Home Makala Kimataifa AFRIKA BADO TUNAHITAJI DEMOKRASIA YA AINA HII?

AFRIKA BADO TUNAHITAJI DEMOKRASIA YA AINA HII?

1503
0
SHARE

NA RAMADHANI MASSENGA

MIONGO kadhaa imepita toka Afrika iingie katika mfumo wa kidemokrasia. Je, Afrika imepata mafanikio halisi kutokana na mfumo huu wa kidemokrasi ama tunahitaji namna nyingine ya demokrasia?

Toka tuingie katika mfumo huu, si tu Afrika imejikuta bado ikihangaika kupata maendeleo na isionekane kuyapata, ila pia mgawanyiko na mauaji miongoni mwa jamii pia yameonekana kukua.

Kila nchi ya Afrika inapoingia katika uchaguzi, tunajiweka tayari kusikia habari kuhusu mauaji, mateso na machafuko makubwa.

Hayo tumeyashuhudia Kenya, Uganda, Tanzania, Kongo, Burundi na nchi nyinginezo nyingi. Swali la msingi hapa, kama Waafrika tumewahi kukaa kwa pamoja na kujadili mfumo huu kwa makini na kujua namna bora ya kwenda nao kwa kuzingatia uwezo wa watu wetu, elimu yao na uelewa wao kuhusu siasa?

Mara nyingi katika makongamano mengi ya kiuongozi, watu hujadili kukuza demokrasia na njia zake. Sijawahi kuona popote watu wakijadili kama demokrasia ya aina hii tuliyonayo Afrika inatustahili ama tuwe na demokrasia yetu itakayoendana na mazingira na hali ya watu wetu.

Tujadili kwa kina. Pamoja na kuwa na hii demokrasia ya magharibi ambayo wao kwa kutumia taasisi mbalimbali wamekuwa wakiipigia chapuo, je, imekuwa na manufaa gani ya kimaendeleo? Tukiachana na suala la watu kupata nafasi ya kujieleza na kutoa maoni hayo, Afrika inapata manufaa gani ya moja kwa moja?

Hayo maoni ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakidaiwa kuwa ndiyo yatakayokuwa chachu ya maendeleo, je, ni kweli yamekuwa na msaada katika kuchochea hayo maendeleo?

Au yamekuwa maoni ya kukubali kila kitu kutoka kwa watawala ama kupinga kila kitu kutoka kwa viongozi?

Wananchi wengi wa Afrika hawana elimu ya kutosha wala uelewa wa majukumu yao ya msingi katika kuchagua na kuleta mabadiliko katika nchi zao. Wengi wako tayari kumpigia kura mtu kwa sababu ya upole wake, kabila lake, dini yake, pesa zake ama umaarufu wake. Kwa hali hii ya kuwa na watu wanapiga kura kama hisani badala ya kutumia kura kama nyenzo muhimu ya kuweka viongozi makini wa kubadilisha hali ya nchi na maisha yao, bado tunahitaji demokrasia hii tulinayo sasa Afrika?

Toka mfumo wa demokrasi hii uingie, nini kikubwa ambacho Afrika tumekipata zaidi ya kutugawa na kuuza maliasili zetu kwa wageni? Kwa ajili ya vita ya kuwania madaraka, baadhi ya wanasiasa wako tayari kuungana na wageni  ili kuifisadi nchi. Kwa namna hii, hakuna haja ya kujitazama kama Waafrika na kuangalia mfumo mwingine wa demokrasia kwa ajili ya Afrika yetu?

Ni wepesi Waafrika wengi kujidai kuipigania demokrasi hii ya magharibi. Ila wengi wanaosema hivyo wanasukumwa na hisia za kimadaraka na uongozi. Sasa ni wakati umefika Waafrika tujadili kwa kina kwanini wenzetu Wazungu wanatulazimisha sana kuingia katika mfumo huu wa demokrasia.

Katika nchi nyingi za Kiafrika, kuna viongozi vibaraka wa mataifa ya Wazungu walioingia madarakani kwa njia ya kupigiwa kura. Ni hii ndiyo sababu inayofanya Ulaya na Marekani kuipigia kelele Afrika kuingia katika mfumo huu?

Katika mfumo huu wa sasa, tumetengeneza wabunge na wananchi wenye kusukumwa na hisia zao za kichama katika kujadili hoja na kutoa changanuzi katika masuala mbalimbali. Mbunge wa chama ‘A’ anaona udhia kuunga mkono hoja ya mbunge kutoka chama ‘B’ kwa hofu ya kuonekana msaliti ama kukipaisha chama cha mbunge mwingine.

Katika masuala muhimu sana ya kitaifa, wananchi wengi bado wanabaki katika hisia na misimamo ya vyama vyao. Kwa namna hii tunaweza kuijenga Afrika bora na yenye neema? Kwa elimu yetu, aina ya changamoto zetu, aina hii ya demokrasia ina manufaa ya kweli kwetu?

Wazungu hawakutaka Muhamaar Gaddaff akae madarakani. Kwa picha ya haraka watasema jamaa alikuwa dikteta na hafai. Ila tumia akili yako vizuri kuchunguza sababu halisi.

Sababu halisi ya Wazungu kumchukia Gaddaf si kuminya wananchi wake. Sababu halisi ni kiburi cha Gaddafi kuwanyima mafuta ya bwerere na kuamua kumfanyizia.

Kama hoja ingekuwa ni udikteta ama kuminya wananchi wake, mbona Yahya Jammer alikuwa rafiki wa Obama na Marekani? Mbona Jameh inajulikana alichukua mali nyingi za Gambia na kuzificha Marekani? Mbona katika hili Marekani na washirika wake walikuwa kimya? Gambia mbona haikuwahi kuwekewa hata vikwazo na Marekani na mashoga (washirika) zake?

Tunahitaji mjadala mpana utakaoegemea katika aina ya uongozi utakaoinua uchumi na kudhibiti rasilimali zetu. Tunahitaji mawazo makubwa ya kuleta majibu ya aina ya uongozi mwafaka tunaouhitaji Afrika. Tunahitaji kutumia mifano halisi na si porojo za Wazungu katika kupata majibu ya aina ya uongozi tunaoutaka.