Home Habari kuu ACT KUIBUKA NA UKAWA YAO

ACT KUIBUKA NA UKAWA YAO

1828
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

BAADA ya kusuasua kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), sasa chama cha ACT-Wazalendo kimeamua kuunda umoja wao ambao unatarajia kuhusisha vyama vyote vya siasa vya upinzani bila masharti.

Umoja huo ambao utajulikana kama United Patriotic Front (UPF) mbali ya kuhusisha vyama vyote vya siasa bila kujali ukubwa na udogo wake, utakuwa na dhamira moja tu ya kusimamia hoja muhimu za kitaifa.

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Yeremia Maganja aliliambia RAI mwanzoni mwa wiki hii kuwa wamechukua uamuzi huo baada ya kuona vyama vya upinzani havina sauti moja hasa katika kusimamia na kupigania hoja za msingi.

“Yapo mambo ya msingi ambayo tunapaswa kuyasimamia kwa pamoja kama vyama vya upinzani, lakini tunashindwa kufanya hivyo kwa sababu hatuna mwamvuli wa kweli unaotuunganisha wote.

“Tutaanzisha umoja huru ambao hautakuwa na masharti na utatoa nafasi kwa vyama vyote vya upinzani kuungana pamoja” alisema.

Alipoulizwa kuhusu Ukawa, Maganja alisema hawana mpango wa kujiunga na umoja huo badala yake wanaiona haja ya kuunda umoja huo ili kusimamia agenda muhimu tu.

“Sisi ni chama kilichosajiliwa, uamuzi wa kujiunga na Ukawa haupo, tunapanga kuvishawishi vyama vya demokrasia kutengeneza muungano ambao tunapozungumzia Katiba, vyama vya kidemokrasia visimame na hilo la Katiba au kama ni kuhusu NEC kutokuwa halali vilevile visimame na hilo kwa sababu tunaona kuwa tume ya uchaguzi haipo huru.

“Katiba yetu haina nafasi ya vyama kushirikiana, hivyo lazima kuwepo na makubaliano ya kusimamia ajenda moja. Sisi hatuachi kupigania masuala mapana ya nchi kama vile kuhakikisha polisi hawashiriki uchaguzi na kuuvuruga kama ilivyotokea.”

MIKUTANO YA KISIASA

Kuhusu kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa Maganja alisema kwakuwa uwezekano wa vyama vya siasa kuendelea kufanya siasa za majukwaani haupo wao wameamua kuisaka haki hiyo mahakamani.

Alisema wanatarajia kufungua kesi ya Kikatiba wakiitaka mahakama kutoa tafsiri ya katazo hilo lililotolewa na Rais.

Uamuzi huo unakuja baada Rais  Dk. John Magufuli kuwataka wanasiasa kuachana na ushindani wa kisiasa majukwaani badala yake wachape kazi ili kuwatumikia wananchi hadi mwaka 2020.

Agizo hilo lilitolewa Juni 24, 2016 na kusisitiza kuwa ni vema sasa wanasiasa wakachapa kazi hadi baada ya miaka mitano kuisha ili wananchi wawahoji wanasiasa kama wametekeleza yale waliyoyaahidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM alisema; Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi kama tumeyatekeleza au hatujayetekeleza.  Kila nchi hata zile zilizobobea kwenye demokrasia unapokwisha uchaguzi unakuwa ni wakati wa kazi,” alisema.

Alisema tayari ACT – Wazalendo imeshaiagiza  Kamati ya Sheria ya chama hicho kuandaa utaratibu wa kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya  Dar es Salaam ili kupata tafsiri ya kikatiba juu ya mambo mbalimbali ikiwemo kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Muganja alisema tayari wameshaanza kukamilisha mambo yote muhimu na muda wowote kuanza sasa wanatarajia kufungua rasmi kesi hiyo.

“Tumepanga kwenda mahakama kupata tafsiri ya kikatiba kuwa kwanini Mwenyekiti wa CCM amezuia mikutano ya kisiasa. Tunataka tupate tafsiri ya kikatiba, hayo madaraka anapewa na nani, tupate mwelekeo.

“Ili tutakapokwenda kwenye uchaguzi 2019, 2020 kama watafanya wanayoyafanya na mahakama imeshatuelekeza, basi CCM akinipiga fimbo na mimi nitampiga fimbo halafu nione nafasi ya polisi ambayo kazi yake ni kulinda raia na mali zao. Kama wakikimbia na sanduku la kura kama wanavyofanya tutamkimbiza na kumkamata na sisi tutapambana nao vilivyo,” alisema.

Alisema kimsingi ACT imelekeza kamati yake ya kisheria kuwasiliana na wanasheria wengine ili kuandaa jalada linalokubalika kisheria kufungua kesi Mahakama kuu.

“Mahakama itupatie tafsiri ya mambo hayo kama kuzuia mikutano ya hadhara, maandamano na mambo mengine yote ambayo ni haki za raia kisiasa, kijamii na kiuchumi.

“Hatujaipa muda kamati hiyo kwa sababu kwa mujibu wa taratibu za ACT tunawaambia tu mkikamilisha mtuletee na sasa kamati inatafuta references (rejea) mbalimbali katika sheria mbalimbali na ili yote hayo yaweze kukusanywa yanahitaji muda, ingekuwa ni maamuzi ya haraka bila shaka kamati ingeagiza wafanye siku saba na kuendelea, ila kwa kuwa ni muda umepita naamini wapo kwenye hatua nzuri ya kufungua hiyo kesi,” alisema.

KESI ZA KIKATIBA

Uamuzi huo wa ACT- Wazalendo hautakuwa wa kwanza kuibuliwa, mwaka 2016 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilifungua kesi katika Mahakama Kuu ya Mwanza wakitaka mahakama hiyo itangaze amri ya jeshi la polisi kuzuia mikutano ya hadhara kuwa ni batili.

Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2016, ilisimamiwa na mawakili watatu Gasper Mwanalyela, John Mallya na Paul Kipeja.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema sababu za kufunguliwa kwa kesi hiyo ni baada ya kuona demokrasia ya vyama vingi “inabakwa nchini.”

Watu waliotajwa katika kesi hiyo ya madai ni Kamanda wa Polisi wilayani Geita, Kamanda wa Polisi wilayani Kahama, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa polisi (Makao Makuu) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema wadaiwa hao wamefunguliwa kesi kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa nchini, kwa kuchukua maamuzi ambayo hayaendani na demokrasia.

“Tunaiomba mahakama itangaze amri ya jeshi la polisi ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ni batili, utekelezaji unaofanywa ni batili, polisi wapewe tangazo la kutowanyanyasa wapinzani na pia itoe amri ya vyama vya siasa kufanya mikutano yake na polisi wawe walinzi wa mikutano hiyo,” alisema Mbowe.

Mwishoni mwa mwezi uliopita zaidi  ya wanasheria 20 wakiongozwa na Fatma Amani Karume na wanaharakati kutoka asasi mbalimbali nchini, walitangaza dhamira ya kufungua mashauri 10 ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Kati ya mashauri hayo 10, mawili yameshafunguliwa, shauri la kwanza likihusu kutetea haki ya mpigakura, mlalamikaji akiwa ni Bob Chacha Wangwe na wakili wake ni Fatma Karume.

Mratibu wa umoja huo, Dk. Makongoro Mahanga, aliwaambiwa Waandishi wa Habari kuwa shauri hilo namba 6 linapinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Uchaguzi vinavyotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwaidhinisha wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi, huku wakiwa ni maofisa wa tume hiyo.

Kuhusu shauri la pili namba 04/2018 ambalo nalo tayari limefunguliwa Mahakama Kuu, Dk. Mahanga alisema linapinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi.

Aliwataja walalamikaji katika shauri hilo ni Francis Muhingira Garatwa, Baraka Mwago na Allan Bujo Mwakatumbula wanaotetewa na Wakili Jebra Kambole.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika kuhusu namna demokrasia inavyokandamizwa, uhuru wa kujieleza na wa kufanya siasa.

“Sasa tukaomba msaada kwa wanasheria na wakawa tayari kutusikiliza, tukaanza kujumuika nao, wamekubali kutusaidia bure.

“Tukakubaliana ndani ya miezi miwili kupeleka kesi kama kumi za kikatiba Mahakama Kuu na ziendeshwe ‘live’ kwa sababu zitavutia sana wengi.

“Tunapozungumza hapa tayari tumeshafungua hizo kesi mbili, tutaendelea kufungua nyingine kadiri tunavyoandaa. Hizi mbili ambazo tumezifungua tunasubiri zipangiwe tarehe na majaji,” alisema Dk. Mahanga.

Alisema wameamua kufanya hivyo lengo likiwa ni kuzipigania haki za kisiasa na kidemokrasia kwa kuzingatia misingi mikuu ya kikatiba na kisheria.

“Katika umoja huu tupo wanasiasa, wanaharakati, mawakili na wanasheria mbalimbali kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinachoongozwa na Dk. Hellen Kijo-Bisimba, Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kinachoongozwa na Tundu Lissu na Kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu (THDC) kinachoongozwa na Onesmo ole Ngurumwa.

“Umoja wetu sisi watu 28 wa kada mbalimbali za kitaaluma ambao ni watetezi na wanaharakati wa haki za kisiasa tunaopigania haki za kisiasa nchini kupitia movement yetu ijulikanayo kama ‘Tunadai Demokrasia Yetu’, tumeona tunazo sababu na tunayo heshima ya kufanya kitu kwa ajili ya taifa letu,” alisema Dk. Mahanga.

Kwa upande wake, Wakili Fatma, alisema ameamua kuungana na wanasheria hao kwa sababu kila uchaguzi unapofanyika kumekuwa na malalamiko.

“Imefika hatua mwananchi anaona kwamba kura yake haina thamani yoyote, matakwa yake hayasikilizwi kwa sababu kuna kitu kinaitwa ‘goli la mkono’.

“Sasa suala likaja nini hasa kinachofanya goli la mkono litokee. Kuna nini hasa kwenye mfumo wa sheria zetu zinazoruhusu ‘referee’ (wasimamizi wa uchaguzi) kiasi kwamba kuna watu wanaweza kusema ‘public’ kuwa wao wana uwezo wa kushinda kwa goli la mkono.

“Sasa mimi nimepewa hiyo kazi kama mwanachama wa TLS na sijaja binafsi, nimechukua hiyo kazi na nimeichukua kuwa ni muhimu sana ili kulinda kura ya kila mwananchi.

“Tutailinda vipi kura? Kwenye mfumo wa nchi Katiba inasema; kila mmoja wetu ana haki ya kujiingiza kwenye mambo ya nchi yake ‘either direct’ au ‘indirect’, na kila mtu ana haki ya kupiga kura na ihesabiwe.

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Ibara ya 21: ‘Raia anayo haki kushiriki kufikia maamuzi ya mambo yanayomhusu yeye au taifa lake’ sasa kama watu wanaweza kupiga goli la mkono haki yako hii imetekwa.