Home KIMATAIFA Ahukumiwa kunyongwa bila kuua

Ahukumiwa kunyongwa bila kuua

893
0
SHARE

Mwandishi wetu na BBC

Wakati wafungwa na mahabusu katika Gereza la Butimba jijini Mwanza wakimeleza Rais Dk. John Mgufuli, kumbamikwa kesi mbalimbali zikiwamo za mauaji kimeibuka kisa cha mtu aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa bila kuhusika katika kosa.

Taarifa za kisa hicho kwa mara ya kwanza ziliripotiwa jana na Shirika la Habari la Uingereza ambapo, Tete Kafunja, anadai kukubwa na mkasa huo baada ya kwenda kumwekea dhamana kwa rafiki yake aliyekamtwa kwa kosa la kuuza bangi.

Taarifa zinadai kuwa tukio hilo lilitokea mwaka 1990 na kwamba baada ya kufika katika kituo cha polisi alikamatwa na kupewa kesi ya mauaji ya mtu ambaye hata yeye mwenyewe hakuwahi kumwona.

Kafunja alkiyekuwa akifanya biashara ya kuuza vinywaji vyenye kilevi (pombe) katika baa moja eneo la Manzese jijini Dar es salaam wakati anakamatwa alikua na mke na mtoto mmoja ambao hata hivyo hajui walipo hadi sasa.

Inadaiwa kuwa baada ya kukamatwa alikaa gereza la keko kwa miaka 11 kama mahabusu akisubiri hukumu yake dhidi ya kesi hiyo hadi hapo alipohukumiwa kunyongwa hadi kufa mwaka 2003.

Baada ya kuhumu hiyo alikata rufaa kupinga uamuzi huo kwa madai kuwa kesi hiyo haikuwa na ukweli.

“Baada tu ya hukumu, nilikata rufaa maana sijawahi hata kuiona sura ya marehemu, sijui chochote mimi nilienda kumuwekea dhamana rafiki yangu aliyekua amekamatwa kwa kosa la kukutwa na bangi, nikashangaa na mimi nakamatwa kisa sijui nini, baadae ndio nikaambiwa nina kesi ya kuua mtu jambo ambalo ni la kushangaza na sijawahi hata kumuona huyo marehemu” alilieleza shirika hilo.

Alidai kuwa wakati kutekelezwa kwa hukumu hiyo maisha yalikua magumu na walipewa jina maalumu la ‘vipusa’ kwa maana watu wanaolindwa na wanasubiri kufa tu.

”Kwa wafungwa wa kunyongwa, maisha ni magumu sana, unakaa ndani tuu, na kutoka ni mara moja moja wakati wa kuota jua, unaletewa uji asubuhi lakini hata hamu ya kunywa uji hakuna”

Hata hivyo kabla ya kutolewa uamuzi wa rufaa yake alielezwa kuwa anatakiwa kuhamishiwa katika gereza la Isanga mkoani Dodoma tayari kwa kunyongwa endapo kama Rais angeidhinisha kutekelezwa kwa hukumu ya kunyongwa hata kama kesi imekatiwa rufaa.

Mwaka 2008 kesi yake ya rufaa ilisikilizwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Rufaa jijini Dar es salaam, ambapo mwishoni mwa wamaka huo alipoachiwa huru baada ya kukutwa hana hatia.

“Wakati jaji anasema unaachiwa huru, sikuamini kabisa, nikauliza tena nimeachiwa huru? Wakasema ndio ikabidi sasa nirudishwe jela baada ya kibali kutoka nikaachiwa rasmi, sikuamini nilimwomba sana Mungu na kumshukuru kwa maajabu yaliyotekea.

Kafunja anadai kuwa baada ya kuachiwa alikabidhiwa kiasi cha Sh 1,000 kisha akaambiwa aondoke ambapo alifunga safari hadi eneo la Kimara Dar es saalam.

Kutokana na kukaa gerenzani kwa muda mrefu alishangaa kuona jinsi mji ulivyobadilika na kuona magari mengi, jambo ambalo lilikuwa geni kwake.

Anadai kuwa baada ya kufika Dar es Salaam aliitafuta familia yake yaani mke wake na mwanae mmoja lakini akaambiwa walihama na hawajulikani walienda wapi na baada ya kufika mahala alipokuwa akiishi alimkuta mzee mmoja jirani yake ambaye alikuwa mtu pekee aliyekuwa akimfahamu akamweleza kuwa yeye ni Tete lakini mzee huyu akakataa.

“Akakataa akesema Tete yupo gerezani na inawezekana hivi sasa ameshanyongwa, nikamwambia hapana, ni mimi akasema hebu nione mwanya, Tete ninayemjua ana mwanya, baada ya kumuonesha ndiyo akaniamini, nikaanza kumwelezea kisa kizima’” alinukuliwa Kafunja.

Hadi sasa Tete haijui familia wala ndugu zake walipo na kwamba wote walikata tamaa wakiamini kuwa tayari ameshanyongwa.

Kutokana na mateso aliyoyapitia akiwa gerezani anasema hukumu hii ni mbaya huku akishauri ifute ili kuepusha mateso kwa wafungwa ambao hawajui hatma yao.

”Unateseka na kama hujafanya kosa kama mimi, si wote wanaokata rufaa na kufanikiwa, kuna watu wengi nimewaacha jela, hata sura za marehemu hawazijui. Nadhani ifutwe, maisha yangu yameharibika sana na sijalipwa fidia yoyote, sina familia wala ndugu”