300,609. Waliopiga kura ni 88270.

Chama Nambari One huenda kimefungua mashina na matawi mengi katika majimbo ya Ukonga na Monduli tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015—ndio tafsiri ya ushindi wa kishindo! Kimefanyakazi kubwa na kuwaingiza wanachama wapya wengi. Na matokeo yake ndiyo hayo. Sio jambo la kubeza hilo.

Chama kimefanya kazi nje na ndani ya chama, ili pasiwepo wanachama wenye manung’uniko ya kuwapendelea ‘wageni’ na kuwaacha wanachama ‘ndakindaki’—ambao wamekipigania chama chao wakati wote—liwake jua au ipige na mvua, wao kijani tu.

Tunajua kwamba Tume ya Uchaguzi iliwahi kueleza kwamba itaboresha kwanza Daftari la Wapigakura ili, wanaopinga matokea kwamba wasimamizi wa baadhi ya vituo, walikuwa wanachama wa chama Nambari One, wafanye ulinganifu.

Tume ilifanyakazi yake kwa uwadilifu—kufuta majina ya waliohama/kufariki katika majimbo ya Monduli na Ukonga. Tume iliwaingiza vijana wengi ambao mwaka 2015 hawakupiga kura kwa kuwa walikuwa na umri mdogowa miaka 15. Miaka mitatu baadaye (2018), wamefikisha miaka 18 ambao ni umri wa kupiga kura.

Monduli na Ukonga kulikuwa na idadi kubwa ya wapigakura waliohamia chama Nambari One kuwafuata Madiwani na Wabunge waliopachikwa jina la Wasaliti!

Sio rahisi chama kujikusanyia kura na kujitangazia ‘ushindi wa kishindo’ katika chaguzi zote za marudio. Ila ni rahisi kuteka nyoyo za watu, ili wafanye yale waliyo yakataa mwaka 2015!

Serikali ya chama Nambari One, imefanya iliyoyakusudia kufanya—kutochezea haki za Wananchi kwa kuwaelekeza watendaji wake wasiwanyime wapinzani haki ya kugombea udiwani na ubunge kwa kufunga ofisi siku ya kurejesha fomu. Wahakikishe kwamba wagombea wa vyama vingine wanaelekezwa namna ya kujaza fomu, ili wasikutane na balaa la kukataliwa kwamba fomu zao zilikuwa na makosa na hivyo kuruhusu wagombea wa chama Nambari One wamepita bila kupingwa. Kwa njia hiyo, tunajua sio kwamba hatujui kwamba tunakijenga chama chetu upya na sio kukiua!

Tunajua pia kwamba Tanzania ni ya Wananchi, wanasiasa ni viongozi, na kwamba viongozi hawana haki ya kuwachagulia wananchi nani awe kiongozi wao—tunalijua hili. Hatuwezi kuwanyang’anya haki yao ya Kikatiba ya kumchagua mtu wanaye mtaka kuwa kiongozi wao.

Lakini haishangazi kuwa kuna wazushi wanaodai kuwa chaguzi za chama Nambari One huendeshwa kimizengwe. Uchaguzi kama ule wa kumpata mgombea urais mwaka 2015, ulitumia Kanuni za chama kuwaengua watia nia—idadi yao ilikuwa kubwa mno.

Wajumbe wa NEC na Mkutano Mkuu, walipitisha jina la mgombea kwa furaha na kumkataa mgombea ambaye alikuwa amebebwa na Mwenyekiti. Matokeo ndio hayo—mnaisoma namba?

Kwa kawaida binadamu anajisikia vizuri kama amechaguliwa kwa uhuru kabisa, ili awaaongoze wenzake. Anafanya kazi yake kwa mapenzi na uhuru, kwa sababu anajua ana watu nyuma yake. Lakini hapawezi kukosekana mtu mmoja au kikundi cha wachache, kudai kwamba ilitumika hila, ili mtu fulani achaguliwe. Madai kama hayo huwa yanamfanya aliyechaguliwa kufanya kazi kwa hofu, na ili kuficha hofu aliyo nayo, huwajengea hofu wengine—wasimwonyeshe kidole—huyo hakustahili, kabebwa!

Nani anasema chama Namba One hakipendwi? Eti kinatumia watendaji wa Serikali na polisi kuhakikisha kinapata ushindi! Uzushi huo. Kwa nini wanashangaa Mkuu wa Mkoa kumwomba msamaha Mwenyekiti wake kwa kupoteza Kata moja katika uchaguzi wa marudio wa Madiwani. Anaonesha kwamba hakutimiza wajibu wake vizuri. Azima yetu ni kuwa na sauti moja tu—ya Serikali inayojali na kutetea haki za wanyonge—ndio maana tunawaambia tutatawala kwa miaka 200—tunakubalika kwa wananchi!

Halafu chama kinatangaza kuwa kimepata ushindi wa kishindo, wanatokea watu kudai ‘uwanja wa mashindano haukuwa sawa’. Wanayatoawapi haya?

Eti JKN aliasa kwamba mtu mwenye afya asijipine afya yake kwa kujilinganisha na mgonjwa, sasa kama hakuna mwenye afya kwa nini usijitangaza kwamba wewe uko vizuri (fit) kiafya!

Angalizo: Yako mengi ambayo sisi washika kalamu tunaogopa kuyaandika kwa sababu tumejazwa hofu. Washika kalamu ndio wanaoshikilia uhai wa Taifa—hata walio madarakani wanajua—ndio maana wanapenda watangazwe kila wanalolifanya. Kuna watu watabisha kwamba washika kalamu sio watu muhimu—wao ni vipasa sauti tu.

Hebu siku moja tufanye jaribio. Tuweke kalamu chini tuone itakuwaje! Sisi washika kalamu ndio wahifadhi wa historia ya awali. Watafiti wanajenga huanzia kwenye mambo ambayo yapo kimaandishi, au yamehifadhiwa kielektroniki au picha mnato.

Baada ya hapo wasomi huandika historia ya nchi au ya jambo lolote la kisayansi, kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Picha ya askari polisi (Mwananchi 18/09/18), wakisherekea ‘Ushindi’ wa chama Nambaeri One, baada ya uchaguzi wa marudio Ukonga kumalizika, huku wakimbeba kada wa chama tawala, ambaye pia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ni mfano mzuri wa kuweka kumbukumbu za historia ya awali ya mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini Tanzania na ni ushahidi usio tia shaka—kwamba chama hicho kinabebwa na dola. Bila dola, hakuna chama Nambari One! Kama mliokabidhiwa dola mnabisha, jaribuni 2020.

Kuna hadithi ya Mfalme ambaye alifunga mto ili kuwakomoa watu wa bondeni wasipate maji kwa sababu walipinga kutawazwa kwake kama mfalme. Watu wale walipata shida sana. Lakini  Waswahili husema; Mungu si Athumani. Baada ya miaka mingi kupita, Mungu aliteremsha mvua kubwa iliyodumu kwa miezi siku kadhaa. Wananchi wale wakapata akili ya kuhifadhi maji.

Mvua zilipokoma wakashituka kuona mto ulioibuka mbali na korongo la mto uliozibwa na Mfalme. Wakamshukuru Mungu kwa maajabu yake. Hawakujua kama katika bwawa alilojenga Mfalme, sehemu moja ya kilima, ilikuwa na mwamba wenye kuvyonza maji (porous)  taratibu, na uliposhiba, ukaachia maji ya ziada na kufungua njia mpya ya mto.

Katika hotuba mojawapo ya mwaka 1993, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema:

“Msitikise nchi kwa mambo ya kijinga kijinga. Nchi kama hii yetu inatawaliwa na Sheria. Haitawaliwi na mtu. Kwa hiyo Rais ni Rais wetu, lakini kwa mujibu wa Katiba. Ni Amiri Jeshi Mkuu kwa mujibu wa Katiba.”

Rais wa Tanzania anaongoza kwa mujibu wa Katiba. Aliapa kuilinda na kuitetea Katiba na wateule wake hula kiapo cha utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye alikula kiapo cha utii kwa Katiba.

Washika kalamu tusifumbe macho, tusifumbe midomo, tuseme na tuandike nakuweka kumbukumbu sawa sawa kama viongozi hawaiheshimu Katiba. Katiba inatamka kwamba Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi. Kwa maneno ya Mwalimu:

“Lazima tufanye jitihada kubwa kuhakikisha Katiba inaheshimika. Tuhakikishe kuwa tunaongozwa kwa mujibu wa Katiba na sheria mbalimbali zilizotungwa. Hili ni jambo muhimu sana.

Tukitaka kufika salama huko tuendako, Chama Nambari One, na vyama vingine vyote, vizingatie Katiba na sheria za nchi. Viongozi watapita, vyama vitapita, Tanzania itabaki.