Home Habari Hekima za Lowassa zilimwokoa Mbowe

Hekima za Lowassa zilimwokoa Mbowe

2627
0
SHARE

mbowe22NA SHABANI MATUTU

MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amejikuta akitumia zaidi ya saa moja kuwashawishi wajumbe wa Kamati Kuu (CC) kulikubali jina la Dk. Vicent Mashinji kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, RAI limeelezwa.
Dk. Mashinnji ambaye kitaaluma ni daktari ameteuliwa kuwa Katibu mkuu wa chama hicho na Kamati kuu ya chama hicho iliyoketi hivi karibuni jiji Mwanza, nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Wilbrod Slaa aliyejiondoa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuingia na kuwa mgombea urais kupitia chama hicho.

Uteuzi wa Dk. Mashindi uliridhiwa na Baraza Kuu la chama hicho lililoketi sambamba na kikao cha Kamati kuu.

Chanzo cha kuaminika katika Kamati hii kilisema sababu ya Mbowe kutumia muda huo ilichangiwa na kuteua mtu anayeelezwa kutokuwa na ushawishi ndani na nje ya chama.

Chazo hicho kilisema pamoja na Mbowe kutumia muda mwingi kuwaaminisha wajumbe kwamba Dk. Mashinji ni mpambanaji kwani alikuwa kiongozi wa  mgomo wa madaktari waliokuwa wakiwakidai maboresho ya mishahara, lakini walionekana kutounga mkono hoja hiyo na waliendelea kushikilia msimamo wao wa kumkataa kuwa hafai kwa maslahi mapana ya chama chao.
Hata hivyo inasemekana Mbowe aliokolewa na aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa katika uchaguzi uliopita, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyesimama na kuwaomba wakubaliane na uteuzi wa Mwenyekiti.
“Lowassa alitoa wito kwa wajumbe wakiokoe chama  kisipasuke kwa kumkubali na kumuamini mtu aliyeteuliwa na Mwenyekiti… wajumbe wote walikubaliana na kutii kauli hiyo ya Lowassa hali iliyomaliza mvutano uliokuwepo katika kikao hicho,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kilisema kabla ya Lowassa kumuokoa mwenyekiti ambaye hajawahi kukutana na hali ya kupingwa kama ilivyotokea kwenye kikao hicho cha Mwanza, alikuwa alikuwa akionyesha hali ya kukata tamaa kugeuza misimamo ya wajumbe waliokuwa wakimpinga Dk. Mashinji kuwa hatoshi kukiongoza chama hicho.
Chanzo hicho kilisema kwamba miongoni mwa wajumbe waliosimama kidete kupinga mapendekezo hayo  mbele ya Mwenyekiti, baadhi yao ni Ezekia Wenje, Mchungaji Peter Msigwa na Lazaro Masei wa Karatu.
“Wenje alisimama na kuomba aingizwe kwenye rekodi ya kumkataa kwa sababu hafai kwa kuwa chama kinahitaji Katibu Mkuu mwenye jina na uwezo,” alisema mtoa taarifa wetu ndani ya kikao hicho.

Mjumbe mwingine anayeelezwa kumkataa alikuwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu aliyesema kwamba kwa uteuzi wa Dk. Mashinji Chadema kimecheza bahati kamari.
Mjumbe mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alilieleza gazeti hili kwamba sababu nyingine waliyokuwa wakimkataa Dk. Mashinji ilichangiwa na ugeni wake katika siasa za Tanzania.
“Chama hiki kwa sasa  kimekuwa hivyo hakikuwa na sababu ya kuwa na Katibu Mkuu atakayetumia muda mrefu kujifunza kazi katika mazingira haya ambayo muda huo haupo.
“Katibu Mkuu ambaye angehitajika kwa sasa ni yule ambaye baada ya kutangazwa tu, kuwa Katibu wa chama hiki kinachokuwa kwa kasi angeanza kazi mara moja baada ya kupitishwa na kikao,” alisema mjumbe huyo.
Alisema chama kilitakiwa kuwa na Katibu Mkuu mwenye uwezo wa kuzuia yale ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kuwepo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama rushwa, makundi na ubaguzi.
Alisema kwamba anawasiwasi kama kweli Katibu Mkuu ambaye ni mgeni atatumia muda mfupi kusimamia maadili bila kupendelea vigogo walio ndani ya chama hicho.
“Ninapata shaka kwa sababu hata baada ya kupita Katibu huyu alishindwa kuelezea mikakati yake ndani ya chama ya kushughulikia rushwa, kukipeleka chama mbele, kuondoa upendeleo ikiwamo na kushinda vishawishi,” alisema mjumbe huyo.

Mjumbe mwingine ambaye naye kutaka kutajwa jina lake gazetini alisema Katibu Mkuu huyo hafai kwa kipindi hiki kwa sababu hajawahi kugombea hata mara moja nafasi ya siasa zaidi ya kuwa muumini wa Ukawa.

“Lakini pia pamoja na kuwa muumini wa Ukawa anaweza kuangushwa na ugeni wake hivyo nina shaka kama ataweza kusimamia ushirikiano huo anaouamini,” alisema mjumbe huyo.
Mjumbe mwingine aliyedai kuwa Mbowe alikuja na jina moja kwenye kikao hicho, alisema Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ndiye alistahili kushika nafasi hiyo kutokana na kuwa na sifa na vigezo vinavyokwenda sambamba na ukuaji wa chama hicho.
“Suala Mwenyekiti kuja na jina moja kwenye CC ilionyesha wazi aliogopa kumshindanisha mtu wake na Sumaye aliyekuwa chaguo la wajumbe wengi na wabunge wenye ushawishi ndani ya chama hicho.
“Sababu ya Mwenyekiti kutoleta jina la Sumaye kwenye CC ilichangiwa na kujua kwamba ni kipenzi cha wajumbe wengi hivyo lazima angetwaa nafasi hiyo, hali ambayo ingempatia wakati mgumu kufanya naye kazi kwa sababu kiongozi huyo ana misimamo na hayuko tayari kuburuzwa,” alisema mjumbe huyo.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alilidokeza RAI kwamba iwapo wajumbe wangefanikiwa kumkataa mtu aliyependekezwa na Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba hata mwenyewe alitakiwa kuachia nafasi yake.
Mjumbe mwingine alifichua kuwa sababu iliyowafanya wambane ilichangiwa na kukiokoa chama katika kosa ambalo lilifanyika katika uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu.

“Hatukutaka Mwenyekiti arudie kosa alilolifanya kwenye uteuzi wa Mwalimu kuwa Naibu Zanzibar kazi ambayo imemshinda kwani hajafanikiwa kusambaza chama visiwani humo zaidi ya kuwa chanzo cha migogoro,” alisema.
Aliongeza kuwa kutokana na urafiki wake na Mwenyekiti alimteua kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu na matokeo yake alikumbwa na malalamiko ya kukosa uadilifu.
Kabla ya Mbowe kuja na jina la daktari awali alihusishwa na kutaka kumpendekeza Mwalimu kushika nafasi hiyo.
Pia ilielezwa kuwepo kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu walikuwa wakimpendekeza, Sumaye kuwa Katibu Mkuu.
Miongoni mwa waliokuwa wakitajwa kumpendekeza Sumaye ni Profesa Mwesiga Baregu, Lissu na Mbunge wa Iringa, Mchugaji Msigwa.
Wengine ni pamoja na Makamu Mwenyekiti bara, Profesa Abdallah safari, Makamu Mwenyekiti zanzibar Said Issa, Anthony Komu na  Benson Kigaila na Katibu Mkuu Baraza la Wanawake (Bawacha), Grace Tendega.
Katika orodha hiyo pia wamo wabunge wenye ushawishi mkubwa ambaye ni Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.
Yumo Mbunge wa zamani wa Ilemela, Ezekia Wenje na baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama.Hata hivyo akitoa ufafanuzi kuhusu katibu huyo, Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene ametetea uteuzi wa Katibu huyo huku akimpinga Naibu Waziri wa Afya, Dk. Khamis Kigwangalah aliyeandika katika ukurasa wake wa Facebook kumponda Dk. Mashinji.

Katika ujumbe wake huo, Dk. Kigwangalla aliyekiri kusoma na Dk. Mashinji amedai kuwa hana uzoefu wa kutosha katika siasa.
“Kingwangalla ambaye ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amedai kuwa Katibu Mkuu Mashinji hakuwahi kuwaokoa yeye na watu wengine walioshiriki mgomo wa madaktari mwaka 2005 wala hakuwahi kuongoza mgomo huo, lakini hapo hapo anajikanganya kwa kukiri kuwa Katibu Mkuu mgomo huo huo,” alisema Makene na kuongeza:

“Kingwangalla awaambie Watanzania ni akina nani waliowaokoa interns (akiwemo yeye Kingwangalla) waliogoma mwaka huo mwezi Februari?”

Akifafanua zaidi, Makene alisema kumbukumbu zinaonesha kuwa baada ya wanafunzi waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo (interns) kugoma ilikuwa imeamriwa wafukuzwe na wanyang’anywe leseni, hivyo viongozi wao kama akina Erasto Ngonyani, Dk. Mashinji na wengine wakaamua kugoma ili kuwaokoa wasifukuzwe.

“Kama Naibu Waziri haujui ukweli kuhusu Dkt. Mashinji na msimamizi wake, asikimbilie kuandika kitu asichokijua na kujishushia hadhi.

“Tumsaidie. Wala asiende mbali. Amtafute Katibu Mkuu wa Wizara yake, atamsaidia kupata ukweli ili siku nyingine aandike kwa usahihi.

“Tumshauri tena Kigwangalla, kama daktari wa binadamu kwa taaluma aheshimu taaluma yake. Pia ajikite katika majukumu aliyopewa. Bado kuna ‘vilio vingi’ katika wizara yake, ambavyo haviwezi kumalizwa kwa staili ya kutumbua majipu bali uongozi wenye dira na maono (Mabadiliko),” alisema Makene.