Home Habari Abdulrahman Babu kichocheo cha vyama vingi

Abdulrahman Babu kichocheo cha vyama vingi

1077
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA

MARA nyingi, tumeambiwa na wanamapinduzi uchwara kwamba dhana ya demokrasia haizungumziki kwa watu wenye njaa, na kwamba demokrasia maana yake ni shibe; fikra inayoonekana kukosa mashiko, potofu na yenye kudhalilisha utu kwamba demokrasia ni kubwa miongoni mwa waliovimbiwa kwa shibe.

Kwa kisingizio cha kuwa vitani dhidi ya umasikini, njaa na maradhi, tumeambiwa huu si wakati wa uhuru wa mawazo ya kisiasa wala uhuru wa kujieleza. Na kwa kisingizio cha kulinda umoja wa kitaifa, tumetakiwa kuunga mkono bila kuhoji wala kuchangia hoja na mawazo huru na kusikilizwa juu ya mambo ya kitaifa, bali kuunga mkono tu maagizo ya wachache madarakani, kwamba [eti] kuruhusu mawazo yoyote mbadala ni kuligawa Taifa kwa maslahi ya ukoloni mamboleo.

Huo ni utafiti wa Mwanaharakati wa siasa za harakati za ukombozi za kimataifa na Waziri wa zamani wa Uchumi na Mipango wa Tanzania Abdulrahman Mohammed Babu, katika barua aliyomwandikia Baba wa Taifa na [wakati huo] Rais Mstaafu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1990 kuelezea namna udikteta unavyoshamiri miongoni mwa nchi za Kiafrika, kwa watawala madikteta kujificha nyuma ya pazia la vita vya uchumi na umoja wa kitaifa kuua demokrasia ya kweli.

Kipindi hicho, Mwalimu alikuwa ameng’atuka Urais lakini bado alikuwa Mwenyekiti wa Chama [tawala] cha Mapinduzi [CCM] ambapo tetesi zilisikika kwamba Chama hicho kilikuwa na mpango wa kuibua kwa mjadala mpana, agenda ya “kuanzisha mfumo wa Utawala wa vyama vingi vya siasa. Babu akaendelea kusema: “Kwa udikteta huu, Afrika imepungukiwa uhuru wa ndani kisiasa na kiuchumi na kufifia kwa haki za msingi za raia kama vile uhuru wa mawazo na wa kujieleza, uhuru wa kushiriki na ushiriki katika mambo ya nchi, uhuru wa imani, haki ya usalama na ya kuishi na hivyo kukithiri kwa ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Barua hiyo yenye maono, ya Februari 1990, ilianza hivi: Ndugu Mwenyekiti, twende moja kwa moja kwenye hoja. Kuna tetesi kwamba Chama cha Mapinduzi [CCM kinatarajiwa kufanya semina kwa vigogo wa Chama, kujadili maendeleo [ya kisiasa] barani Ulaya na kutathmini madhara yanayoweza kutokea Afrika. Watanzania wengi wa kawaida watapenda kuchangia mawazo juu ya jambo hili, mradi tu mkutano huo hautakuwa mmoja wa mikutano ya faragha iliyozoeleka; mikutano ya siri ya ndani ya Chama, inayohudhuriwa na wateule wachache.

Gwiji hilo la siasa za mapambano kwa mrengo wa Kisoshalisti/Kikomunisti na mmoja wa wanamikakati wakuu wa Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, alisema: “Matukio haya barani Ulaya yanatia hamasa Watanzania kwa sababu yanatokea katika nchi za Kisoshalisti chini ya tawala za Chama kimoja ilivyo Tanzania. Kwa sababu hii tunapaswa kujifunza mengi kukidhi usemi wa kale, kwamba, “mwenzako akinyolewa wewe tia [nywele zako] maji”.

“Nimefanya tafiti kuona nini Watanzania wanafikiri juu ya yote haya na kubaini kwamba wana hoja ya msingi kuhusiana na siasa zetu za ndani, kwamba lazima tujifunze somo namna jamii zetu zinavyopaswa kutawaliwa; uhusiano kati ya watawala na watawaliwa; namna madaraka yanapaswa kugawanwa na nani agawe madaraka hayo. Na juu ya yote, wanaridhika na kukubali nguvu ya mabadiliko kwa kuzingatia “nguvu ya umma”, japo wengi hawakubaliani na jinsi Rais wa zamani wa Romania, Ceausescu alivyouawa kwa kunyongwa kwa nguvu ya umma iliyopotoka au kupitiliza..

“Somo tunalojifunza kwa matukio haya ni pamoja na kwamba, kuna umuhimu mkubwa na wa haraka kubadili mwelekeo wa siasa zetu, kwamba mfumo wa Chama kimoja uliwatenga Viongozi na wananchi wasijue nini [wananchi] walitaka, nini [Viongozi] walitakiwa kutekeleza na hivyo kujenga chuki dhidi ya watawala. Licha ya kuwepo mtandao mkubwa wa “shushu”, Polisi wapelelezi na watoa taarifa, bado Viongozi walibakia gizani [kwa jeuri ya Chama na madaraka] kutoweza kujua yaliyotakiwa kwa wananchi na nchi.

“Kilichochukiwa na kushambuliwa na wananchi katika nchi hizo sio mfumo wa haki za kijamii

[wanaouthamini]

, bali mfumo wa Serikali uliowanyima haki zao halali katika siasa nchi na uchumi wake – mfumo uliozaa rushwa, upendeleo, tija duni, ubabe kwa njia ya “maagizo toka juu”, na hatimaye, utawala wa mtu mmoja.

“Chama cha Mapinduzi kitakuwa kinafikiria kwa makini nafasi yake kama Chama turufu nchini. Wakati miaka ya 1960 Chama cha Tanganyika African National Union [TANU] kilikuwa vivyo hivyo Chama turufu kwa iliyokuwa nchi ya Tanganyika, CCM, bila kujaribiwa [kujipima] katika uchaguzi huru kwa kushindanishwa na Vyama vingine, hakiwezi kudai kwa haki ubora wa kisiasa machoni mwa Watanzania wa miaka ya 1990.

Babu akaendelea kuelezea kwa kutoa mifano, akisema: “Matukio Visiwani Zanzibar, kwa mfano, kufukuzwa kwa wanachama waandamizi kwenye Chama; kukamatwa na kufungwa kwa Wazanzibari wengi “wasaliti” akiwamo Seif Sharrif Hamad na wenzake wengine; maandamano ya kisiasa dhidi ya Chama Visiwani Pemba na Zanzibar; mitafaruku ya kidini dhidi ya CCM na kuharibiwa kwa mali za Chama hicho; na mengine, ni ushahidi wa kuwepo mikondo ya upinzani dhidi ya CCM – Na vivyo hivyo Tanzania Bara.

“Mikondo hii lazima ipewe uhalali wa kujiibua kuweza kujilea na kujikuza yenyewe hata kama ni kwa chukizo kwa wengine, lakini ukweli kwa yanayotokea kwa msukumo wa nyakati na mazingira udhihirike. Jaribio lolote la kuyazuia linawea lisifanikiwe na huenda likazaa machafuko kama yale tunayoshuhudia Ulaya Mashariki.

“Wala haina mantiki, na kusema kweli, ni upunguani, kuyaita matukio hayo kazi ya “maadui wa umma”, au “mawakala wa ubeberu wakiitika Sauti ya Bwana wao”, au vibwagizo vya aina hiyo kuweza kupigiwa makofi ya kinafiki”.

Akielezea kuwa upinzani sio uadui au usaliti kwa nchi, Babu alisema, “Kukipinga CCM haina maana ya kuwa msaliti kwa nchi yako. Ukweli, wasaliti wa nchi chini ya mfumo wa Chama kimoja huona rahisi kuficha uzandiki wao kwa kujifanya watiifu wakubwa kwa Chama ili ama wauze nchi au wapore rasilimali [utajiri] zake

“Kimataifa, kuna kila dalili kuonesha kwamba miaka ya 1990 itakuwa miaka ya kutoka jasho kwa nchi masikini, hasa barani Afrika. Umasikini barani Afrika utaongezeka wakati idadi ya watu wake ikikaribia kufikia bilioni moja mwishoni mwa karne [2000]; Tanzania pekee ikizidi milioni 35 na Dar Es Salaam kulemewa na idadi ya wakazi milioni 2 wakigawana huduma duni za jamii.

“Kukabiliana na changamoto za miaka ya 1990, tunahitaji Taifa la watu huru kwa kuanzia – waliokombolewa kutoka minyororo ya “maagizo” ya Chama na mbwembwe za watawala wenye kujiona kuliko wananchi; watu huru kutokana na jicho onevu la “shushushu” na wapelelezi wa Jeshi la Polisi na watoa habari ambao ndio mhimili wa mfumo wa Chama kimoja kwa ukatili mkubwa, usiohojika; watu huru kutoka unyonyaji wa kiuchumi kutokana na udhaifu wa wafanyakazi na wakulima kupokonywa uhuru na uwezo wao kisheria kuwawezesha kuendesha harakati za kupata mgawo wa haki wa utajiri wa nchi. Watu wawe huru kujiunda wenyewe kisiasa; wawe huru na makucha ya Chama tawala; wawe huru kuibua hadharani makosa na matumizi mabaya ya madaraka kwa vigogo wa Chama ili kuuelimisha umma uweze kuwadhibiti watawala wabovu.

Akamshauri Mwalimu, akisema: “Kama tunataka kuwa washiriki kwenye jukwaa la dunia, na kulinda nafasi yetu kuepuka kuwa wahanga wa kudumu wa matendo ya wengine, lazima kwanza, kabla ya yote, tusahihishe mapungufu yetu ya ndani kuweza kufungua minyororo na nguvu ya watu wetu katika Nyanja zote za maisha kama nchi, na kwa kufanya hivyo watashiriki vyema katika kuokoa/kuisalimisha nchi”.

“Kama CCM kinataka kusalimika kama chama cha siasa na kutekeleza wajibu wake, kinapaswa kuwa na maono kwa kuacha kuhodhi madaraka na kuruhusu wengine kuwa huru kuunda vyama vya siasa wapendavyo. Hapo kitaweza kupata “mpiga kengele” kukiamsha kutoka usingizini na ulevi wa madaraka uliokifanya kijitenge na wananchi na kupoteza mwelekeo na dira kwa yale ambayo kinapaswa kutekeleza na kusababisha nchi kukosa hamasa ya maendeleo, ufanisi na tija; kwamba ilivyo sasa Chama kipo tu kwa sababu ya kubebwa na dola. Muda wa kutenda ni huu, na kwa mara ya kwanza katika historia ya kileo, kitovu cha siasa za kiharakati zinahama haraka kutoka Ulaya kuja katika nchi zetu. Tuwe tayari.

“Ndugu Mwenyekiti, haya ni mawazo ya Watanzania walio wengi, baadhi yao ni wanachama wa CCM, wengine kama mimi, sio wanachama. Lakini wote kwa ujumla wana matumaini kwamba, tathmini ya Chama ya hali halisi ya ndani na ya kimataifa itatoa matokeo chanya kwa manufaa ya Watanzania wote”. A. M. Babu.

Kwa kiasi gani Mwalimu aliyazingatia maneno/mahubiri ya Babu juu ya: kushamiri kwa udikteta kwa kificho cha vita ya kiuchumi isiyojua wala kuvumilia uhuru wa hoja na majadiliano; kwamba, maendeleo ya Afrika yaliendelea kushuka na umasikini kukithiri kwa sababu ya udikteta wa Chama kimoja; kwamba sauti zilizoanza kujitokeza Bara na Visiwani juu ya demokrasia ilikuwa ishara ya yaliyotokea Ulaya Mashariki kufikia “nguvu ya umma” kunyonga Viongozi madikteta akiwamo Rais Ceausescu wa Romania.

Kwamba CCM kililala usingizi na kiliishi kwa kubebwa na dola na hivyo kwamba yalitakiwa mabadiliko haraka kukiamsha kuepusha nchi kutokana na yaliyokuwa yakitokea Ulaya Mashariki kuashiria kwamba siku za madikteta na udikteta wa mtu na wa Chama kimoja zilikuwa zikihesabika na kupita haraka sana.

Miaka kumi kabla ya hapo, Mei 1980, Babu aliwahi kumwandikia barua kama hiyo, Waziri Mkuu [mpya] wa Zimbabwe, Robert Mugabe kufuatia uhuru wa nchi hiyo, kumhubiria na kumtahadharisha juu ya majukumu yake ya mbele kwenye nchi hiyo ambayo rasilimali na uchumi wake ulihodhiwa na Masetla walowezi wa Kizungu. Alimuonya kutopaparika na njia rahisi lakini yenye kutibua uchumi, ya kubinafsisha njia kuu za uchumi [mashamba makubwa, Viwanda n.k.] akasema, “Ni rahisi kutamka hilo lakini lina hatari kubwa, bila kujiuliza: Wapi pa kuanzia?. Kisha akaendelea kumshauri akisema, “Kubinafsisha ghafla mashamba makubwa ya Masetla wakati nchi haijajijengea utaalam wa kutosha na mitaji ya kuyaendesha kutasababisha majanga haraka. Lakini pia kuwaruhusu pia kuendelea kunyonya kama mwanzo kutamaanisha kuendeleza dhuluma kwa Taifa. Yote haya yanaweza kuepukwa kwa pamoja na kwa mpigo, alisema.

Alishauri akasema, “Yaache yaendelee; lakini, pale inapowezekana hakikisha yanazingirwa na Vyama vya Ushirika vya Kilimo vya uzalishaji mali [AMCOs]; pili yashurutishe mashamba ya Masetla, kama sharti muhimu, kutumia pamoja na Vyama vya Ushirika vipya, huduma zake za mashamba [zama za kilimo, utaalam, masoko, zahanati n.k.].

“Hii itasaidia, kwanza, kuendeleza mashamba ya Vyama vya Ushirika vyenye nguvu kwa gharama ndogo. Pili, itasaidia kuweka sawa mzania kati ya uzalishaji wa kisetla na uzalishaji wa kiushirika na kuondoa ile dhana potofu ya kuyaona mashamba ya Masetla kama Visiwa vyenye ukwasi katikati ya umma masikini. Lengo pia ni kuona hatimaye uzalishaji wa kiumma unachukua nafasi hiyo.

“Tatu itasaidia kupambanua kati ya Masetla wema waliotayari kufanya kazi na Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, na wale wafia ubaguzi wa rangi na kiuchumi na kuwachuja.

“Nne, na hili ni muhimu sana; itasaidia kuunganisha, kuimarisha na kupanua uzalishaji wa umma, tofauti na uzalishaji binafsi, bila kuathiri uzalishaji uchumi mkubwa

[na madhara yake makubwa kimatokeo]

katika kipindi hiki cha mpito”, alishauri Babu, huku akionya vikali dhidi ya mtizamo usio na mashiko, wenye kuthamini uzalishaji mdogo akisema, “Hakuna nchi iliyopata kuendelea kwa mfumo huo; labda njia nzuri itakuwa karibu na hiyo ni kuchanganya uzalishaji wa kilimo kikubwa na kilimo cha kati na kuachana na kilimo kidogo kisicho na tija”.

Mugabe hakuzingatia ushauri wa Babu, badala yake alinyakua mashamba yote ya wazalishaji wakubwa na kuwagawia wazalendo, wengi wao Viongozi na wapiganaji wenzake wa vita vya uhuru. Uzalishaji ukafa; mashamba yakageuka misitu; uchumi ukayumba, kisha ukaporomoka na njaa ikaandama Taifa. Mwisho wa yote, machafuko ya kisiasa na kiuchumi yakamea na kuzaa mitafaruku iliyomwondoa Mugabe madarakani.

Mwalimu alimfahamu vema Babu, kwa uwezo wake kifikra na kimaono pamoja na mchango wake katika ujenzi wa Taifa kuonekana lilivyo. Bila shaka hakutaka kupuuza ushauri huo, kama alivyopuuza Mugabe.

Katika hoja zake za kutetea kuanzishwa kwa Mfumo wa utawala wa vyama vingi vya siasa, japo yeye mwenyewe alikuwa Mwasisi na mtetezi wa Mfumo wa chama kimoja tangu mwaka 1965, alikuwa na haya ya kusema kama vile kurudia tu ushauri wa Babu:  Kwamba, CCM, chama ambacho kilipaswa kuwa zana ya maendeleo ya watu na kielelezo cha uhuru wa wananchi kimekengeuka kwa malengo, sasa hivi kipo tu kwa ajili ya chaguzi za kisiasa. Akasema, kipo kipo tu kwa sababu tu kinalindwa na sheria na dola inayopiga marufuku upinzani, “Kukosekana kwa upinzani unakifanya Chama kilale usingizi juu ya uwapo wake halisi na uwepo wa kufikirika”, alisema.

Akahoji, “Je, CCM kinaweza kusimama kupambana na upinzani?. Nchi haiwezi kuendelea kuongozwa na Chama ambacho kukubalika kwake kunatokana na kulindwa kwa upendeleo wa sheria; vinginevyo, kisingelindwa na sheria kidola, mambo yangekuwa tofauti”.

Kwamba, kwa kuwa uwepo wa CCM kama Chama tawala unalindwa na sheria, hivyo Chama hiki kina kila sababu ya kujadili juu ya uwezo wake wa ndani na udhaifu, na kuibua fikra mpya juu ya uwepo wake katika mazingira ya siasa za ushindani. Alihoji, “…..CCM kinakabiliwa na mkanganyiko wa kimadaraka na wa kutojali yanayoendelea nchini; vipi Chama hiki kitaweza kuongoza Tanzania kwenye vita vya uhuru kiuchumi?. Kama hakiwezi, kwa nini kisiibuke Chama kingine?.

Akasema: “Mfumo wa vyama vingi, kwa mazingira ya sasa, hauepukiki; tunapita kwenye mabadiliko na mabadiliko lazima yaongozwe. Ni lazima CCM kisimamie mabadiliko haya bila ukiritimba na kujipendelea, vinginevyo kitajitia kitanzi chenyewe.

Mwalimu aling’atuka uongozi wa nchini kama Rais mwaka 1985 na kutumia muda mwingi “kufufua” Chama [CCM] kilichokuwa kikipoteza mng’aro ambacho aliendelea kuwa Mwenyekiti wake hadi mwaka 1990, chini ya Mradi wa “Uhai wa Chama”. Aliweza kukutana na wanachama mashinani na kufungua macho kumfanya afahamu kuwa Chama kilijiendesha kwa njozi za “Ukuu wa Chama” na kwa kujiweka mbali na umma wa wadunda kazi huku ufa wa kitabaka, kati ya wenye ukwasi na “mafukara” wa nchi ukipanuka kwa kasi ya kutisha mikononi mwa Chama.

Ni Mwalimu ambaye mwaka 1962 aliwaambia Watanganyika kwamba, Tanganyika [Tanzania] haikuhitaji vyama vingi vya siasa kwa sababu hapakuwa na matabaka. Akasema, ikitokea kuzuka kwa matabaka, haikwepeki, vyama [vingi] vya siasa vitaundwa, na ikiwa hivyo, basi, itamaanisha kwamba TANU [Chama kimoja] kitakuwa kimeshindwa kuongoza.

Je, Mwalimu, kwa kuibua Agenda ya Mfumo wa vyama vingi, alimaanisha kushindwa kwa CCM kuongoza nchi?. Au alitishwa na yaliyokuwa yakitokea Ulaya Mashariki dhidi ya udikteta wa Viongozi na wa Chama kimoja na kwa maono ya Mwanaharakati wa siasa za kimataifa, Abdulrahman Babu?. Je, kwa maono haya na kwa yanayotokea, Afrika imepiga hatua gani kwenye Nyanja za demokrasia na utawala bora kuepuka historia kujirudia na kuzua kile Babu alichokiita vita ya Ukombozi Awamu ya pili?.