Home Makala ACACIA NA UTAYARI WA KUSHIRIKIANA NA RAIS MAGUFULI

ACACIA NA UTAYARI WA KUSHIRIKIANA NA RAIS MAGUFULI

1431
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU,

SAKATA la mchanga wa dhahabu (makinikia) limeendelea kuchukua sura mpya baada ya Kampuni ya Acacia Mining kusema ipo tayari kushirikiana na serikali katika kujenga kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia hayo. RAI linaripoti.

Taarifa hiyo imekuja ikiwa ni wiki chache zimepita baada ya Rais John Magufuli kupokea ripoti ya kamati ya kwanza uchunguzi wa makotena 277 yaliyosheheni makinikia ambayo pamoja na mambo mengine ilibainisha kuwa Taifa linaibiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kutoka nchini Uingereza mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia, Brad Gordon alisema Acacia ipo tayari kushirikiana na serikali katika kuhakikisha mkakati wa upatikanaji wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia kinajengwa nchini.

Katika taarifa hiyo ambayo pia iliripotiwa June 3 mwaka huu na Gazeti la Financial Times la Uingereza, Gordon alisema wako tayari kufadhili utafiti wa ujenzi wa kiwanda cha kuchengua makanikia.

Mkurugenzi huyo alisema Acacia wako tayari kwa hilo ili kutimiza malengo ya Rais Magufuli anayotaka Tanzania inufaike zaidi na sekta ya madini.

Akizungumza na RAI juzi, Afisa Mawasiliano wa kampuni hiyo ya Acacia, Necta Foya, alithibitisha kuwapo kwa taarifa hiyo na kubainisha kuwa ufafanuzi zaidi wa mkutano huo wa waandishi wa habari na Mkurugenzi huyo upo katika tovuti ya Acacia.

Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi huyo, alisema Acacia ambayo inamiliki migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu   huzalisha tani 50,000 hadi 60,000 kwa mwaka wakati mashine za uchenjua huhitaji tani 150,000 kwa mwaka kutokana na teknolojia iliyopo sasa.

Pia alisema mgodi huo wa Buzwagi unatarajiwa kufungwa mwaka huu hivyo kushusha shughuli za uzalishwaji wa makinikia hayo hadi kufikia tani 25,000 kwa mwaka kutoka katika mgodi wa Bulyanhulu pekee.

“Hata hivyo, tunaweza kuangalia teknolojia nyingine au kama serikali itachukua makinikia kutoka nje ili kutosheleza kiwanda hicho, sisi tupo tayari kushirikiana nao,” alisema.

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema ndani ya wiki mbili zijazo, Acacia itakutaka na viongozi wa juu wa serikali ili kuzungumza mambo licha ya kuwapo kwa ukimya tangu ripoti ya kwanza itoke.

Alisema hivi sasa wanasubiri ripoti ya pili ambayo inatarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia sasa.

Tangu Machi mwaka huu Serikali ilisitisha usafirishwaji wa makotena 277 nje ya nchi ambayo yamesheheni makinikia.

Mchanga wa madini uliositishwa huchimbwa katika migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu iliyopo katika mkoa wa Shinyanga. Kutokana na sitisho hilo, wiki iliyopita hisa za Acacia katika soko la London zilishuka kwa asilimia 46.

Aidha, katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mkurugenzi huyo alisema Acacia Mining itawagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 30  kuweka mgodi wa Bulyanhulu katika matunzo na matengenezo baada ya Serikali kuzuia usafirishaji wa mchanga wa madini kuuza nje.

Acacia kwa sasa inapoteza dola milioni 15 kwa mwezi tangu kusitisha kwa usafirishaji wa mchanga wa madini mwezi Machi mwaka huu.

Tangu kamati ya wataalamu wa sayansi iliyoundwa kuchunguza kiwango cha madini katika mchanga uliohifadhiwa katika makontena 277 yaliyoko bandarini Dar es Salaam, iwasilishe ripoti yake, kumekuwapo na sintofahamu  ya kujua nani mkweli katika sakata hili kwa maana ya Serikali ya Tanzania kwa upande mmoja na wawekezaji Kampuni ya Acacia kwa upande mwingine.

Itakumbukwa kuwa katika ripoti iliyowasilishwa kwa Rais Dk. John Magufuli ilionyesha kuwa kiwango cha madini kinachosafirishwa nje ya nchi ni mara 10 zaidi, ikilinganishwa na kile ambacho kimekuwa kikielezwa, Acacia katika matamko yao mawili waliyoyatoa wiki hii imepinga ripoti hiyo.

Acacia inadai kuwa kama kiwango hicho kinachosemwa katika ripoti ya kamati hiyo ni kweli, basi Tanzania ni nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha madini ya dhahabu.

Katika tamko lake la mwanzo, Acacia ambayo inachimba madini katika migodi mikubwa ya Bulyanhulu na Buzwagi, ilieleza kuwa katika kila kontena la mchanga kuna madini ya shaba kilogramu 3,000, dhahabu kilo 3, na madini ya fedha kilo 3 na hivyo kufanya thamani ya kontena moja kuwa ni Sh milioni 300.

Katika ripoti ya Kamati ya Rais Magufuli, inaeleza kuwa katika makontena yote 277 yaliyochunguzwa dhahabu ilikuwa na uzito wa kati ya tani 7.8 na 13.16 zenye thamani kati ya Sh bilioni 676 na trilioni 1.147.

Kiwango hicho ni tofauti na makadirio ya wazalishaji na Wakala wa Serikali wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) ambao walionyesha kuwa katika makontena hayo, dhahabu ilikuwa ni tani 1.2 yenye thamani ya Sh bilioni 97.5 tu.

Kwa upande wa madini mengine kama fedha, katika ripoti aliyokabidhiwa Rais Magufuli ilikuwa ni kati ya tani 1.7 na 1.9 yenye thamani kati ya Sh bilioni 2.1 na bilioni 2.4 wakati TMAA ikidai ni kg 831 zenye thamani ya Sh bilioni moja.

Kuhusu madini ya shaba, kamati hiyo ilibaini kulikuwa na tani 1,440.4 na 1,871.4 zenye thamani ya Sh bilioni 17.9 na bilioni 23.3.

Kiwango hicho ni tofauti na nyaraka zilizopatikana bandarini ambazo zilionyesha kulikuwa na tani 1,108 zenye thamani ya Sh bilioni 13.6.

Hali hiyo ilimlazimu Rais Magufuli kumtimua waziri wa Nishati na Madini pamoja  na kuvunja bodi ya TMAA kutokana na ripoti ya Tume ya Mruma iliyochunguza makanikia ya madini yasafirishwayo nje na kampuni ya ACACIA .

Zitto

Katika siku za karibuni, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), aliwataka wataalamu kukaa na kubuni teknolojia yenye uwezo wa kufanya uchenjuaji kwa kiwango cha mchanga tunachozalisha nchini.

“Haiwezekani dunia nzima ikawa na teknolojia moja tu ya tani 150,000 la hasha. Ushauri wangu ni kwamba Serikali ikae na sekta ya madini ili kupata jawabu la kudumu na kuweka commitment (dhamira ya utekelezaji) ya muda maalumu wa kuendelea kusafirisha mchanga na baada ya muda huo mchanga huo uchenjuliwe nchini kwetu na kuzalisha ajira na kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha.

“Hii sio Zero – Sum game (Kama sio kusafirisha basi hakuna lingine). Hapana. Mjadala unaweza kuleta jawabu lenye faida kwa nchi” alisema.