Home kitaifa AGIZO LA MASAUNI KITANZI KWA MADEREVA

AGIZO LA MASAUNI KITANZI KWA MADEREVA

3562
0
SHARE

Na PENDO FUNDISHA, MBEYA


Jitihada na harakati za kupambana na ajali zimekuwa zikiendelea, kwa miaka mingi sasa serikali imekuwa ikitafuta kila namna ya kuhakikisha madereva wanazingatia sheria za barabarani.

Sheria kadha wa kadha zimetungwa ili kuweka mkazo kwenye utekelezaji wa sheria za barabarani, hata hivyo bado hali inaonekana kuwa tete.

Kutokana na hali hiyo, hivi karibuni Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masaun, alionesha dhahiri kuwa hataki mchezo katika kusimamia utekelezaji wa sheria.

Masauni aliagiza kukamatwa kwa mmiliki wa roli  namba T929 BDF la Kampuni ya Azania Group, baada ya kusababisha ajali iliyoua  watu 15 na kujeruhi 15  katika eneo la mteremko wa mlima Igawilo  Jijini hapa.

Alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya mamlaka husika kujiridhisha na uchunguzi wa awali kwamba gari hilo halikukaguliwa na kukabidhiwa stika ya nenda kwa usalama barabarani pamoja na kutiliwa mashaka kwa uwezo wa dereva wa gari hiyo kwa sababu ajali hiyo ingeweza kuepukika.

Masaun, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani, alisema hayo baada ya kutembelea majeruhi.

Alisema, licha ya gari hilo kufeli breki, lakini  dereva wake alikuwa na uwezo mkubwa wa kulichepusha gari hilo kandokando ya barabara ili lisisababishe ajali kubwa iliyochangia kupoteza uhai wa watu wengi na wengine kupata ulemavu wa kudumu.

“Udereva wa dereva huyu, unatutia mashaka,  na hapa tumeona mmiliki wa gari alivyoshindwa kuwasilisha nyaraka muhimu za gari yake, hivyo natoa maelekezo sasa hivi mmiliki wa hili gari leo hii asilale kwake, wamkamate wamuweke ndani aende akashtakiwe na mahakama itatoa suluhisho, hatuwezi kucheka na watu ambao wanamiliki mali halafu wanahatarisha mali na uhai wa watu wasio na hatia,”alisema.

Alisema, jambo hilo halikubaliki na huo ndio mwendo watakaoenda nao na kamwe hawatawafumbia macho matajiri wala watu wenye majina makubwa, kwani wanachotakiwa kukitekeleza ni kuhakikisha magari na madereva wanaowatumia wanakidhi vigezo na viwango vya usalama barabarani.

Alisema, asilimia kubwa ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo wamesababishiwa kwani maelezo yanaeleza kwamba baada ya roli hilo kufeli brek lilienda kugonga gari ndogo ya abiria aina ya Hiace na kugonga magari mengine manne pamoja na watembea kwa miguu.

Akizungumzia tukio hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa, alisema barabara hiyo ipo kwenye kiwango kizuri na  alama za barabarani zipo kubwa, kinachoonekana ni umakini wa dereva ambaye alikuwa na nafasi kubwa ya kuzuia ajali hiyo isileta madhara.

“Miundombinu ya barabara inaweza kusababisha ajali kwa asilimia 12 tu na asilimia  78 ni makosa ya kibinadamu na hapa tunaona kabisa, barabara hii ni nyembamba, ndefu na inamteremko mkali, alama zinazoelezea hili zipo, hivyo wakati umefika kwa watu kuwa makini na kazi wanazozifanya, hakuna sababu ya kwenda mwendo kasi wakati unapaswa kutembea kwa taratibu,”alisema.

Hata hivyo, alisema Wizara inaendelea na mkakati wa kuboresha na kufanyiwa marekebisho maeneo korofi na yenye changamoto kama ile ya miteremko mirefu na mikali kuangalia namna ya kuongeza upana wa barabara hizo.

Katika kusisitiza utekelezaji wa sheria, Masauni, amewataka watumiaji wa vyombo vya moto pamoja na vyama vya siasa kuhakikisha wanazingatia na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.

Masaun,  alisema, nchi inaongozwa kwa misingi ya utawala bora kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria hizo, hivyo ni vema jamii na vyama vya siasa vikakaheshimu sheria hizo kwa maslahi ya Taifa.

“Watumiaji wa vyombo vya moto wamekuwa wakivunja sheria za usalama barabarani, baadhi ya vyama vya siasa navyo vinatajwa kukwamisha utendaji kazi wa kikosi cha usalama barabarani wakati wa usimamizi sheria, nawaombeni sana kila mtu atii sheria kwani hakuna aliyejuu ya sheria hizi,”alisema.

Naibu waziri huyo, ameliagiza jeshi la polisi Mkoa wa Mbeya, kuendesha zoezi la ukaguzi wa magari na kwa yale ambayo yatabainika kukiuka sheria za usalama barabarani yachukuliwe hatua.

Alisema, Baraza la Usalama Barabarani, lilitoa muda kwa wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha wanapeleka magari yao kukaguliwa na kupewa stika za nenda kwa usalama barabarani hivyo muda huo umekwisha na kilichobaki ni utekelezwaji wa sheria mama.

Hata hivyo, alisema Wizara kupitia kikosi cha usalama barabarani kinaendelea na utoaji wa elimu kwa watumiaji wa barabara ili kupunguza ajali zinazotokana na uzembe wa madereva.