Home Habari Agizo la Majaliwa kung’oka na Ma-DC

Agizo la Majaliwa kung’oka na Ma-DC

2816
0
SHARE

 MWANDISHI WETU

AGIZO la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Suleiman Jafo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi wa Utawaka Bora), George Mkuchika, linatajwa kuwa kitanzi kwa baadhi ya wakuu wa wilaya nchini.

Mwanzoni mwa wiki hii, Majaliwa aliwataka mawaziri hao kwenda mkoani Kilimanjaro kutatua tatizo la uhusiano kati ya Mkuu wa mkoa huo Anna Mghwira na wilaya za mkoa huo.

Agizo la Majaliwa linakuja kutokana na kuwapo kwa taarifa za kutokuelawana na wakati mwingine kupishana kwa kauli na maagizo kati ya Mkuu huyo wa mkoa na baadhi ya wakuu wa wilaya.

RAI limeelezwa kuwa ni wakuu wa wilaya mbili tu kati ya sita wa mkoa huo ndio wamekuwa mstari wa mbele kupingana na Mkuu wa mkoa.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kuibua hali hiyo ni wakuu hao wa wilaya kuingiza masuala ya utendaji na siasa za maji taka.

Imeelezwa kuwa wakuu hao wa wilaya, hawako tayati kumuheshimu Mkuu wao wa mkoa, kwa hoja kuwa si mwenzao kwa sababu hazijui vema siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mghwira aliteuliwa kushika wadhifa huo akitokea chama cha ACT-Wazalendo, akiwa ndiye Mwenyekiti wa chama hicho.

RAI limeelezwa kuwa wakuu wa wilaya wanaompinga Mghwira, wanamatamanio makubwa ya ubunge, hali inayowafanya kutumia muda wao mwingi kwenye harakati zao hizo na si kuwahudumia wananchi hali inayompa wakati mgumu Mghwira, ambaye anatajwa kuwa kiongozi mpole mwenye kutumia busara zaidi ya ukali.

“Mazaa (mama) ni mpole sana, hana hulka ya uongozi wa kimabavu na kufokeana, yeye anatumia busara na hekima zaidi katika kuelekeza, hali hiyo inamfanya aonekane ni dhaifu.

“Busara zake hizo ndizo zinawafanya hao wakuu wa wilaya wawili kumdharau na kumwona hana anachojua, wakati wakijua wazi kuwa mama ni jembe kweli kweli,”alisema mmoja wa maofisa wa serikali mkoani Kilimanjaro.

UGOMVI WA ma-DED na ma-DC

Mbali ya kuwapo kwa dharau kati ya baadhi ya wakuu wa wilaya dhidi ya Mkuu wa mkoa, lakini pia RAI limeelezwa kuwa kuna kutokuelewana kati ya Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wao ndani ya mkoa huo.

Imeelezwa kuwa viongozi hao wanadharauliana waziwazi huku kila mmoja akitaka kuonekana bora kwa hoja kuwa wote ni wateule wa Rais.

Baadhi ya wananchi wa Kilimanjaro, wameweka wazi kuwa mvutano huo, hauna tija kwao na badala yake unaweza kuchangia kuvuruga jitihada za mkuu wa mkoa na Rais Dk. John Magufuli za kuwaletea maendeleo wananchi.

RAI limedokezwa kuwa upo uwezekano mkubwa wa agizo la Waziri Mkuu likafuatiwa na kung’olewa kwa baadhi ya wakuu wa wilaya, ambao wanaonekana kujikita zaidi kwenye masuala yao binafsi hasa ubunge kuliko majukumu waliyopewa na Rais, hali inayowasukuma kumdharau mkuu wao wa mkoa.