Home Makala Kimataifa Afrika kusini kufuta Manaibu waziri

Afrika kusini kufuta Manaibu waziri

1089
0
SHARE

Rais Jacob ZumaNA HILAL K SUED

SERIKALI ya Afrika Kusini imetakiwa kuondoa cheo cha naibu waziri kwenye orodha ya viongozi wa serikali ili kubana matumizi.

Hatua hiyo inatokana na hali mbaya ya kifedha inayoikabili serikali ya nchi hiyo.

Wito huo umetolewa na wasomi na wanasiasa wa nchi hiyo. Msomi wa sheria  wa  Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Johannesburg anayeshughulika na masuala ya jamii, Paul Kaseke amekuwa miongoni mwa watu waliopendekeza kuchukuliwa kwa hatua hiyo.

Hoja inayobeba dhana hiyo, inachagizwa na madai kwamba kuwapunguza au kuwaondoa kabisa manaibu mawaziri kutaisaidia serikali kubana matumizi.

Hivi karibuni serikali ya Afrika Kusini ilibainisha hatua kadhaa itakazotumia  katika kubana matumizi.

Hatua hiyo ni pamoja na punguzo la Rand 7 bilioni (Dola za Marekani bilioni 4.7b) katika fungu la mishahara kwa watumishi wa umma katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, ikijumuisha punguzo katika gharama za usafiri, posho za burudani, vinywaji na gharama za mikutano na makongamano.

Ubanaji huu wa matumizi unatokana udhaifu wa sarafu ya nchi hiyo (rand) pamoja na kupungua kwa pato la serikali katika kuendesha shughuli zake.

Aidha, ni mwitikio wa ripoti chafu ya Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu za Serikali iliyobainisha wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma uliofikia Rand 25.7 bilioni mwaka 2015.

Ubanaji huu wa matumizi ya serikali umesifiwa na wananchi wengi, lakini wanasema umepuuza sehemu moja ya matumizi ambayo serikali inaweza kuachana nayo bila ya athari yoyote kwake.

“Manaibu waziri wanaweza kufutwa, ingawa siyo suluhisho la tatizo lakini kuwaondoa hawa au kuwapunguza kutaisaidia sana serikali katika kuweka mapato yake katika hali nzuri.”

Wachambuzi wa mambo wanasema wakati Rais Jacob Zuma anaanza kipindi chake cha pili cha uongozi aliteua mawaziri 35 na manaibu waziri 37, uteuzi ambao ulichangia Baraza lake la Mawaziri kuwa kubwa.

Russia kwa mfano ina baraza la mawaziri la watu 23 tu, China 20, Botswana 17 (na manaibu waziri 7), wakati Nigeria ni mawaziri 31 tu.

Hakuna atakayejali ukubwa wa baraza la mawaziri iwapo hii haitasababisha kuwepo kwa gharama kubwa kwa serikali. Kila naibu waziri analipwa rand 902,729 kwa mwaka ambazo ni sawa na dola za Marekani 608,000, sawasawa na Spika wa Bunge.

Kwa ujumla wao serikali hulazimika kutenga kiasi cha rand 70.3 milioni kwa ajili ya mishahara ya manaibu waziri kila mwaka, bila kujumlisha posho nyingine.

Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema kuokoa rand bilioni 70 kwa kuwafyeka manaibu waziri ni kama vile unaondoa tone la maji kutoka baharini kutokana na bajeti kubwa ya rand trilioni moja ya nchi hiyo, lakini kila senti moja ya nchi inayookolewa inahesabiwa.

Hata hivyo hoja kubwa inayoakisi matakwa hayo ya kuwaondoa manaibu waziri ni kukosa kwao umuhimu.

Wengi wanajiuliza ni nini kazi ya hawa manaibu waziri?

Swali hilo linajibiwa kwa hoja kwamba majukumu ya manaibu waziri, kama vile mawaziri kamili imeainishwa katika Katiba, lakini wengi wanaamini kwamba manaibu waziri ni sehemu ya Baraza la Mawaziri na Muhimili wa Dola. Jambo ambalo si la kweli.

Kifungu cha 185 cha Katiba ya Afrika Kusini kinasema mamlaka ya dola yako kwa Rais na Baraza la Mawaziri, lakini kutokana na Kifungu cha 91, Baraza la Mawaziri linamjumuisha Rais na mawaziri.

Na kikawaida manaibu waziri huwa hawahudhurii vikao vya Baraza la Mawaziri kwani ni kinyume na sheria na hata kama waziri wake hayupo, hawezi kuwa mbadala.

Kifungu cha 98 cha Katiba hiyo kinamuelekeza Rais kuteua mtu mwingine mbadala, au miongoni mwa mawaziri kukaimu kwa muda nafasi ya naibu waziri anapokuwa hayupo.

Kwa maana hii iwapo naibu waziri atateuliwa kukaimu nafasi ya uwaziri, basi itakuwa kinyume na sheria.

Na hali hii haiko Afrika ya Kusini tu, iko katika nchi nyingi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth) ambazo bado zina utaratibu wa kuwa na manaibu waziri.

Hivi karibuni, Rais wa Zambia alimualika naibu waziri mmoja kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri, lakini alipingwa vikali kwa madai kwamba hatua hiyo ilikuwa ni kinyume na Katiba. Uingereza haina tatizo hili na haina manaibu waziri, sawasawa na Nigeria.

Wakati majukumu na uwajibikaji wa mawaziri umeainishwa katika kifungu cha 92 cha Katiba ya Afrika Kusini, yale ya manaibu waziri yamo katika Kifungu cha 93 na kikubwa kinachotajwa hapa ni katika “kuwasaidia wajumbe wa Baraza la Mawaziri.” Maneno hayo yana maana kwamba manaibu waziri hutegemea Baraza la Mawaziri katika majukumu yao.

Tatizo kuu ni kwamba hakuna kipimo kilichoainishwa waziwazi cha kuhakikisha wanafanya kazi yoyote.

Wakati mawaziri na manaibu wao wanawajibika kwa Bunge na ni mawaziri kamili tu ndiyo wanatakiwa kutoa ripoti zao Bungeni kwa wakati unaotakiwa.

Hivyo ni vigumu kwa Bunge kuwawajibisha manaibu waziri wote 37 pamoja na shughuli zake nyingine kama zile za Bunge, ingawa hawa manaibu waziri wanapokea mishahara mikubwa kuliko wabunge.

Ni dhahiri kwamba kuna baadhi ya manaibu waziri ambao hawana kazi kulingana na mishahara yao minono.

Na kutokana na hii nafasi za unaibu waziri hushikiliwa na watendaji hewa na uwepo wao huonekana tu pale tuhuma za kashfa za matumizi ya anasa ya fedha yanapoibuka. Hivyo ni vyema kuiga nchi nyingine ambazo zimeondoa nafasi hizo.

Tatizo la kukosekana kwa majukumu yalioainishwa ya watendaji hawa yameelezewa katika nchi nyingine. Mfano mzuri ni Kenya ambapo huko nyuma manaibu waziri waliwahi kulalamikia ile hali ya kukaa bila kazi kwa sababu mabosi wao walikuwa hawawapi kazi za kufanya.

Kila idara ya serikali ya Afrika Kusini ina Mkurugenzi Mkuu ambaye ni mtaalamu katika eneo husika. Iwapo waziri atahitaji ushauri wa kitaalamu kuhusu jambo fulani, basi hutegemea kuupata kutoka kwa mtendaji huyo moja kwa moja na si kwa naibu waziri.

Kama vile mawaziri, manaibu waziri pia huteuliwa bali si kutokana na ujuzi wao katika idara husika. Hili hutokea kwa wakurugenzi wakuu tu.

Hivyo basi ni rahisi sana kufuta nafasi za unaibu waziri. Kifungu 93 cha Katiba ya Afrika ya Kusini kinatamka “Rais aweza kuwateua” manaibu waziri (the President may appoint …”). Kwa maana hii halazimiki kuwateua, hivyo anaweza akaamua asiwe na mannaibu waziri kabisa.

Na hii inaonyesha kwamba wale watunzi wa katiba hawakuona kwamba manaibu waziri walikuwa ni watu wa lazima katika serikali.

Hivyo kutokana na malalamiko ya manaibu waziri kuwa walikuwa hawapewi kazi na mabosi wao, Kenya iliamua kufuta nafasi hizo kufuatana na katiba mpya iliyozinduliwa miaka mine iliyopita.

Taarifa hii imetayarishwa kutokan na vyazo mbalimbali vya mashirika ya habari.